Friday, September 11, 2009

Wazungu wakejeli Serikali ya Kikwete



-Wasema posho zawapofua watendaji
-Wasema inajali wawekezaji kuliko raia

SURA ya Tanzania katika duru za kimataifa imeanza kuchafuka na sasa vyombo vya habari, hususan magazeti barani Ulaya, yameanza kuielezea Tanzania katika tafsiri ambayo ni kinyume cha juhudi za maofisa wa serikali kuinadi kwa madhumuni ya kuvutia zaidi wawekezaji.

Miongoni mwa mambo yanayoandikwa na vyombo hivyo yakiwamo magazeti ya The Guardian, Economist na Financial Times, ni pamoja na urasimu unaokwaza wawekezaji, maofisa wa serikali kupenda posho, serikali kukumbatia wawekezaji dhidi ya wananchi katika baadhi ya maeneo na kusuasua kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki.

Magazeti hayo yamechapisha taarifa kuhusu Tanzania katika matoleo yake ya hivi karibuni kati ya Julai na Septemba mwaka huu likiwamo gazeti la Financial Times lililonukuu maofisa wa kampuni moja ya uwekezaji iliyokusudia kujenga kiwanda cha dawa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na gazeti hilo, inaelezwa kuwa wakati Kamal Kotecha alipoanza mazungumzo ya kujenga kiwanda cha dawa mjini Dar es Salaam ambacho kingezalisha dawa bora na kukuza uchumi, mamlaka zilimhakikishia kwamba dawa hizo zingeidhinishwa ndani ya miezi mitatu.

Leo, zaidi ya mwaka mmoja na nusu na uwekezaji wa dola za Marekani milioni 13, Kotecha bado anasubiri kibali hicho kutoka.

“Huwezi kuwaona maofisa au kupata uamuzi. Siku zote wako katika mikutano,” analalama Kotecha, mfanyabisahara Mhindi ambaye amepata kuishi Jamhuri ya Kongo (DRC) mmiliki wa Zenufa Pharmaceuticals.

Anaongeza: “Unaweza kusema ofisi zetu ziko kwa msajili, kwa kuwa kila siku tuna mtu kati yetu anayekwenda katika ofisi yake (kufuatilia).

“Katika Tanzania, moja ya nchi ya Afrika yenye afueni kidogo katika muundo wa sekta ya utendaji, tatizo si rushwa pekee. Ni aina ya mfumo ambao umekuwa kama taasisi, yaani taratibu za kisheria ambazo huchelewesha muda, ambao umehalalishwa na wafadhili na mashirika ya kimataifa. Lakini pengine chimbuko la hali hii ni utamaduni wa malipo ya posho (per diem)”.

Malipo ya kila siku kwa maofisa wanaohudhuria mikutano na warsha yanayolenga kulipia gharama za safari, chakula na malazi.

Mtumishi mmoja wa Serikali aliimbia kampuni ya Zenufa kisa cha kampuni hiyo kusubiri kibali kwa mwaka na nusu.

Alisema, ya kuwa msajili wa cheo cha chini hupata mshahara wa dola za Marekani 600 (takriban shs 72,000) kwa mwezi lakini akisafiri au akiwa mkutanoni hupata dola 50 (sh zaidi ya 50,000) za Marekani. Msajili mwandamizi hupata mshahara wa dola za Marekani 2,000 au posho ya siku ya dola 200 za Marekani akiwa katika mikutano na kuongeza;

“Ndiyo maana hawashikiki ofisini. Hali hii ni habari ya kawaida. Msomi mmoja alilipwa posho ya kikao kilichofanyika mita chache kutoka ofisini kwake. Alipohoji ni za nini aliambiwa za mafuta, aliposema kwake ni jirani, akaambiwa wasipolipa hakuna atakayehudhuria. ”

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mdudu huyu wa posho haishii serikalini tu bali mashirika yasiyo ya kiserikali nayo yanachangia na hayo hualika wataalamu kutoka serikalini na kuwapa posho nono huku wakwavunja moyo wanaobaki ofisini.

Klaus Leisinger, mkuu wa Novartis Foundation, shirika la misaada la Uswizi alipata mara kadhaa kuomba kufadhili kituo cha mafunzo ya afya (Tanzanian Training Centre for International Health) akajikuta akiambulia patupu.

Anasema: “ Ilikuwa vigumu kuanzisha malengo makubwa kwa kuwa wafanyakazi walikuwa wakilipwa mishahara ambayo ilikuwa lazima ichangiwe na posho za vikao na safari”.

Nalo gazeti la Economist, Septemba 3, mwaka 2009, limeripoti kuhusu kusuasua kwa Tanzania kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki kwamba, Uganda imepata kupitia mapinduzi na hata wakati mgumu wakati wa utawala wa Milton Obote, yote yakijidhihirisha katika umwagaji mkubwa wa damu wakati wa utawala wa Idi Amin, na vipindi virefu vya ukiukwaji wa haki za raia.

Gazeti hilo limeeleza kwamba chini ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Tanzania ilichukua siasa ya ujamaa iliyowafanya watu wake wajikokote katika umasikini lakini wakabaki na mshikamano na amani na Kenya ilishamiri kuendana na dunia, lakini yenyewe ikijidhihirisha kwa matendo ya ukosaji amani na rushwa. Sasa Kenya inaweza kuwa isiyo na utulivu kulinganisha na majirani zake.

Kwa mujibu Economist mwaka 1967 Kenya, Tanzania na Uganda ziliunda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa nia kuanzisha shirikisho lakini hakukuwa na maendeleo ya maana kabla ya jumuiya hiyo kuvunjika mwaka 1977, huku baadhi ya Wakenya wakishangilia, wakifurahi kwamba nchi yao ilikuwa ikiwabeba sana wanachama wengine wa jumuiya.

Hata hivyo, mwaka 1999, mpango huo ulifufuliwa na mwaka 2007 ulipanuka kuzijumuisha Burundi na Rwanda na sasa linaeleza gazeti hilo kwamba wengi wana shaka kama Umoja wa aina ya ule wa Ulaya unaweza kufikiwa katika eneo hili hata kama kuna ahadi ya kuwa na sarafu moja ifikapo mwaka 2015 ili kuwezesha muungano wa forodha kufanya kazi.

Hata hivyo linaeleza kwamba matukio ya hivi karibuni yanaashiria kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na shirikisho lakini Tanzania ndiyo ambayo mara nyingi imekuwa ikikwamisha mambo yasiende katika EAC, ikihofia kufunikwa na Wakenya na Waganda watafuta ardhi na ambao wanaaminika kuwa na elimu zaidi kulinganisha na Watanzania.

Lakini Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, sasa anasema hakuna sababu kwa Watanzanua kuendelea kulialia, bali wajiandae kuingia katika soko la pamoja.

Soko la Mitaji Tanzania, ambalo ni dogo, linaamini katika miaka michache ijayo patakuwa na soko la pamoja la Afrika Mashariki. Kazi si mbioni ya kuanzisha mfumo wa biashara ya pamoja.

Kama Tanzania imekuwa ikibaki nyuma, Uganda imekuwa ikichangamkia sana wazo la kuwa na shirikisho, pamoja na mambo mengine, kwa kuwa Rais Yoweri Museveni ana ndoto ya muda mrefu ya kuustafu akiwa rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Hata Paul Kagame, Rais wa Rwanda, anaelezwa kwamba anafurahia wazo la kuwa na EAC. Ushirikiano wake wa hivi majuzi na Jamhuri ya Kongo (DRC) unalenga kukuza biashara baina ya nchi hizo kwa kutumia soko kubwa la Afrika Mashariki. Anataka kuwa anasafirisha bidhaa za Kongo, zilizoongezewa thamani Rwanda kupita katika mianya ndani ya EAC.

Na Kongo haina tatizo na maono hayo ya Kagame. China ambayo ndiye mwekezaji mkubwa katika DRC inataka mbao, chuma na madini mengine yasafirishwe kupitia bandari za Afrika Mashariki.

Kwa sababu hiyo, na sababu nyingine, Kenya, kwa upande wake inataka kujenga bandari mpya ya kina kirefu karibu na kisiwa cha Lamu, karibu na mpaka wa Somalia. Kwa ajili hiyo baadhi ya maofisa wa Kenya wanasema mikoko na mazalia ya samaki jirani na mahali itakapojengwa bandari hiyo si masuala ya kuzuia kujengwa kwake.

Wanasema bandari hiyo, kiwanda cha kusafisha mafuta na mji mpya vitawekwa mahali ambako havitavuruga urithi na biashara ya utalii ya Lamu. Matarajio ya baadaye ni kuwa na barabara na reli kwenda Mogadishu, Addis Ababa na Kigali bomba la mafuta likileta mafuta ya Uganda na Sudan Kusini.

Fedha za uwekezaji zitakuja kutoka Kuwait na matajiri wengine kutoka katika nchi za Ghuba, kwa njia hii Afrika Mashariki itaunganishwa kuliko ilivyopata kuwa na soko la pamoja litakuwa na maana zaidi.

Na hakika kwa nini shirikisho la Afrika Mashariki lisipanuke nje ya nchi wanachama wa sasa? Likitazamwa kwa maana ya lugha ya maeneo haya, yaani Kiswahili, malori ya bidhaa yatayokuwa yakitoka katika bandari ya Mombasa na mvutano wa kisumaku unaoufanya mji mkuu Nairobi kuwa kitovu cha shughuli nyingi, Afrika Mashariki inasambaa hadi Ethiopia, inahusisha sehemu za Somalia, sehemu ya mashariki mwa DRC na ukanda kaskazini mwa Msumbiji na na eneo lote la kusini mwa Sudan ambayo inatarajiwa kuwa huru ifikapo mwaka 2011 kama kura za maoni za raia wa eneo hilo zitaamua hivyo.

Kuna watu wapatao milioni 126 katika EAC. Likipanuka watu zaidi ya milioni 120 wataongezeka hiyo ikifanya idadi ya watu zaidi ya mara mbili ya nchi kadhaa ndogondogo katika maeneo mengine ya Afrika, idadi inayotosha kulifanya eneo hilo kuvutia zaidi kwa wawekezaji wa nje na kulifanya kuwa na nguvu zaidi katika majadiliano na dunia nyingine.

Lakini wafanyabiashara wakazi bado wana wasiwasi. Kwao shirikisho linaweza kukwazwa na mgogoro wa kibiashara, mapigano ya kikabila au likabanwa tangu mwanzo na wanasiasa wafanyabiashara wenye uchu na urasimu wa watendaji. Hakika kuna maoni m changanyiko.

Nalo gazeti la The Guardian na The Obsever yote ya Uingereza, yalieleza kuhusu uwekezaji katika mbuga ya Loliondo, kaskazini mwa Tanzania kuwa ni kati ya mifano ya Serikali ya Tanzania kutokana na kuwa na njaa ya “dola za Marekani” inakumbatia zaidi wawekezaji kuliko wananchi wake, na inathamini wanyama wanaovutia watalii wengi kuliko kuthamini wananchi.

Katika machapisho hayo yaliyoandikwa na waandishi waliofika eneo la Loliondo, imewekwa bayana kuwa licha ya malengo ya serikali kujiongezea mapato kutokana na sekta ya utalii, lakini maisha ya wenyeji katika maeneo ya uwekezaji ni duni, na hakuna uhusiano mzuri kati ya wawekezaji na wenyeji.

Kwa mujibu wa habari hizo, wamasai ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiendeleza utamaduni wao wa ufugaji kwenye ardhi yao, kwa vizazi na vizazi, sasa wanatakiwa kuhama maeneo hayo ili kuwapisha wawekezaji mamilionea, kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kitalii.

“Nikiwa katika eneo la umasaini, simu yangu inasoma ujumbe unaonikaribisha katika Jamhuri ya Kiarabu (United Arab Emirates).

“Ni ujumbe unaosema furahia mtandao bora zaidi wa simu na huduma nyingine wa Etisalat," "Furahia uwapo wako hapa Jamhuri ya Uarabuni!"

Ni eneo ambalo wenyeji wamelipachika jina la Uarabuni. Ni eneo yalipo makao makuu ya Shirika la Biashara la Ortelo (OBC), kampuni inayohusika na masuala ya utalii ambayo haijawekwa katika matangazo ya tovuti.

Ilianzishwa mwaka 1993 na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Uarabuni (UAE) yenye uhusiano wa karibu na familia ya kifalme, Dubai.

Ni kampuni ambayo pamoja na mambo mengine ni mahsusi kwa ajili ya kuwapokea masheikh na mamilionea wa kiarabu ambao hufika Kaskazini mwa Tanzania kupumzika, eneo la Loliondo.

Katika habari iliyoandikwa na gazeti la The Obsever la Uingereza, Loliondo inaelezwa kama eneo la kuvutia ambalo “kutokana na njaa ya dola (fedha) kwa serikali ya Tanzania limetolewa kwa wawekezaji wa kigeni.

“Mkakati wa maendeleo wa Tanzania unaeleza kuwa ni lazima idadi ya watalii wanaotembelea nchi hiyo ifikie watalii milioni moja mwaka 2010.

“Ni dhahiri kuwa maofisa wa serikali wanafanya chochote ili kuhakikisha malengo hayo yanatimia. Takriban robo ya eneo la nchi limetengwa kwa ajili ya kile kinachoitwa hifadhi.

Maili chake kutoka kilima kilichopewa jina la “Uarabuni” kuna shughuli nyingine za kijasiriamali zinazoendelea zikihusisha wajasiriamali wa kiarabu.

Kuna eneo la hekari 12,000 lililotengwa kwa ajili ya hoteli na kupiga kambi kwa watalii. Eneo hilo limetolewa kwa mwekezaji ambaye shughuli zake zinaunganishwa kwa jina la kikampuni la Thomson Family Adventures.

Utoaji wa maeneo hayo umekuwa ukilalamikiwa na wenyeji ambao ni wamasai wakidai hawana maeneo ya kulisha na kunywesha mifugo yao.

Lakini mwekezaji huyo amekuwa akikanusha madai ya wenyeji hao akisema; "Wamekuwa wakipewa huduma ya maji ya visima wakati wa kiangazi.” Imeripotiwa kuwa kwa miaka miwili sasa, kumekuwapo na mashambulizi hata ya kutumia risasi kati ya walinzi wa mwekezaji huyo na polisi dhidi ya wenyeji.

Liz McKee, ambaye ni Meneja Mkuu wa shughuli za mwekezaji huyo amenukuliwa akimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa mradi unaokusudiwa kuanzishwa utahifadhi ardhi na wanyama.

Haamini kwamba ni busara kuwaacha wafugaji kuendelea na mfumo wao mkongwe wa maisha uliodumu kwa karne kadhaa.

Hakuna ardhi ya kutosha, sidhani kama wamasai wataendelea na maisha haya ya kufuga kwa kuhama hadi mwisho wa dunia.” Anasema mwanamama huyo mwenye asili ya Uingereza.

McKee ni mtu ambaye aheshimu kwa asilimia 100 utamaduni wa kimasadi na hasa unaohusu tabia dhidi ya wanawake ikiwamo ya kuoa watoto wadogo hata wenye umri wa miaka 12.

Ni wazi kuwa sasa utamaduni imara wa wamasai unaanza kunyongwa kisayansi. Serikali ya Tanzania imekuwa karibu zaidi na wawekezaji wa kitalii, huku wamasai wakilalamika kuhamishwa kwa nguvu kwenye makazi yao ya asili.

Taarifa hizi zinanukuu matamko ya wanaharakati nchini kwamba kati ya miezi ya Julai na Agosti, mamia ya wamasai walichomewa nyumba zao za polisi ikiwa ni majibu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya wamasai kuingiza mifugo yao eneo la mwekezaji wa kiarabu.

"Wamasai wanaonekana kuwa wanahitaji katika kupigwa picha na watalii, kubeba mabegi ya watalii, au hata kuwalinda," anasema Moringe ole Parkipuny, ambaye ni mzee wa kimasai aliyewahi kuwa mbunge na kuongeza kuwa; "Siku hizi wanyama wanakuwa na thamani zaidi kuliko watu."

Hapa, wamasai wanatakiwa kuhama kwa amri ya serikali ili kupisha nyati 25 ambao ni kivutio kwa mamia ya watalii ndani ya mbuga ya Ngorongoro.

Ololosokwan ni mkazi wa umasaini ambaye alituhadithia kuhusu uvumi kuwa Sheikh kutoka Dubai atawasili hivi karibuni katika Shirika la Ortelo.

Kumekuwapo na maelezo kutoka kwa wenyeji kuwa kila wanapokuja wageni maarufu kutoka Uarabuni hutandikiwa zulia jekundu. Mwandishi aliyekuwapo huko alitaka kujua kama anaweza kupiga picha na alipowaeleza nia yake hiyo, alijibiwa; "Watu hukamatwa wanapokaribia eneo hilo.”

Inaelezwa kuwa kampuni ya OBC imepewa leseni ya kuua simba watano kwa msimu. Lakini swali linakuja nani anayehakikisha idadi hiyo? Anahoji mkazi mmoja wa kijiji jirani na Jamhuri ya Kiarabu, Loliondo.

Waandishi wa habari na watu kutoka Mashirika yasiyo ya Serikali (NGOs) wamekuwa wakipigwa marufuku kufika eneo hilo na hata wenyeji wamekuwa wakionywa na polisi kuwa hata kuzungumzia kwa ubaya kuhusu OBC kutawatia kwenye matatizo.

Mfugaji mmoja wa kimasai alieleza kuwa amekwishawahi kuona mtego wa kutega chui wakiwa hai, ikielezwa kuwa wamepewa kibali hicho na serikali.

Inadaiwa kuwa msimu uliopita wa kiangazi, kijana wa kimasai mwenye umri wa miaka 29 alikufa kutokana na ajali, lakini ilidaiwa kuwa kijana huyo alipigwa risasi na baadaye kugongwa kwa gari ili kuzima joto la vurugu ambalo lingeweza kuibuka kutoka kwa wenyeji.

Hata hivyo, kampuni ya OBC imekuwa ikitoa misaada ikiwamo ya mahindi ili kukabili tatizo la njaa lililokuwa likiwakabili wenyeji. Inaelezwa pia kwamba kampuni iliwahi kutoa shilingi milioni 25 lakini baadhi ya wanavijiji walikataa fedha hizo.

"Hatukushirikishwa wakati waarabu wanapewa maeneo haya," anasema Kirando ole Lukeine, mmoja wa wazee wa kimila na kuongeza kuwa; "Kwa hiyo, kijiji chetu hakitaji msaada wowote kutoka kwao.”

Mzee mwingine wa kimasai anasema; “Tunaeleza ni lazima tuitii serikali lakini hizi ni mbinu tu za kutaka kuchukua sehemu nyingine ya ardhi yetu."

Kumekuwapo na madai kuwa maofisa wa serikali wakiwamo baadhi wanaoshughulikia masuala haya wamekuwa na ukwasi wa kupindukia. Takwimu za rushwa zinaonyesha kuwa Tanzania ambayo mwaka 2008 ilikuwa nchi ya 102 kati ya 180 zilizokithiri kwa rushwa, iliambulia dola za Marekani milioni 9.3 mwaka 2002, kutokana na masuala ya uwindaji kwa leseni.

Hata hivyo, taarifa za waandishi wa kigeni zinaeleza kuwa licha ya mapato hayo hali ya umasikini miongoni mwa wenyeji ni duni.

Mchakato wa kuhamisha wafugaji una historia ndefu nchini Tanzania, ikiwa ni mpango ulioanza mwaka 1959, wakati huo mpango huo ukiendeshwa na serikali ya kikoloni kutoka Uingereza.

Baada ya uhuru, mwaka 1961 hifadhi nyingi za taifa zilianzishwa, uanzishwaji ulioambatana na kuhamisha wenyeji kwenye maeneo husika.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya wananchi ni masikini wa kutupwa, na asilimia 15 ya watoto wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa na umri chini ya miaka mitano.

Hata hivyo, licha ya takwimu hizo mbaya inaelezwa kuwa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka na hivyo kuongeza mapato ya serikali.

Liz McKee, amekuwa akielezea matarajio yake kama mwekezaji kuwa wenyeji watapata ajira kutokana na kuanza shughuli kwa kampuni anayosimamia, ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwakani.

McKee ndiye aliyemwalika mwandishi wa jarida la The Observer kutembelea kampuni yake na kumhoji meneja mwenyeji, Daniel Yamat.

Hata hivyo, kutokana na maelezo hayo ya kupatiwa ajira, mwandishi kabla ya kufuatilia mwaliko huo alitaka kujua maoni ya mwenyeji, Lesingo Ole Nanyoi, kama yuko tayari kupewa ajira, naye alimjibu; hapa, hilo haliwezekani.

Lesingo ambaye ni baba wa watoto wanne akiwa na wake wawili, wakati mwingine amekuwa akilazimika kuuza ng’ombe wake ili kupata fedha za kuendesha familia yake ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za matibabu.

Source:wwww.raiamwema.co.tz

No comments: