SERIKALI imeshauriwa kuongeza fedha kwenye sekta ya kilimo kwa kupunguza matumizi mengine yakiwamo ya posho za wabunge na mafao yao.
Mkulima Zephania Lugembe, alitoa ushauri huo jana wakati akizungumza kwenye mkutano na timu ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, inayotathmini matumizi ya vocha za ruzuku za pembejeo za kilimo wilayani Bariadi.
Lugembe ambaye ni mkulima wa kijiji cha Nyakabindi, alisema “wakati tunapozungumzia Kilimo Kwanza, ni lazima Serikali ione umuhimu wa kuongeza fedha ili kumwinua mkulima.
“Mnazungumzia Kilimo Kwanza, lakini lazima mkumbuke kuwa fedha za kilimo hazitoshi, wakulima wawezeshwe zaidi tuachane na posho za wabunge, kila mara unasikia kuwa maslahi yao yako juu, na hivi karibuni watapewa furushi la pesa Bunge likivunjwa, lakini kwa wakulima fedha ni kidogo,” alisema Lugembe.
Alisema wabunge wanafikiria maslahi ya juu, lakini ni bora Serikali ikaona umuhimu wa kupunguza fedha kwa watunga sheria hao, ili zipelekwe kwa wakulima kuinua kilimo nchini.
Mkulima huyo alitoa ushauri huo baada ya wataalamu wa wizara hiyo kufafanua kwamba bajeti iliyotengwa kwa utaratibu wa vocha nchini isingeweza kutosheleza wakulima wote kupata pembejeo za kilimo.
Lugembe na wananchi wengine waliohudhuria mkutano huo, walilalamika kwamba vocha zilizotolewa kwa msimu huu ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji kwa kijiji cha Nyakabindi ambako wanufaika ni 1,800.
Mbali ya kulalamikia bajeti ndogo katika sekta ya kilimo, wananchi hao pia waligusia ucheleweshaji wa vocha na kutaka kamati za vocha za vijiji zilipwe posho.
Akijibu hoja hizo, Ofisa Kilimo wa Wizara hiyo, Samson Poneja, alisema ni kweli wanufaika wa mfumo wa vocha nchini ni wachache na kwamba hiyo ni moja ya changamoto zinazokabili mfumo huo.
Alisema ni nia ya Serikali kuwapa vocha hizo wakulima wote, lakini kwa sasa bajeti haitoshelezi mahitaji hayo na itaongezwa kadri fedha zinavyopatikana.
Wilaya ya Bariadi ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Shinyanga zinazopata ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha kwa zao la pamba ambapo wakulima huchangiwa asilimia 50 ya bei ya soko ya mbegu za pamba na dawa za kuulia wadudu.
No comments:
Post a Comment