Wednesday, September 30, 2009

Sitta ajitoa mhanga kumaliza ufisadi

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ametangaza rasmi kuwa amejitoa mhanga kupambana na ufisadi ili nchi isiangamie.

Sitta amesema, ufisadi nchini ni wa kiwango cha juu hivyo yeye na baadhi ya wabunge wameamua kujitoa mhanga kupambana nao, na hawafanyi mzaha.

Amesema, ufisadi unatisha Tanzania, na kwamba, mafisadi wanaiangamiza nchi.

“Nyinyi vijana mnakua wakati wa mikataba hii mibovu mimi naweza kuwa nimeshakufa kwa wakati huo, ndio maana baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge wanachukia rushwa,” Sitta amewaeleza waandishi wa habari leo mjini Arusha.

Rais huyo wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola amesema, gharama za ufisadi nchini zinaweza kuambukiza vizazi vijavyo.

“Rushwa ni tatizo kubwa katika bara letu la Afrika, wala rushwa wanatumia utajiri wao kuingia kwenye siasa huku wakiwa na nguvu kubwa ya kiuchumi,” amesema Sitta.

Ametoa mfano wa ufisadi huo nchini kuwa ni viongozi wa Serikali kusaini mikataba feki itakayoliingiza taifa kwenye gharama kubwa siku zijazo. Amesema,Tanzania itaonja machungu ya gharama hizo kupitia madeni.

“Sasa tunatumia kama asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kulipia madeni ya nje; lakini kuna uwezekano wa kufikia asilimia 50 kama tutaendelea kuingia mikataba feki na ikifikia hapo tumekwisha.

“Ufisadi umefikia hatua ya juu ndio baadhi yetu hatufanyi utani na tumeamua kujitoa mhanga kupambana dhidi ya wahusika wa ufisadi huo.

Kwa mujibu wa Sitta, mwaka jana Afrika ilipoteza takribani dola za marekani bilioni 20 kutokana na vitendo vya ufisadi. “Kiasi hiki ni kikubwa kwani ni zaidi ya msaada ambao bara hili linapata, hii ni hatari kubwa.

Sitta amesema, mkutano huo wa CPA utalijadili suala hilo la ufisadi wakati watakapokuwa wanajadili moja ya mada zitakazowasilishwa.

Amesema, rushwa ni chanzo cha migogoro mingi Afrika kwa kuwa watu wachache wana utajiri walioupata kwa njia ya rushwa, wananchi wengi ni masikini.

Kwa mujibu wa Sitta, watu wamekuwa wanakasirishwa na ustawi huo kwa watu wachache na hivyo kuwa chanzo cha mapigano na migogoro isiyokwisha katika baadhi ya nchi.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, kitendo cha watu wachache kumiliki uchumi na kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa kunasababisha watu wengi wawe masikini.

Katika mkutano huo baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni Serikali ya mseto, majukumu ya Bunge katika kutoa habari kwa jamii, na mabadiliko ya hali ya hewa.

3 comments:

Anonymous said...

Asante sana mpiganaji mwenzetu katika vita dhidi ya ufisadi, shime watanzania tumuunge mkono ingawa anapigana toka sehemu finyu. Hapa nina maana mpiganaji huyu na wengine wachache wenye Tanzania moyoni wangekuwa na nafasi ya kujigeuza kama wangejiunga na wenzao walioko kambi ya siasa mbadala eti wanaoitwa 'wapinzani'. Sita usiogopeni, jiungeni na safu ya kina Slaa, Zitto, Hamad Rashid, Mbowe, Lipumba n.k. wanaobezwa na chama tawala lakini wanaotugusa mno sisi walalahoi. Mungu awatie nguvu, 2010 mfanye kweli ili pamoja tubadilishe mwelekeo wa nchi hii inayoangamia.

Mahenga

Anonymous said...

Watanzania wote tumuenzi baba wa Taifa mwl JK NYERERE kwa kujitoa mhanga kupiga vita ufisadi.Vita hivi si lelemama.Hakika tukijiachia mno ufisadi utatumaliza.MH Sitta yuko sahihi,lakini atalemewa bila kupata usaidizi kutoka upinzani.MUNGU WETU yu upande wa wapiganaji wa kweli,na haki itatendeka kweupe bila kificho.BWANA AWE NANYI.Vita ni vya BWANA.

Mkereketwa

Anonymous said...

Mungu awatangulie wote mnaopigana vita hivi. Swali moja, tu mheshimiwa Sitta, kama nakumbuka vizuri wakati mbunge mwenzako Dkt. Slaa anazungumzia ufisadi wa BOT ulimkebehi, Je! ili tuweke kumbukumbu sawa, unakubali ulikosea na sasa unapigana vita hivi kwa dhati?