KANISA Katoliki nchini limepuuza makaripio na kejeli zinazotolewa na wanasiasa na baadhi ya viongozi wa dini nyingine kuhusu waraka wao unaozungumzia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Raia Mwema limebaini.
Kwa wiki mbili sasa, Raia Mwema limebaini kwamba kila baada ya sala katika makanisa yote Katoliki nchini, viongozi wa Kanisa hilo wamekuwa wakiwatangazia waumini wake ambao hawajaupata waraka huo kuununua nje ya makanisa hayo.
Maeneo ya nje ya makanisa yote ambako huuzwa maandiko ya kiroho, rozali na vitu vinginevyo kumekuwapo na vijitabu hivyo vya waraka ambavyo vimeendelea kuuzwa kwa wingi kuliko ilivyokuwa awali kabla ya makemeo kutolewa.
Joseph Ibreck, Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT), ambacho ndicho kilichochapisha waraka huo ameiambia Raia Mwema wiki hii kwamba wao wanaendelea kuchapisha na kusambaza waraka huo bila kujali wanaopinga.
Ibreck amesema kila siku mahitaji ya warakara huo uliogawanywa katika vijitabu vitatu yamekuwa makubwa na wamekuwa wakiendelea kuchapisha na kusambaza nchi nzima na hivi karibuni walichapa nakala zaidi ya 7,000.
Miongoni mwa walioonekana kutoridhishwa na waraka wa Wakatoliki ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na mwanasiasa mkongwe ambaye amekuwa karibu na watawala kwa muda mrefu, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Akijibu maswali ya wananchi moja kwa moja kupitia televisheni na redio, Rais Kikwete alisema matamko ya kidini yanayohusu uchaguzi ujao yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa dini yamemshitua na ameamuru kuanzia sasa asiwepo kiongozi mwingine wa kidini atakayetoa matamko ya namna hiyo.
Lakini kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki, ameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba kwa sasa wameamua kufunga mjadala wa suala hilo na watawapuuza wote wanapingana nao kwa kuendelea kuusambaza kwa nguvu nchi nzima.
Akijibu moja ya swali liloulizwa Rais Kikwete alisema hatua hiyo ya viongozi wa kidini ya kutoa matamko ni jambo ambalo sio la kawaida kwani yanawataka Watanzania waende kwenye uchaguzi wakiangalia wagombea wa dini zao na sio Utanzania wao, maelezo ambayo yanapingwa na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini.
Rais Kikwete alibainisha kwamba suala hilo limejadiliwa hata ndani ya vikao vya CCM hususan Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) iliyokutana mjini Dodoma hivi karibuni akisema:
"Hili tumeliona kwenye kikao cha NEC, tukaona halituweki kwenye mwelekeo mzuri, Taifa hili waasisi wake wamelijenga si kwa kutazamana dini, rangi au kabila bali Utanzania."
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment