Thursday, September 16, 2010

Slaa amuweka pabaya Salma

-Atumia nyenzo za serikali kumkampenia mumewe
-Kinana amtetea
MWENYEKITI wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana amekiri kuwa Mke wa Rais, Salma Kikwete, hutumia ndege za Serikali wakati wa kumfanyia kampeni mume wake, Rais Jakaya Kikwete na wagombea wengine wa chama hicho katika nafasi za ubunge na udiwani.

Hata hivyo, Kinana amemtetea Salma Kikwete kwa kusema kwamba hakuna sheria iliyovunjwa kwa kuwa ndege hizo hukodishwa.

Kwa mujibu wa Kinana, hata mgombea urais wa CCM, Kikwete wakati mwingine hutumia ndege za serikali kwa kukodi pindi inapotokea ndege za mashirika binafsi zinazoaminika kwa usalama zimekodiwa na watu wengine.

Ufafanuzi huo wa Kinana unatokana na tukio la Mke wa Rais, Salma, kuwasili mkoani Mara kwa ndege ya Serikali aina ya Focker 50, yenye namba 5H-TGF na kupokewa na viongozi wa Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa, Enos Mfuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Maram, Robert Boaz, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Geofrey Ngantuni na viongozi wengine wa mkoa na ngazi ya wilaya, wote wakifika uwanjani hapo kwa kutumia magari ya Serikali.

Baada ya kuwasili na kupokewa na wana-CCM uwanjani hapo, tofauti na ziara nyingine ambazo zimekuwa zikitangazwa ili wananchi wajitokeze kumpokea, wakati huu haikutangazwa na hivyo alipokewa na watu wanaoaminika wafuasi wa CCM waliopewa taarifa kwa masharti ya kutotangaza ujio huo.

Kiongozi huyo baada ya kupokewa na kukagua vikundi vya ngoma alipanda katika gari lililokuwa na namba za kiraia aina ya VX V8 Land cruiser T206 BJY lakini linaloaminika kuwa ni la serikali; huku ujumbe wake ukitumia pia magari ya serikali kuelekea Ikulu ndogo, Mjini Musoma.

Akizungumzia hali hiyo, Kinana alikiri Salma kutumia ndege ya serikali na kwamba si katika safari yake ya Musoma tu bali hata alipokwenda Mwanza alitumia ndege ya serikali. Alisema ndege hiyo imekuwa ikikodiwa kutoka kwa Wakala wa Ndege wa Serikali na kwamba mtu yeyote anaruhusiwa kukodi ndege hizo.

“Tumekuwa tunatumia ndege za Serikali kwa kukodi hasa pale ndege za mashirika binafsi ambazo tunaziamini kwa maana ya usalama wake zinakuwa zipo kwenye matumizi mengine. Kwa hiyo hatuwezi kutumia ndege nyingine tusizoziamini kiusalama, na kwa hivyo tunakodi ndege hizo. Tunazo risiti za malipo na mtu yeyote anaweza kukodi ndege hizo,”

“Kuna upotoshaji tu unafanywa na watu ambao wanajua ndege hizo zinaweza kukodiwa na yeyote. Kwa hiyo mgombea wetu wa urais aliwahi kutumia ndege hiyo katika baadhi ya kampeni na Mama Salma ameitumia mara kadhaa,” alisema Kinana na kusisitiza kuwa CCM inatambua vyema masharti ya sheria zote za Uchaguzi Mkuu na haiwezi kufanya kinyume kwa kuwa sheria hizo zimepitishwa chini ya Serikali ya chama hicho.

Hata hivyo, Kinana hakufafanua matumizi ya magari ya serikali katika mikutano ya kampeni ya Kikwete ambayo Mama Salma anaifanya akiandamana na viongozi wa mikoa.

Wakati CCM ikitoa ufafanuzi huo wa matumizi ya Salma Kikwete ya ndege ya serikali, taarifa zaidi kutoka mkoani Mara kuhusu ziara ya mama huyo zinaeleza kuwa, alizuru Wilaya ya Bunda baada ya kumaliza shughuli zake wilayani Musoma.

Akiwa wilayani Bunda alifanya mkutano wa ndani wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na pia ratiba ilimuelekeza kwenda Jimbo la Mwibara, Jumatatu wiki hii, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na eneo hilo kuwapo mgombea wa urais wa CHADEMA, Dk Willbrod Slaa.

Taarifa hizo zinabainisha kuwa pamoja na kuwapigia debe wagombea wa CCM akiwamo mumewe Rais Jakaya Kikwete, Salma amekuwa akijitahidi kufanya usuluhishi wa makundi ili kuvunja kambi zilizoibuka wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Hoja ya ufisadi inayotumiwa kumtambulisha Dk. Slaa ikionekana kumbeba katika taswira ya kukubalika zaidi kwa wapiga kura, imekuwa pia ikitolewa ufafanuzi na Salma Kikwete katika ziara zake hizo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, Salma amekuwa akizungumzia hoja ya ufisadi kwa maelezo kuwa Serikali ya CCM imefanya na inaendelea kufanya kazi kubwa kupambana na vitendo hivyo ambavyo alidai vilikuwapo tangu enzi za TANU. TANU ndiyo moja ya chama kiasisi cha CCM, kikiwa na rekodi ya kuongoza mapambano ya kudai uhuru.

“Jamani hata nyumba haiwezi kujengwa kwa siku moja. Nawaomba sana kuvunja makundi na kuwa pamoja na walioshindwa kura za maoni ili kuhakikisha CCM inashinda na hili ndilo lengo kuu la ziara yangu hapa. Muende nyumba hadi nyumba kueleza mafanikio ya Serikali ya Rais Kikwete ili wananchi watambue pumba na mchele ni upi,” alisema

Soma zaidi

No comments: