Monday, April 12, 2010

Sitta awaponda wanaosema yeye fisadi

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta amesema, maadui wake kisiasa wameshindwa kudhibitisha madai ya kuwa yeye ni fisadi.

Akizungumza kabla ya kuzindua programu ya Urejeshaji wa maadili kwa Umma (PIRI) unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sitta amesema, kama angekuwa na hata dola moja kwenye akaunti ya nje basi mpaka sasa adui zake wangeweza kuliweka peupe.

“ Maadui zangu wanapenda kunisema kuwa mimi ni mnafiki, na kama ningekuwa na dola moja nje ya nchi wangekuwa wameweka wazi, lakini sasa wameishia kusema natembelea benzi la gharama wakati si mimi ninayenunua, na hata waziri mkuu na Jaji Mkuu wanayo.

“ Pia wanasema kuwa ninaishi kwenye nyumba ya gharama, wameuza nyumba zote na nikipangishiwa wanasema inagharama kubwa.”

Sitta amesema, kama angekuwa fisadi basi angefanya hivyo tangu alipoteuliwa na Rais wa awamu ya Kwanza kuwa Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano mwaka 1974.

“ Nikiwa na miaka 34, niliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano na nikahusika katika kununua ndege za abiria tatu huko Canada baada ya Jumuia ya Afrika Mashariki kuvunjika, tulipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ( kwa wakati huo-Pierre Trudeau) aliniambia kunakamisheni ya dola za Marekani laki 3 na kupewa maelekezo hizo hela ziende wapi.

“ Kwa vile mimi nilikuwa na maadili, nilipiga simu nyumbani na Nyerere alinaimbia fedha hizo zichukuliwe na ndizo zilizosomeshea marubani wa kwanza wa ATC, lakini asilimia kubwa ya viongozi wa sasa wangepata nafasi hiyo fedha hizo zingekwenda mifukoni mwao.

Sitta aliongeza kuwa: “ Nilihusika kusaini mkataba ya ujenzi wa daraja la Salender mwaka 1981, barabara ya Moro-Dodoma mwaka 1983, ningeweza kupata fedha ambazo kwa sasa ningekuwa nawatemea mate, sio kama najivuna, mikataba yote hiyo sikuweza hata kujenga kibada. Mfano wa mikataba mibovu ni ule wa TRL.”

Amesema,kuna haja ya kuanza kufuata misingi iliyoweka na Nyerere inayozingatia usawa, kuwajali na kuwatumikia wanyonge, uadilifu na kuheshimu utu wa mtu bila kujali kabila, rangi, utajiri, jinsia au eneo wanaotoka ambayo imeifanya kuwa kisiwa cha amani na utulivu .

“ Hatuna budi kuidumisha misingi hiyo kwa nguvu zote kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo. Nayasema haya kwa sababu zimeanza kujitokeza dalili na vitendo vya waziwazi vyenye mweleko wa kuibomoa misingi hii ambavyo ni rushwa, ufisadi, ubadhirifu, ubabe katika utawala na kuhubiri siasa za chuki. Vitendo hivi na vingine vimeanza kuzoeleka na kuwa sehemu ya utamaduni,”

Amesema,kwa muda mrefu taifa halikuwa na utaratibu rasmi wa kuandaa viongozi,wakati umefika kwa suala kupewa kupaumbele na uzito unaostahili kwa kuweka utaratibu wa kuandaa viongozi kwa kuwapatia nyezo na mafunzo katika nyanja za maadili, uzalendo na uadilifu.

“ Kizazi chenu kitafaidika na elimu ile, lakini wapo ambao kwa sasa ndio wanaoendesha mambo ya nchi ambao wataweza kutumia nafasi zao kutunga sheria za kukandamiza, na wale ambao wana miaka 40, ili watakapoaachia ninyi basi mambo yawe rahisi kwani kinyume cha hapo mtakapotaka kufanya mabadiliko basi mtaambiwa mnafanya mapinduzi.”

Pia Sitta ametaka programu hiyo ifike kwenye vyuo vya kati kama vyuo vya uwalimu, ufundi kutokana na kuwa navyo vinahusika kuzalisha wanafunzi wengi.

Sitta alisema ni vyema program hii ikafika katika ngazi za chini kama vijijini, kata na halmashauri ambao ndio waathirika wakuu wa mmomonyoko wa maadili.

1 comment:

Anonymous said...

Ninakubaaliana na anayosema Mheshimiwa Sitta na ni kweli ni mtu ambaye ni muwazi katika kuwajibika kwake. hiyo inajulikana kupitia kazi ambazo aalikabidhiwa na taifa kuzifaanya kwani alionesha umakini, uaminifu na uzalendo wa hali ya juu katika kuzitekeleza.

Hata hivyo pamoja na kumsifu kwa utendajikazi wake ambao unaaendelea kudhihirika hata katika nafasi aliyonayo hivi sasa ya uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ningependa kumkumbusha Meshimiwa Sitta kwamba Taasisi anayoiongoza ya Bunge licha ya kuwa ni chombo chenye jukumu la kutunga sheria ili ziweze kuhakikisha kwamba nchi inatawalika kwa misingi ya kisheria, taasisi hiyo imekuwa ni chombo cha unyonyaji kwa watumishi wake. kwa mfano mimi nina kijana wangu aambaye anafanyakazi katika taasisi hiyo licha ya kwamba ameajiriwa akiwa na kiwango cha elimu ya chuko kikuu aamekuwa akilipwa stahilizi ambazo si zake. kijana huyo aamejaribu mara kadhaa kufuatilia hazi zake lakini wenye mamlaka wamekuwa wakionesha ubabe, hasa kutokaana na ukweli kwamba wao wananeemeka na keki kubwa kwa sababu wao ndiyo walioshika mpini wa kisu.

ombi langu kwa Spika Sitta ambaye najua ni mtu anayependa haki na mafanikio ya watu anaowaongoza, ni kwamba ahakikishe anasaidia wafanyakazi wake wa chini hasa kuhusiana na stahili zao kwani wote piaa wana mchango katika mafankio ambayo Sitta ameliwezesha bunge la jamhuri ya Tanzania kuyafikia.

Hayo ndiyo maoni na ujumbe wangu kwa Sitta, ahsante.