TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) imebaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wanaowania kugombea uongozi katika jamii, kutoa rushwa kwa visingizio vya misaada na hivyo kushawishi wapiga kura.
Hali hiyo imejitokeza hata katika misiba, ambapo baadhi ya wawaniaji uongozi hao, hujitokeza na kushinikiza watambuliwe wao binafsi na michango waliyoitoa, ili kujionesha kuwa ni watu wema na wanaostahili kuchaguliwa na wananchi kuwaongoza.
Kinachosikitisha ni kwamba hata mambo ambayo yalikuwa ni sehemu ya utamaduni na yaliyoheshimika na kutohitaji majigambo na tambo, ndiyo sasa yamegeuzwa sehemu ya kampeni na hasa inapokuwa ni katika misiba.
Wakati huu wa kuelekea uchaguzi, tabia hiyo imejitokeza mpaka kuitia shaka Takukuru ambayo imeanza kuwachunguza watu wa aina hiyo, ambao bila shaka wanajaribu hata kukwepa Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Si siri kuwa wanasiasa wamekuwa wakijipitisha majimboni wakiwamo wanaotaka kuwania kwa mara ya kwanza na wale wanaotaka kurudi bungeni, wakitoa misaada na pole kwa wafiwa na wanaouguza hata kama zamani hawakuwa wakiyafanya hayo.
Upole na ukarimu huu wa sasa, ndio unaotia shaka, wenye lengo la kuwapumbaza wananchi ili waone kuwa misaada misibani, utoaji zawadi za vyakula, vinywaji na nguo, ndivyo vigezo vya kupata kiongozi bora!
Sisi tunaungana na Takukuru kutaka watu wa aina hii wadhibitiwe na ikiwezekana waanikwe ili wananchi wawajue na wasithubutu kuwachagua, kwani ni wazi watu hao hawajiamini na wanajua hawana uwezo, hivyo wanatumia nguvu za ziada kurubuni wananchi.
Kwa upande wa wananchi ni vizuri wasibabaishwe na watu wa aina hii na badala yake waangalie uwezo wa mwombaji kura bila kuangalia ana mali au hana, lakini cha msingi ni kujiridhisha kuwa watakayemchagua ndiye kweli ana nia ya kuwasaidia.
Kumjua mwenye uwezo na asiye na uwezo havihitaji ramli wala dawa, bali atajulikana kwa mchango wake wa tangu zamani lakini pia maadili aliyonayo na si yule anayeomba leo akapewa na kesho akawatupa mkono.
Kiongozi safi ni yule anayeelewa matatizo ya anaowaongoza na aliye tayari kushirikiana nao kuyatatua kwa uwazi bila kuhitaji msukumo wa kivutio au kujifanya mkarimu na mpole; ni vizuri wakafahamika kuwa upole wao ni wa muda mfupi.
Watanzania wanapaswa kuwajua watu na hulka zao, wasije siku ya siku wakajikuta wanachagua chui waliojivika ngozi za kondoo na hatimaye wakajikuta wanalia kwa kufanya makosa katika uchaguzi, waelewe kuwa wanaojipitisha na misaada ya uongo na kweli, ni bora viongozi.
No comments:
Post a Comment