KUANZIA Juni mwakani, Serikali haitagharimia watu safari na matibabu ya nje, hasa kwa wagonjwa wa moyo ikiwamo kufanyiwa upasuaji.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na ujenzi wa Kituo cha Upasuaji Moyo, Tiba na Mafunzo kinachojengwa na Serikali ya China katika eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambao unatarajiwa kuchukua miezi 14 kukamilika.
Akiweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kujengwa kwa kituo hicho jana Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alisema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kupeleka wagonjwa wa moyo nje kutibiwa, hali ambayo hata hivyo haikutosheleza mahitaji kutokana na uhaba wa fedha uliopo.
“Tangu uhuru tumetumia fedha nyingi kupeleka ndugu zetu nje, lakini kutokana na uwezo mdogo si wote waliobahatika kwenda kutibiwa, mfano mwaka 2001 kulikuwa na wagonjwa 200 wa moyo na kati yao 156 walihitaji upasuaji lakini ni 60 tu ndio waliopelekwa nje kutibiwa,” alisema Rais.
“Sina uhakika hao wengine zaidi ya 100 waliobaki kama wako hai au wametangulia mbele za haki, kwa kweli inasikitisha na inauma sana. Kutokana na hali hii, ndiyo maana tuliamua ni bora tuanze wenyewe safari ya kujijengea uwezo wetu katika tiba ya maradhi hayo,” alisema
Rais Kikwete.
Alisema anaamini baada ya kukamilika kwa kituo hicho ambacho kitakuwa na wodi 11 na vitanda 36 na Chumba na Watu Mashuhuri (VIP), utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje kutibiwa moyo utakwisha isipokuwa kwa wanaotaka kwa hiari yao kutembea nchi za nje.
Alisema pamoja na hayo, watakaomua kwenda nje hawatakuwa na tofauti na watakaotibiwa nchini, kwa kuwa vifaa, madaktari na huduma hazitatofautiana.
“Ila naupongeza uongozi wa MNH kwa kuanza mpango wa kupeleka madaktari nje kwa ajili ya mafunzo ya magonjwa moyo,” alisema.
Alisema tayari madaktari 26 wamerudi nchini na wameanza kutoa huduma hiyo na hadi sasa wagonjwa wa moyo 160 wamefanyiwa upasuaji ambao umekwenda vizuri bila matatizo, jambo ambalo ni la kujivunia.
Kikwete alisema nchi nyingi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, zimekuwa zikikabiliwa na matatizo makubwa katika matibabu ya magonjwa sugu kama vile kisukari, figo, saratani, moyo na mishipa ya fahamu, jambo ambalo Tanzania inajipanga kukabiliana nalo na kuondokana na adha hiyo.
“Kwa sasa tumeanza kuhangaika kuwa na kituo cha upasuaji wa mishipa ya fahamu ambacho kitakuwa kikubwa na cha kisasa katika nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema.
Aliishukuru Serikali ya China kwa ushirikiano wake ambao umesababisha kujengwa kwa kituo hicho cha magonjwa ya moyo.
“Hii ni faida ya ziara yangu ya mwaka 2006 Uchina ambapo nilikutana na Rais wa nchi hiyo, Hu Jintao, na hata alipotutembelea aliahidi kutimiza ahadi yake hiyo,” alisema Rais.
Naye kiongozi wa ujumbe China, Sun Liang, alisema ujenzi wa kituo hicho ni katika kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na China. “Naamini baada ya jengo hili kukamilika, litatoa huduma bora za upasuaji kwa Watanzania wenye matatizo ya moyo,” alisema Sun.
Alitoa papohapo msaada wa dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo nchini ili wapelekwe nje kutibiwa, wakati ujenzi wa kituo hicho ukiendelea.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema kwa muda mrefu Serikali imejitahidi kupambana na tatizo la kupeleka wagonjwa wa moyo nje ambalo limekuwa likiielemea kutokana na uwezo wake kuwa mdogo.
Alisema kutokana na hali hiyo, walipeleka madaktari 26 nje kwa kujifunza namna ya kutibu moyo na tayari wamerudi na kuanza upasuaji huku Serikali ikijiandaa kupeleka madaktari wengine katika awamu ya pili.
Balozi wa China nchini, Li Xinsheng, alisema kituo hicho ni alama ya ushirikiano wa miaka 46 wa Tanzania na China ambapo pamoja na jengo hilo, nchi hiyo pia imejipanga kutoa misaada mingine katika sekta za elimu, afya na kilimo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Adolar Mapunda, alisema pamoja na kwamba Serikali kwa sasa imetoa kipaumbele katika kilimo na kuanzisha mpango wa Kilimo Kwanza, anaomba pia masuala ya elimu na afya, yaingizwe katika vipaumbele muhimu vya nchi.
No comments:
Post a Comment