Thursday, April 15, 2010

Wabunge wabanwa

SERIKALI imewaagiza watumishi wa umma wasiwape wabunge taarifa za siri za Serikali zikiwemo zinazohusu mambo ya usalama wa Taifa.

Hata hivyo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Philip Marmo, amewaruhusu watumishi wawape wabunge taarifa muhimu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Marmo amesema, wabunge hawaruhusiwi kudai taarifa zinazohusu ulinzi na usalama wa Taifa, mwenendo wa Majeshi ya Ulinzi na Polisi.

“Mkiomba taarifa hizo hamtapewa, alisema Marmo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Vijijini, Damas Nakei (CCM), ambaye alitaka kufahamu mipaka ya mbunge kupewa taarifa kutoka ofisi za umma.

Amesema, mipaka au masharti yaliyowekwa na kifungu cha 10 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, katika kutoa taarifa zinazoombwa na mbunge, ni ombi la kupewa taarifa husika na sharti liwe limetolewa na Mbunge mwenyewe na si mtu kwa niaba yake.

Sheria hiyo pia inasema ombi husika ni sharti lizingatie na kufuata masharti yaliyowekwa na sheria au kanuni nyingine yoyote kwa ajili ya kudhibiti utoaji taarifa kwa watumishi wa umma.

Pia alisema taarifa ambazo mbunge akiziomba anaweza kukataliwa ni zile ambazo hazizingatii na zinakiuka masharti yaliyowekwa na sheria au kanuni nyingine yoyote kwa ajili ya udhibiti wa utoaji wa taarifa husika.

Lakini Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alitaka kufahamu maana ya maneno yaliyoko kwenye sheria hiyo, ya bila kuathiri masharti mengine.

Waziri Marmo alisema masharti hayo ni yanayohusu mambo ya usalama wa Taifa na mengine aliyoyataja, lakini pia akaongeza kuwa masharti mengine ni yaliyoko katika sheria ya uhuru wa kupata habari.

Lakini hata hivyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliwataka wabunge wachangamkie kutumia kanuni ya 81 inayowataka kuwasilisha miswada binafsi na ya kamati hasa wanapoona kuna mambo ambayo yamepitwa na wakati katika sheria zilizopo.

Alisema ni wabunge peke yao ndio wanaweza kuleta mabadiliko katika nchi, kwa kuweka sheria nzuri na kuondoa zilizopitwa na wakati, kwani ndicho chombo pekee cha kutunga sheria.

Lakini alisema kamati zenyewe zimekuwa vyombo vya kupokea taarifa kutoka serikalini na miswada ili kuijadili, badala ya kuibua miswada yao na matokeo yake wamekuwa watu wa kulalamika kuhusu sheria hizo.

“Mkija hapa mnalalamika! Kwa nini wakati sisi ndio tunatunga sheria?” alihoji Spika Sitta.

Kuna madai kwamba, baadhi ya watumishi wa umma wanachomoa nyaraka nyeti za Serikali na kuwapa wanasiasa ambao wamekuwa wakizitumia katika majukwaa yao ya kisiasa.

No comments: