Friday, September 3, 2010

Jino kwa jino CUF, CCM na CHADEMA

-Makamba aambiwa hajui maana ya matusi
-Kashfa ya EPA bado mwiba kwa CCM
WAKATI vumbi la kampeni likiendelea kutimka, Chama Cha Wananchi (CUF) kimelalamikia mwenendo wa kampeni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), malalamiko yanayohusisha kauli za vyama hivyo na matumizi ya fedha.

Mbali na malalamiko hayo, Mgombea Mwenza wa CUF, Juma Duni Haji, amedai kukutana na vituko alivyoviita vya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa Duni Haji, vituko hivyo ni pamoja na kukuta shule yenye Mwalimu mmoja ambaye ndiye Mwalimu Mkuu na alipomuuliza kwa nini anajiita Mwalimu Mkuu, aliambulia kicheko kutoka kwa mwalimu huyo.

Akizungumza na Raia Mwema kwa simu kutoka mkoani Kagera, Msemaji wa Kampeni za CUF, Mbarara Maharagande, alishangazwa na ujasiri wa CCM kutumia mabilioni ya fedha kiasi cha kupindukia kwenye kampeni zake, wakati huduma za jamii zikizidi kuwa duni kwenye maeneo wanakojinadi.

“Athari kubwa ambayo inatukabili ni matumizi makubwa ya fedha kwa upande wa CCM, tupo njiani kuelekea Bukoba Vijijini ni dhahiri fedha nyingi zimetumika na hii ni njia mojawapo ya kukandamiza demokrasia,”

Alipoulizwa kwamba matumizi ya fedha hizo inawezekana ikawa kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi inayotaja kiwango hadi Sh bilioni 50, Maharagande alisema kwa vyovyote vile na hasa kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania, demokrasia inaathirika.

“Wamesambaza mabango kila kona, fulana zitagawiwa karibu kwa kila Mtanzania…najiuliza inakuwaje mabilioni yamwagwe kiasi hicho wakati huduma za jamii kule wanakoenda kuomba kura zikiwa zimezorota. Dawa hospitalini hakuna hata karatasi za kuandika taarifa za wagonjwa lakini karatasi za kampeni zimesambazwa hadi vyooni,” alisema Maharagande na kuongeza kuwa wana matarajio makubwa kwamba Profesa Ibrahim Lipumba mgombea urais kwa tiketi ya CUF atashinda na kuunda serikali licha ya matumizi hayo makubwa ya fedha kwa upande wa CCM.

Katika hatua nyingine, Maharagande alikilalamikia CHADEMA akisema kimekuwa kikitumia lugha za kashfa dhidi ya wagombea wengine bila kujali ni wa CUF au chama kingine.

Alibainisha kuwa kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Wilibrod Slaa kuzungumzia posho, mishahara na mafao ya wabunge kuwa ni makubwa na kutumia ajenda hiyo kwenye kampeni ni usaliti.

Alisema Dk. Slaa ni sehemu ya viongozi waliopitisha mafao hayo kwa kuwa alikuwa Naibu Kiongozi wa Upinzani pamoja na Mbunge wa CUF, Hamad Rashid Mohamed na kwamba Dk. Slaa mwenyewe alichukua mafao na mishahara hiyo ya wabunge anayodai ni mikubwa.

Mbali na kulalamikia hoja hiyo ambayo inaelekea kukikera CUF, Maharagande alisema CHADEMA pia imejihusisha na vitendo vya vurugu dhidi ya chama chake.

“CHADEMA walimshambulia mgombea wetu wa ubunge Tarime (Charles Mwera) na hivi karibuni wametoa lugha za kashfa kwa wagombea wa chama kingine….huu si ustaarabu, tunawashauri waache mwenendo huo,”

Alipoulizwa ni kwa nini ameanza kuwa na mwelekeo wa kutetea wagombea wa CCM ambao hivi karibuni ndio waliodaiwa kushambuliwa na viongozi wa CHADEMA, alisema CUF ina haki ya kutoa msimamo wake kuhusu masuala ya msingi yanayoweza kuathiri mwenendo wa nchi.

Malalamiko dhidi ya CHADEMA yamekwishatolewa na CCM, kupitia mwenyekiti wa kampeni za chama hicho, Abdulraham Kinana, akidai kusikitishwa na maelezo ya wakili mwandamizi nchini, Mabere Marando aliyesema Mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, Rostam Azizi na Edward Lowassa wanahusika kwenye wizi wa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema Jumanne wiki hii, Kinana alishauri CHADEMA watumie hoja kushawishi wapiga kura na si kuzusha kashfa, kuhangaika kuweka pingamizi au kukimbilia mikutano na waandishi wa habari, akisisitiza ni muhimu kukimbilia kujinadi kwa wapiga kura ili kueleweka na kuchaguliwa.

“Siku hizi za awali kwa mujibu wa kampeni zetu kuna kila dalili za ushindi mkubwa kwa sababu tunaeleza tulichofanikiwa kufanya na tutakachofanya tukiendelea kuchaguliwa, wananchi wanatuelewa vizuri,”

“Hali hiyo ni tofauti na wenzetu ambao wanaendeleza yale ya miaka 15 iliyopita ya kufanya kampeni za kuzua kashfa, waeleze watafanya nini,” alisema Kinana.

Katika hatua nyingine, Mgombea Mwenza wa CUF Juma Duni Haji alilieleza gazeti hili kwamba Watanzania waelewe kuwa hata wakiipa CCM miaka mingine 100 ya kutawala hawataweza kuwa na maisha bora.

“Kuna silaha mbili zinazotumiwa na CCM kushinda. Kwanza, masikini na mtu mjinga ndiye anayetawalika. Pili, tajiri hawezi kutawalika. Kwa hiyo wanatambua hizi silaa na wanahakikisha watu wanabaki kuwa masikini na wajinga ili waendelee kutawala.

“Tumefika kwenye shule moja tumekuta ina wanafunzi 900 lakini walimu wanne, kwenye shule nyingine mwalimu mmoja huyo huyo amejiita Mwalimu Mkuu, ukimuuliza kwa nini ajipe cheo hicho anacheka tu,” alisema Duni.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, amemjibu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Kinana, akisema kwamba hakuna kiongozi wala mgombea wa chama chao aliyetoa matusi ama kufanya vurugu bali kinachotokea ni CCM kutapatapa.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu jana, Profesa Baregu amesema anashangazwa na kauli kwamba CHADEMA imetoa matusi na kufanya vurugu katika kampeni zake za hivi karibuni.

“Tangu tulipokuwa kwenye mkutano wa kuzindua kampeni, hakuna mzungumzaji aliyetoa matusi ama kufanya vurugu. Wanashindwa (CCM) kutenganisha kati ya matusi na kusema ukweli, maana kilichozungumzwa ni kwamba kesi za EPA zilizopo mahakamani hazitoshi na waliohusika moja kwa moja hawajaonekana na wakatajwa. Hakuna matusi hapo,” alisema Baregu.

Baregu alizungumzia pia kuhusu kauli ya Makamba kudai kwamba Mgombea Urais wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa haaminiki akisema kwamba hayo maneno hayo ni dalili ya kutapatapa.

“Kuna mazungumzo mengine kama ya Makamba anaposema Dk.Slaa haaminiki na kwamba kaasi dini na kaasi mke wake. Hayo sijui ana uhakika gani? Slaa hana ugomvi na Kanisa Katoliki na ndiyo maana alihusika kupanga safari ya Papa (John Paul II) alipokuja Tanzania.

“Hapa ukweli ni kwamba alishindwa taratibu za upadri na ni uaminifu si ukosefu wa uaminifu ndiyo maana aliomba ruhusa ya Kanisa Roma na akakubaliwa, kusema ukweli ndiyo uaminifu na ndiyo maana alikubalika. Anataka awe mnafiki aende kanisani mchana halafu usiku aende mtaani kubangaiza,” alisema Baregu.

1 comment:

Anonymous said...

Uchaguzi wa mwaka huu kazi ipo, hii ndio demokrasia tunayoitaka!

Mdau,
Shinyanga