OFISI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanza kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ikiwa ni pamoja na kufahamu namna lilivyotumia mkopo wa sh bilioni 280.
Wabunge wametuhumu shirika hilo wakidai kuwa kuna ubadhirifu ukiwamo ukarabati wa nyumba zake kwa gharama kubwa na kupanga kuwauzia wakurugenzi wake kwa bei nafuu.
Ofisi ya CAG imeanza kukagua hesabu za Tanesco ili kufahamu pia kama shirika hilo lilitumia ipasavyo Sh bilioni 280 lilizokopa katika benki za nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Peter Ngumbulu, alisema jana kuwa, tayari taarifa zote za matumizi zimeshapelekwa kwa CAG kwa ukaguzi huo.
“Mimi nilikuwa safarini lakini kwa mujibu wa taarifa nilizopata, CAG ameshapelekewa nyaraka zote alizozitaka na ameshaanza ukaguzi wa mahesabu,” alisema.
Alipoulizwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika lini alisema “siwezi kufahamu lakini wakishamaliza, taarifa zitatolewa na ni vizuri ukawauliza Tanesco wakueleze kiundani juu ya nyaraka zilizoombwa na CAG”.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovic Utouh, amekiri kwamba ofisi yake imeanza ukaguzi huo.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilitupa kazi hiyo tuifanye na wakatupa hadidu za rejea ambazo tutazifuata, lakini hadidu hizo muulize Mwenyekiti wa Bodi mwenyewe atakueleza.
Kwa mujibu wa Utouh, kazi hiyo ya ukaguzi waliianza wiki mbili zilizopita lakini hakusema itakamilika lini.
Wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge uliojadili Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Nishati na Madini, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alieleza kuwa Tanesco ilitumia Sh bilioni 1.4 kukarabati nyumba zake saba, huku moja ikitumia Sh milioni 600 na ikitarajiwa kuuzwa kwa asilimia 10 ya gharama - Sh milioni 60.
Alizitaja nyumba hizo kuwa ziko Oysterbay na Masaki na thamani ya ukarabati kwenye mabano kuwa ni ya barabara ya Chole (Sh milioni 600); Guinea 24 (Sh milioni 258.4); Laibon 65 (Sh milioni 190); Mawenzi 454 (Sh milioni 138); Guinea 93 (Sh milioni 88.5); Toure Drive 315 (Sh milioni 79) na Uganda Avenue 98 (Sh milioni 73.6).
Mwenyekiti wa Bodi alikiri kutofahamu jinsi Sh bilioni 1.4 zilivyotumika kukarabati na mpango wa kuwauzia nyumba hizo wafanyakazi wake wa ngazi za juu.
Kuhusu mkopo wa Sh bilioni 280 ambao ilikopa kutoka benki za nchini ambazo wabunge walidai zimetumika vibaya, Ngumbulu amesema: “Fedha hizo naamini zimetumika vizuri kama ilivyopangwa kwani hata benki zenyewe ni wakali na wanafuatilia.
“Fedha hizo zimetumika kuliweka sawa shirika kama kulipia madeni yake na ukarabati mbalimbali lakini taarifa za matumizi yake naomba waombe Tanesco”.
Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa kuhusu matumizi ya fedha hizo na taarifa walizompa CAG, alisema: “Tusubiri uchunguzi ukamilike, kwa sasa siwezi kuzungumza lolote, Wizara ya Nishati na Madini itatoa taarifa ya uchunguzi kama ilivyoahidi”.
No comments:
Post a Comment