Tuesday, September 14, 2010

Mbatia: Kampeni za kashfa hazina tija kwa umma

Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ametoa rai kwa wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa kushindana kwa hoja za kimaendeleo badala ya kashfa zisizokuwa na tija kwa umma.

Mbatia anayewania ubunge wa jimbo la Kawe, alitoa rai hiyo juzi katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.

Alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za NCCR-Mageuzi, uliohudhuriwa pia na mgombea urais kupitia chama hicho, Hashim Rungwe na mgombea mwenza wake, Ally Omary.

Mbatia alisema wagombea hao wanapaswa kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu kila wanapokuwa jukwaani, ili hekima, umoja na amani vitumike badala ya kauli zinazoweza kuchochea chuki.

Mbatia aliwataka wapiga kura kuwa na hekima ya kuchagua viongozi bora na si kuangalia vyama wanavyotoka.

Mbatia alitaja vipaumbele vya ilani ya chama hicho, vikigusia utawala bora, sekta ya uchumi, huduma za kijamii, makundi ya watu maalumu, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na usawa wa jinsia.

Alisema ikiwa NCCR itashinda katika uchaguzi huo, asilimia 30 ya bajeti ya nchi itaelekezwa katika uboreshaji wa elimu.

Mbatia alizungumzia msongamano uliopo jijini hapa na kuahidi kutumia mbinu mbalimbali zitakazofanikisha kuondokana na kero hiyo.

Alisema ikiwa NCCR itapata ushindi serikali itaanzisha usafiri imara wa majini na kujenga gati ufukweni wa bahari.

Alisema usafiri huo utaanzia Bagamoyo-mbweni-Kunduchi-Mbezi beach-Msasani mpaka bandari ya Dar es Salaam.

Pia alisema serikali ya NCCR itaanzisha usafiri wa reli ikiwa ni mojawapo wa njia za kukabiliana na msongamano jijini humo.

Alisema usafiri wa reli utawalenga zaidi wakazi wa jijini kutoka Pugu-Gongolamboto-Vigunguti-Buguruni mpaka kituo kikuu cha kati.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordani Rugimbana na Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: