Thursday, September 24, 2009

Waliomuua albino kunyongwa

MAHAKAMA Kuu Tanzania wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, leo imewahukumu kifo wanaume watatu waliopatikana na hatia ya kumuua mtoto albino wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 14.

Jaji Gabriel Lwakibalira amewahukumu washitakiwa hao kwenda jela na wanyongwe hadi wafe.

Masumbuko Madata (32) mkazi wa Itunga, Emmanuel Masangwa (28) wa Bunyihuna na Charles Kalamuji ‘Charles Masangwa’ (42) wa Nanda, Bukombe , wamepatikana na hatia ya kumvamia, Matatizo Dunia,wilayani Bukombe mkoani Shinyanga wakamkata miguu.

Kwa mujibu wa Jaji Lwakibalira, mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi 15 katika kesi hiyo ya mauaji namba 24 ya mwaka 2009 hivyo washitakiwa hao wanastahili kunyongwa.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban saa moja, Jaji Gabriel Rwakibalila, amesema, mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa kuwa washtakiwa hao watatu walikula njama na kufanya mauaji hayo usiku wa kuamkia Desemba mosi mwaka jana, katika Kijiji cha Bunyihuna, Bukombe.

Jaji Rwakibalila awali alisema ushahidi wa upande wa utetezi uliotolewa mahakamani hapo ulionesha kuwa washtakiwa hawakuwapo, lakini ni utetezi huo huo ulioonesha kuwa ushahidi wao ni wa kweli na ndio waliokula njama na kufanya mauaji hayo.

Amesema, dosari ndogondogo zilizooneshwa na upande wa mashitaka haziharibu mashitaka yaliyokuwa yanawakabili washitakiwa hao.

Baadhi ya dosari ni ushahidi wa idadi ya askari na magari yaliyofika eneo la tukio.

Amesisitiza kwamba, ushahidi wa upande huo unatosha kuwatia hatiani washitakiwa hao na kustahili adhabu hiyo.

Kuhusu ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali alisema nao ulionesha kuhusika kwa mshitakiwa wa kwanza, Madata na wa tatu Kalamuji katika mauaji hayo, hasa baada ya kupatikana kwa vinasaba ambavyo damu ya miguu yote miwili ya albino Dunia ilipochukuliwa, iligundulika kuwa na vinasaba hivyo.

Jaji Rwakibalila alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulionesha jinsi washtakiwa wote watatu walivyoshiriki katika mauaji hayo na ndiyo maana mahakama ikawatia hatiani.

“Mshtakiwa wa kwanza, Masumbuko Madata, mshtakiwa wa pili Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji au Charles Masangwa, nyote kwa pamoja mmepatikana na kosa la mauaji, hivyo mahakama inawahukumu kunyongwa hadi kufa na mnaweza kukata rufaa kama hamridhiki,” alihitimisha kusoma hukumu hiyo.

Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa, upande wa utetezi ulidai kuwa utakata rufaa Mahakama ya Rufaa.

Kesi nyingine za mauaji ya albino zinaendelea katika Mahakama Kuu Kahama na Shinyanga. Wakili kiongozi wa upande wa utetezi, Kamaliza Kayaga, alisema hawakuridhika na hukumu na kwamba kazi yao ni moja ya kukata rufaa.

Hii ni hukumu ya kwanza kutolewa nchini dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya albino tangu kuibuka kwa vitendo hivyo kwa imani za kishirikina na kusababisha vifo vya zaidi ya albino 50 nchini.

No comments: