Friday, September 17, 2010

CUF ikishinda Chenge kukamatwa

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kikichaguliwa kuingia Ikulu, ndani ya siku 11 watamkamata mgombea wa ubunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na kumuweka chini ya ulinzi.

Mkurugenzi wa Siasa na Naibu Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Mbarala Maharagande aliyasema hayo juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la kituo cha basi cha zamani mjini hapa.

Aliilaumu serikali kwa kile alichodai kuwa imewaacha watuhumiwa wa rushwa kuwania nafasi za uongozi za kisiasa jambo linaloisumbua jamii.

“Tayari tumekubaliana kama chama kwamba hatutawavumilia wala rushwa ambao majina yao yameorodheshwa, tutavalia njuga suala hili na kwa kuanza tutamkamata Chenge katika siku kumi na moja baada ya uchaguzi tukiingia madarakani,” alisema.

Maharagande pia alizungumzia hali duni ya maisha ya wananchi sambamba na huduma mbovu za jamii katika jimbo la Bariadi Magharibi ambako mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Juma Duni Haji alikuwepo akifanya kampeni katika vijiji vya Manemhi na Mihango.

Alisema watamshitaki Chenge kwa matumizi mabaya ya madaraka aliyoyafanya wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu kwa kuingia mikataba mibovu ikiwa ni pamoja na ule wa ununuzi wa rada.

“Ni aibu kujua kuwa nusu ya watu wa Bariadi Magharibi hawana viatu hasa katika wakati huu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia na mbunge wenu hafanyi jitihada zozote kuwakwamua katika hili,” alisema Maharagande.

Katika hatua nyingine, Maharagande alimkosoa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kwa maoni yake aliyodai hayakuwa na busara kuhusu baadhi ya ahadi zilizotolewa na wagombea wa urais wa upinzani.

Maharagande alidai Sitta aliidhinisha matumizi ya fedha nyingi katika ujenzi wa ofisi yake na hakutarajiwa kutoa maneno hayo na kulalamika kuwa nchi ni masikini na hakupaswa kutumia kiasi chote hicho cha fedha.

“Tatizo pekee hapa ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa na kutokuwa na vipaumbele, lakini kama tukitumia hekima katika matumizi ya rasilimali zetu, tungefanya makubwa.

“Haileti maana ni kwa namna gani Sitta aliridhia kiasi hicho cha fedha kwa ujenzi wa ofisi yake wakati barabara ya kwenda jimboni humo imejaa vumbi,” alisema.

No comments: