Wednesday, April 14, 2010

Azimio la Arusha litalinda wote

MAGWIJI wa fani mbalimbali za jamii wamekuwa wakikutana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuzungumzia, pamoja na mambo mengine, uwezekano wa kurejesha Azimio la Arusha katika uendeshaji wa siasa na uchumi wa Tanzania.

Makamu Mkuu wa UDSM Profesa Rwekaza Mkandala; Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Issa Shivji; Katibu Mkuu wa zamani wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU, sasa Umoja wa Afrika, AU, Salim Ahmed Salim na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Juma Mwapachu, kwa kutaja magwiji wachache, wote wamezungumzia Azimio la Arusha wakitaka lirejeshwe.

Na Azimio la Arusha wala si kitu kigumu kiasi hicho. Kwa ufupi, Mwalimu Nyerere na wenzake wenye uelewa wa aina moja, waligundua mapema kwamba katika dunia ya ubepari uliokomaa, raia wa kawaida wa nchi ambazo ndiyo kwanza zilikuwa zimejitawala kama Tanzania, asingeweza kufaidi matunda ya uhuru.

Wakaweka misingi ya kuhakikisha kila raia anapata haki na nafasi ya kuishi kama mtu katika nchi yake, hiyo ikiwa ni pamoja na kuainisha ni siasa ya mwelekeo gani Tanzania ifuate. Ujamaa na Kujitegemea yalikuwa ni matunda ya mawazo haya ya kina Mwalimu Nyerere na wenzake.

Kimsingi Azimio la Arusha liliweka miiko kadhaa, lakini hasa ya uongozi. Kwa tafsiri nyepesi, miiko hii ililenga kukabili choyo na ulafi katika mioyo ya waliokuwa na nafasi za maamuzi katika safu mpya za uongozi zilizokuwa zinajengwa, zilizotokana na makovu ya ukoloni uliohimiza matabaka ya kimapato katika jamii.

Wengi wetu, kama alivyopata kusema Mwalimu Nyerere mwenyewe, hatujawahi kuona hitilafu kubwa za Azimio la Arusha lililopatilizwa katika awamu ya pili ya utawala nchini, tena na watu walewale ambao mwanzoni waliliimba kama kasuku.

Lakini tumebahatika kuona hasara kubwa za huo mfumo unaonadiwa sana, mfumo mbadala wa Ujamaa na Kujitegemea ambao leo umesababisha kuibuka kwa pengo kubwa kati ya matajiri na masikini nchini. Mfumo ambao umezua chuki ambayo imeandikwa katika kila uso unaopishana nao, pale uso huo unapohisi ya kuwa wewe u ahueni kidogo, hata kama hiyo ni mara yenu ya kwanza kupishana barabarani.

Na chuki hii inachochewa na ukweli kwamba wengi wa walioshiriki kuua Azimio la Arusha ndio matajiri wa leo. Walizika Azimio la Arusha ili wale, wavune. Wangekuwa wamefanya biashara hahali ungeweza kusema wanastahili utajiri huo, lakini wapi. Wameneemeka kwa mikondo ileile ya umma, ambayo kimsingi ilipaswa kuwanufaisha Watanzania wote.

Hakika haiwezekani Azimio la Arusha la mwaka 1967, miaka sita tu baada ya uhuru, likawa ni lilelile miaka hii ya 2010. Litahitaji mabadiliko ili liende na wakati. Lakini yote kwa yote, yapo mambo ya msingi ambayo hayawezi kubadilika, na haya ni pamoja na maadili ya viongozi na maamuzi yanayotokana na viongozi wa umma wasiokuwa na maadili.

Hivi hatushangai kwamba katika Tanzania na Afrika yote matajiri wakubwa ni wanasiasa?! Na wengi wa hawa wanapoingia katika nyadhifa zao za siasa wanakuwa hawana kitu, hawana biashara wala hawamiliki makampuni. Wape miaka mitano tu katika siasa, basi watakuwa ndio wenye hodhi ya kila kitu na hasa : mali na akili. Wakati umefika tuanze kujadili kwa uwazi jinsi ya kurejesha Azimio la Arusha. Litatulinda wote, wasio nacho na wenye nacho.

Source:www.raiamwema.co.tz

No comments: