Thursday, September 17, 2009

Wakili awakaanga Mramba na Mgonja

MKATABA uliosainiwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Daudi Ballali kwa niaba ya BoT na kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Coporation ulikiuka taratibu za manunuzi ya Serikali.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, amedai mahakamani leo kuwa, Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hawakuupitia mkataba huo kabla yakusainiwa.

Manyanda ametoa madai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akisoma maelezo ya awali ya mashitaka ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya sh bilioni 11.7.

Kesi hiyo inawakabili aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gray Mgonja, na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Manyanda alilieleza jopo la makimu wakiongozwa na Hakimu John Utamwa,kuwa, Mkuu wa kitengo cha masuala ya sheria, Godwin Nyelo, alimshauri Yona kutoingia mkataba na kampuni hiyo kwa kuwa ulikuwa unakiuka taratibu za zabuni.

Alidai kuwa, ushauri huo ulipuuzwa, makubaliano ya awali yaliandaliwa na kwamba, vipengele vya 4 na 5 vya mkataba huo vilikuwa vinazungumzia msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Imedaiwa mahakamani kwamba, Mei 26 mwaka 2003 Ofisa udhibiti wa fedha alitoa ushauri kwamba Wizara ipate ushauri kwa TRA ili kuona kama kampuni hiyo ilistahili kusamehewa kodi.

Kwa mujibu wa Manyanda,ofisa huyo alipeleka dokezo hilo kwa Mkurugenzi wa masuala ya ya kisheria Wizara ya Fedha akisisitiza ufanywe uchunguzi mpya kuhusu vipengele vilivyokuwa vikizungumzia msamaha wa kodi.

Mahakama ilielezwa kwamba,wakati ushauri wa TRA ukisubiriwa,yalifanywa marekebisho kwenye mkataba na ulisainiwa Septemba 18,2003.

Manyanda amesema, Balali alisaini mkataba huo kwa niaba ya BoT, Erwin Flores alisaini kwa niaba ya kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Coporation, na kwamba, kipengele cha msamaha wa kodi hakikufutwa.

Manyanda alidai kuwa Mramba alimuandikia Mgonja kuwa utaratibu wa makubaliano kati ya kampuni hiyo na BoT ulikiuka sheria na taratibu za nchi, hivyo akaomba ushauri wa namna ya kuidhinisha msamaha wa kodi.

Imedaiwa kwamba, Wizara ya Nishati na Madini iliandika barua Wizara ya Fedha kupitia kwa Mgonja kwa niaba ya kampuni hiyo ikiiomba msamaha wa kodi.

Mahakama imeelezwa kwamba, Mramba alitoa idhinisho la msamaha wa kodi kwa kusaini katika matangazo ya Serikali baada ya Mgonja kumuomba afanye hivyo.

Wakili amedai kuwa, matangazo hayo yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa TRA ya kuwa kampuni hiyo haikustahili msamaha wa kodi.

Washitakiwa hao wanadaiwa waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Gorvement Bussiness Corporation kutolipa kodi tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA).

Inadaiwa kuwa, uamuzi huo uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00 kati ya mwaka 2002 na Mei2005.

No comments: