Tuesday, September 1, 2009

EPA yazaa deni jipya

SERIKALI imetakiwa kuilipa Benki Kuu Tanzania (BOT) deni la sh bilioni 135 lililosababishwa na hasara iliyotokana na matatizo ya uendeshaji wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), iliyokuwa katika benki hiyo.

Serikali imekubali kubeba mzigo huo lakini imekiri kushindwa kulilipa kwa mara moja hivyo imeamua kuanza kulipa deni hilo taratibu huku ikichajiwa riba ya asilimia 8.5 mpaka mwaka 2028.

Taarifa za kuaminika zimebainisha kuwa benki hiyo imepata hasara hiyo baada ya kulazimika kuwalipa waliokuwa wakidai fedha zao zilizohifadhiwa katika akaunti hiyo kwa vipindi tofauti vilivyokuwa na viwango tofauti vya ubadilishanaji wa fedha za kigeni kati ya mwaka 1985 na Juni 30, mwaka jana.

Kukiri kwa Serikali kwamba hasara hiyo italipwa, kumeifanya benki hiyo itarajie kujipatia pato litokanalo na riba hiyo la Sh bilioni 10.8 kwa mwaka, ambayo ni tofauti na malipo ya deni hilo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, BoT imepeleka taarifa kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, ikimkumbusha kuwa jukumu la uendeshaji wa EPA iliyokuwa NBC, lilikuwa la Serikali na hivyo hasara yake haistahili kubebwa na benki hiyo.

BoT imemkumbusha Mkulo kuwa mwaka 1985, benki hiyo ilipewa dhamana ya kusimamia akaunti hiyo kwa niaba ya Serikali na hivyo ikalazimika kuihamishia akaunti hiyo kutoka NBC kwenda BoT. Taarifa hiyo ambayo 'HabariLeo' inayo, iliendelea kueleza kuwa akaunti hiyo wakati ikihamishiwa BoT, ilikuwa na Sh bilioni 6.6 tu.

Ilibainisha kuwa malipo mbalimbali kwa waliokuwa wakidai kwa fedha za kigeni kutoka katika akaunti hiyo, yaliendelea kufanyika kati ya mwaka 1985 hadi Juni 30, mwaka jana wakati ambao akaunti hiyo ilisimamishwa.

Taarifa hiyo iliendelea kumbainishia Mkulo kuwa katika kipindi hicho, kulikuwa na tofauti za viwango vya ubadilishanaji fedha za kigeni na za Tanzania.

Ilikumbusha pia kwamba kwa kuwa malipo yalitolewa kwa fedha za kigeni kwa wadai ambao walikuwa ni wa kigeni, tofauti za viwango vya kubadilishana fedha za kati ya mwaka 1985 na mwaka jana, ziliisababishia benki hiyo hasara ya Sh bilioni 135.

HabariLeo ilizungumza na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye alifafanua kuwa deni hilo limetokana na ucheleweshaji wa malipo ya wadai ambao walipaswa kulipwa kwa fedha za kigeni na mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha hizo za kigeni.

Profesa Ndulu alifafanua, kwamba wafanyabiashara wa Tanzania katika miaka ya 1980 walilipa fedha za ndani NBC iliyokuwa ya Serikali na kuruhusiwa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, ambapo NBC ilipaswa kutafuta fedha za kigeni na kulipa waliowauzia Watanzania bidhaa.

Alibainisha kuwa wakati huo fedha hizo za kigeni zilikuwa zikipatikana BoT na katika benki ya NBC pekee ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Serikali. Kwa mujibu wa Profesa Ndulu, kutokana na upatikanaji mdogo wa fedha hizo za kigeni, malipo kwa waliowauzia Watanzania bidhaa, yalicheleweshwa huku kiwango cha kubadilisha fedha kikipanda kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu.

“Kwa mfano, BoT ilipochukua EPA, ilichukua fedha zilizohifadhiwa kwa kiwango cha ubadilishanaji wa Sh 7.14 kwa dola, lakini wakati wa kulipa deni, ililipa kwa kiwango cha Sh 1,000 kwa dola na Serikali ikasema itafidia tofauti,” alisema Ndulu.

Alibainisha kuwa tofauti ya Sh 7.14 waliyoichukua kutoka NBC na kujikuta ikilipa Sh 1,000 kwa waliokuwa wakiidai NBC, ndiyo hasara waliyoipata. Alisisitiza iwapo Serikali ingekataa kulipa deni hilo, Sh bilioni 69 zilizorejeshwa na wafanyabiashara waliodanganya kuwa sehemu ya wadai, wasingeziruhusu zitumike kwenye kilimo na badala yake wangezitumia kufidia sehemu ya hasara hiyo.

No comments: