-Baadhi ya siri za unyumba wa vigogo zaanikwa
GUMZO la unyumba wa mgombea urais wa CHADEMA, Dk.Willibrod Slaa na Josephine Mushumbusi, limeibua utata ndani ya familia za vigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na hali si shwari baada ya baadhi ya mambo kuanikwa hadharani, Raia Mwema limebaini.
Suala hilo ambalo tayari limeingia katika mikono ya kisheria, limeelezwa kuwakera baadhi ya wafuasi wa Dk. Slaa wakiwamo baadhi ya viongozi ambao sasa wamebainisha wazi kwamba viongozi wa CCM “wanaishi nyumba za vioo wasirushe mawe.”
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA wakiwamo wanasheria na wanasiasa wamelieleza Raia Mwema kwamba taarifa na matukio yanayoendelea kuhusiana na maisha unyumba wa Dk. Slaa ni ishara tosha ya CCM kukosa hoja dhidi ya mgombea wao na hivyo kutafuta hoja dhaifu zisizo na maana.
Akizungumza na kwa simu kutoka Singida alipo na Dk. Slaa, mwanasheria wa CHADEMA na mgombea Ubunge wa chama hicho Singida Magharibi, Tundu Lissu, alisema ni utamaduni wa CCM wanapoona wamezidiwa kutafuta hoja dhaifu kushambulia wagombea wenye nguvu na kwamba CHADEMA watajibu mapigo ikibidi.
Lissu ambaye amekuwa na historia ya kupambana na Serikali kuhusiana na masuala ya madini, alisema hawaoni sababu ya kujibizana na propaganda za CCM pamoja na kuwa wana taarifa nzito kuhusiana na uchafu wa viongozi wa CCM ikiwa ni pamoja na uchafu huo kuhusisha matumizi ya fedha za umma.
“Hatutaki kujibizana na propaganda zao chafu ambazo wamezizoea tangu kuanza tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 walipomtafuta Angelina kumchafua Mrema (Augustine Mrema) wakati ule Mrema akiwa na nguvu. Lakini lazima tujiulize wana uhakika gani na maisha binafsi na afya za wagombea wao?”
Alisema baada ya kumchafua Mrema mwaka 1995, mwaka 2005 waliibuka na mkakati wa kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa kina nguvu kilikuwa kimeingiza nchini kontena la visu katika taarifa ambayo ilitangazwa na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Omari Mahita.
Alisema pia kwamba ni mambo ya aina hii yaliyoibuka pia mwaka huohuo walipoanza kuchafuliwa wagombea wa urais katika uchaguzi wa ndani ya chama pale mwanadiplomasia Dk. Salim Ahmed Salim na aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye walipochafuliwa na wana CCM wenzao.
Lissu alisema ni viongozi wachache ndani ya CCM wanaoweza kujitokeza hadharani kuzungumzia mahusiano yao ya unyumba na kwamba baadhi yao hawajawahi kuweka wazi kuhusiana na idadi ya wake na watoto walio nao nje ya ndoa zinazofahamika hadharani.
“Je, wako tayari kutueleza idadi ya wake na watoto ambao hawataki wajulikane? Je, wako tayari kutueleza jinsi viongozi wanavyothubutu kuchangia mahusiano bila aibu na baadhi yao kuhusishwa hadi katika uteuzi katika nafasi za chama na Serikali? Wanatutaka tuanze kuwataja hadharani?”, alihoji.
Akizungumzia kesi inayofunguliwa dhidi ya Dk. Slaa na Josephine, mwanamke aliyeibua mjadala, alisema kisheria hawezi kuzungumzia suala ambalo halijamfikia rasmi na kwamba anachoweza kuzungumza ni masuala ya kisiasa tu hadi hapo mawasiliano ya kisheria yakapomfikia.
Lakini habari zilizovuja kutoka CHADEMA zinasema Josephine mwenyewe anajiandaa kufungua kesi mahakamani kudai Sh bilioni mbili kwa kuchafuliwa jina na Lissu alikataa jana Jumanne kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba hana taarifa hizo.
Uchunguzi wa Raia Mwema wiki hii umebaini kuwapo kwa mijadala mizito miongoni mwa watu baadhi ikiwa katika mitandao kuhusiana na maisha binafsi ya viongozi wa juu wa CCM huku majina na picha za wahusika vikianikwa.
Maoni ya baadhi ya waliozungumza na Raia Mwema ni kwamba habari za mahusiano ya unyumba wa watu hazina tija wakati huu kwa vile kwa hakika hakuna atakayesalimika miongoni mwa viongozi wengi zikianza kutangazwa hadharani. Wanatoa mwito kwamba vyombo kama Tume ya Uchaguzi na Msajili wa Vyama viingilie kati kurejesha kampeni katika masuala ya msingi, yaani kero za kweli za Watanzania na Tanzania ijayo.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rajabu Kiravu, alisema ofisi yake haiwezi kuchukua hatua wala kukemea hadi itakapopata malalamiko rasmi kutoka kwa vyama ama wagombea, na kwamba hakuna malalamiko yoyote yaliyokuwa yamewasilishwa kwake.
Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema Baraza la Ushauri la Vyama vya Siasa, limetolea kauli suala hilo bila kufafanua.
Tendwa ambaye ni Katibu wa Baraza hilo, amenukuliwa akisema kwamba baraza hilo limekemea tabia ya baadhi ya vyama kuchafuana badala ya kutangaza sera za vyama husika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Kampeni ya CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, ameliambia Raia Mwema kwamba mgombea wao (Dk. Slaa) anaendelea na kampeni bila kujali propaganda chafu zinazoenezwa na CCM dhidi yake.
“Sisi kwa upande wa mgombea wetu hana muda wa kampeni chafu na badala yake anaendelea kuchanja mbuga na kutangaza sera kwa wananchi na kuwalezea ufisadi wa CCM na Serikali yake na jinsi atakavyowashughulikia mafisadi atakapoingia madarakani,” alisema Profesa Baregu.
Profesa Baregu alisema chama cha siasa ama mgombea anayeanza kujadili mambo binafsi ya mshindani wake anakuwa amepoteza mwelekeo na kwamba ni dalili za kuishiwa kwa hoja.
Akitoa mifano ya Rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton na Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Baregu amesema CCM wameishiwa hoja na kwamba wanazidi kusaidia kumuinua kisiasa Dk.Slaa badala ya kumharibia.
“Wanadhani wamchafua lakini kwa kweli wanatusaidia sana kumpigia kampeni. Mambo binafsi hayana nafasi katika siasa za sasa na muliona mfano wa Clinton na Lewinsky (Monica) na juzi juzi kule Afrika Kusini Zuma aliibuliwa kashfa ya ngono lakini matokeo yake ndiye Rais, na sisi tunaamini Dk. Slaa ndiye ataibuka mshindi,” alisema.
Tayari mtu anayejitambulisha kuwa mume wa ndoa wa Josephine, Aminiel Mahimbo, ameibuka na kulifikisha katika vyombo vya sheria suala hilo akidai fidia ya Sh bilioni moja.
Akizungumzia suala hilo na kunukuliwa na vyombo vya habari, Dk. Slaa alisema hana wasiwasi na kufunguliwa kesi na kutaka Mahimbo aulizwe wakati anaporwa mkewe yeye alikuwa wapi.
Dk. Slaa aliliambia gazeti moja la kila siku kwamba hizo ni kampeni chafu za kutaka kumharibia katika kipindi hiki na kwamba zinafanywa na CCM na kudai kuwa chama hicho kimemnunulia gari Mahimbo ili amchafue.
Tayari Dk. Slaa amekwisha kubainisha kwamba Josephine ndiye mke wake mtarajiwa baada ya kuishi na Rose Kamili na kuzaa naye watoto bila ndoa na kwamba hana tatizo naye, hali iliyojidhihirisha kwa wanawake wote wawili kupanda jukwani kumpigia kampeni.
Rose ambaye alikuwa Diwani wa CCM, amekihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA ambako ameamua kugombea ubunge jimbo la Hanang kupitia chama hicho cha upinzani dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Mary Nagu.
Rose, mwanaharakati na mwanasiasa aliyeiongoza CCM katika Kata ya Basotu Hanang akiwa Diwani kwa miaka 16, ameelezwa kutoa upinzani mkali dhidi ya Dk. Nagu.
Rose alikaa jukwaa moja na Josephine katika kampeni za Dk. Slaa hadi mgombea huyo wa urais alipoondoka Hanang kwenda Mbulu kuendelea na kampeni.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na Josephine wameliambia Raia Mwema kwamba mke huyo mtarajiwa wa Dk. Slaa amebeba siri nzito kuhusu vigogo wa CCM ambao wamekuwa wakifanya naye mawasiliano kadhaa katika siku za karibuni.
“Josephine ana siri nzito ambayo atalazimika kuianika hadharani kwa ushahidi pale itakapobidi na hapo hakutakuwa na wa kulaumiwa,” anasema kwa ufupi mtu huyo wa karibu na Josephine ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
Suala la unyumba wa Dk. Slaa lilianza mara baada ya CHADEMA kuzindua kampeni zake katika viwanja vya Jangwani na kutaja viongozi wa CCM kuwa wanahusika na wizi wa fedha za EPA, kauli ambazo Katibu Mkuu wa CCM Yussuf Makamba alidai kwamba ni matusi dhidi ya viongozi wa chama chao. Makamba ndiye aliyeanza kwa kusema kwamba Dk. Slaa anasumbuliwa na ndoa yake kabla ya yeye kudaiwa kwamba alifukuzwa ualimu kwa aibu.
Chanzo: Raia Mwema
1 comment:
huyu ni mtu mkware hafai kuongoza nchi chadema leteni mtu mwingine huyu aende akgombee umeneja bills club au klabu ya wakware wenzake huko anakojua yeye
Post a Comment