Friday, September 4, 2009

Wabunge kutetea msimamo Kamati ya Mzee Mwinyi

-Wakataa viapo vyao kugeuzwa kiini macho
-Wasema wananchi ni makini kuliko vigogo

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kujipanga kutetea msimamo wao wa kutaka mijadala ya ufisadi iendelezwe wazi wazi, na wahusika wachukuliwe hatua badala ya kuwalinda, pindi watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Wabunge hao wameahidi kuwa na msimamo unaowiana na matakwa ya Katiba ya Tanzania, waliyoapa kuilinda na kuitetea. Wamebainisha kuwa, itakuwa fursa nzuri kwao kutetea Katiba kwa mujibu wa viapo vyao, mbele ya kamati hiyo iliyoundwa kwa matakwa ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, ikiwashirikisha Spika wa zamani, Pius Msekwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdurahman Kinana.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa kiu ya wabunge hao kukutana na kamati hiyo imekuwa kubwa na hasa kwa upande wa wabunge wasiopendezwa na juhudi za kutaka kufunika mijadala ya ufisadi badala ya kuwachukulia hatua wahusika.

Wabunge waliozungumza na Raia Mwema bila kutaka kutajwa majina yao kwa madai kuwa wakati wa kuwasilisha hoja hizo bado, wameeleza kuwa tayari kuchambua kwa kina namna ambavyo chama na serikali yao inavyojitenga na wananchi kutokana na kuwapo kwa juhudi za kulinda watuhumiwa wa ufisadi, na kuzima mijadala ya namna hiyo.

Kwa mujibu wa wabunge hao, tayari matokeo ya hali hiyo ya kuzuia mijadala ya wazi ya ufisadi yamekwishajitokeza katika kampeni za chaguzi ndogo Tarime, Mbeya Vijijini, Busanda na Biharamulo, ambako vyama vya upinzani vimekuwa vikiinadi CCM kuwa ni chama chenye ubia na watuhumiwa wa ufisadi.

“Kwa kadiri unavyozuia wabunge wa CCM kuzungumzia ufisadi kwa kuulani au kutaka wahusika wachukuliwe hatua, ni wazi unapeleka ujumbe kwa umma kuwa chama kama taasisi kinakubaliana na matendo ya watu hao. Hatua hii ni kunufaisha vyama vya upinzani. Ndani ya vyama vya upinzani hakuna kuzuiana kupinga ufisadi.

“Ndiyo inaeleweka kwamba unapozungumzia ufisadi maana yake unagusa watendaji wa chama na serikali ya CCM. Wanachoshindwa kuelewa hapa ni kuwa wanaoguswa ni hao watendaji na si serikali au chama kama taasisi. Kwa hiyo hukibomoi chama au serikali bali unabomoa wanaonufaika na ufisadi na kukiacha chama au serikali salama. Binafsi, napenda ieleweke kuwaandamana watuhumiwa wa ufisadi ili waache si kukiandamana chama, ni kukiimarisha chama,” alisema mbunge mmoja kutoka Tanga.

“Kuna viongozi wetu katika CCM bado wanaamini wananchi ni mbumbumbu, hawawezi kuelewa uchafu wa kifisadi wanaofanya eti wakitaka sote katika CCM tuwalinde, hili haliwezekani. Kutopinga ufisadi hadharani maana yake ni kuimarisha vyama vya upinzani majukwaani,” alisema mbunge mwingine kutoka mkoani Iringa.

Mbunge mwingine kutoka Ruvuma ameiambia Raia Mwema kuwa; “Sitegemei kuona wabunge wenzangu wakikubali kuruhusu viapo walivyokula kuilinda na kuitetea Katiba inayolinda maslahi ya wananchi wote, vikigeuzwa kuwa ni viapo kiini macho. Kama watafanya hivyo Mungu na Watanzania hawatawasamehe.”

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge wamedhamiria kuweka bayana vielelezo kadhaa vinavyothibitisha kulinda ufisadi si malengo ya CCM, na hujuma za kuhakikisha mijadala ya ufisadi inafungwa pia ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Tanzania, waliyoapa kuilinda.

Lakini wakati wabunge hao wakijipanga kwa staili hiyo, Raia Mwema imebaini kuwa ingawa wiki tatu zimepita tangu kuundwa kwa kamati hiyo itakayochunguza kile kilichoitwa “uhusiano mbovu” miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawaziri, msingi wake ukitajwa kuwa ni Spika Samuel Sitta kutoa uhuru mkubwa kwa mijadala ya ufisadi bungeni na hivyo kukidhoofisha chama hicho na serikali yake, hakuna taarifa zozote rasmi zilizowasilishwa ofisi ya Bunge kama mdau mkuu, na hasa kuhusu ratiba ya kukutana na wabunge.

Kamati hiyo ambayo inatarajiwa kukutana na wabunge wa CCM pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kusikiliza maoni yao na hata kubaini chanzo cha mpasuko kati yao na serikali, bado haijaweka bayana utaratibu wake wa namna ya kukutana na wawakilishi hao wa wananchi, ingawa taarifa zinaeleza kuwa huenda wakakutana na wabunge katika mkutano ujao wa Bunge, mjini Dodoma.

Mkutano ujao wa Bunge unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Oktoba na kuendelea hadi katikati ya Novemba, mwaka huu. Ni katika mkutano huo ambapo serikali italazimika kuwasilisha taarifa yake kuhusu hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wa serikali waliobainishwa na Kamati Teule ya Bunge kuwa wawajibishwe.

Serikali itawasilisha taarifa hiyo kutokana na taarifa yake ya awali kukataliwa na Bunge ikiwekwa bayana kuwa, kilichofanyika katika taarifa hiyo si utekelezaji bali uchunguzi uliolenga kuwasafisha wahusika na si kuzingatia hali halisi inayotawaliwa na matakwa ya sheria.

Katika kikao cha NEC wiki tatu zilizopita, iliripotiwa kuwapo kwa mjadala mkali kuhusu uendeshaji wa Bunge, huku wajumbe wengi wakionekana kuchoshwa na utendaji kazi wa Spika, na hasa uamuzi wake wa kuachia uhuru mpana zaidi wa mijadala ya ufisadi bungeni.

Wajumbe wengi waliochangia katika mkutano huo walimwelezea Spika kama mtu anayestahili kuvuliwa uanachama kwa kuwa utendaji kazi wake unakidhoofisha chama na serikali yake.

Imeripotiwa kuwa kati ya wajumbe hao ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Kingunge Ngombale-Mwiru pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

Hata hivyo, hoja za wajumbe hao na wengine ambao majina yao hayajaorodheshwa hadharani zilipingwa vikali na wanachama wengine wa CCM nje ya mkutano huo na hata wanataaluma wengine wasio wanachama wa chama hicho.

Wengi waliopinga vitisho vya kumnyang’anya kadi ya CCM Spika Sitta walidai kuwa hatua hiyo ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 100, inatamka kuwa masuala ya Bunge hayapaswi kuhojiwa nje ya chombo hicho.

Hata hivyo, licha ya upinzani huo, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati kwa nyakati tofauti walijitokeza hadharani ili kutetea uamuzi huo, na kusisitiza kuwa “wanajeuri ya kumwita na kumhoji Spika.”

Wakati Makamba akitamka kuwa wanajeuri ya kumwita na kumhoji Spika, Chiligati alifafanisha uendeshaji wa midajala bungeni kuwa wakati mwingine ni sawa na kundi la wasanii wachekeshaji.

Kauli hizo za Makamba, Chiligati na hata ile ya Mkuu wa Idara ya Propaganda ya CCM, Hiza Tambwe zilimfanya Spika, Samuel Sitta, akiwa jimboni kwake Urambo Mashariki kulalamika kuwa viongozi hao wamekuwa wakiingilia majukumu ya Kamati ya Mzee Mwinyi.

Kwa mujibu wa Spika, kauli hizo zilikuwa zikiingilia utendaji wa kamati hiyo kwa kuwa tayari zilikuwa zikiegemea zaidi upande mmoja kati ya makundi yanayopaswa kusikilizwa malalamiko yao na kamati Mwinyi.

Uamuzi wa kikao hicho cha NEC uliambatana na matukio mbalimbali ya kisiasa, ikiwamo madai ya Spika kuwa mapokezi yake mkoani Tabora yalihujuiwa na baadhi ya viongozi CCM makao makuu.

Pia baada ya kikao hicho kuliibuka madai mazito ya wajumbe wengi wa NEC kuhongwa fedha na kundi la mafisadi ili kuhakikisha Spika anavuliwa uanachama na pale mkakati huo ulipokwama, taarifa zilieleza kuwa kundi hilo lililotoa fedha limechukizwa na mpango huo kufeli.

Madai ya Spika kuandamwa yalianzia katika mkutano uliopita wa Bunge, ambako alifikia hatua ya kuomba ulinzi serikalini na kuweka bayana kuwa maadui zake kisiasa wamekuwa wakimwandama hadi jimboni kwake ambako fedha nyingi zimemwaga na akiwahimiza wananchi kutumia bila kusita fedha hizo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba mnipe ulinzi zaidi, hii vita ni ngumu na kubwa sasa. Ulinzi mnaonipa ni dhahiri kuwa hautoshi,” alilalamika Spika Sitta, katika moja ya vikao vya mkutano uliopita wa Bunge.

Kumekuwapo na hali ya kutoridhishwa na mwenendo wa vikao vya NEC, hali ambayo ilianza kujitokeza tangu kikao cha Juni, mwaka jana, mjini Dodoma.

Source:www.raiamwema.co.tz

No comments: