WANAWAKE wa Kimasai wanaoishi katika wilaya ya Ngorongoro eneo la Loliondo wametoa tamko rasmi la kuiomba Serikali iwape misaada ya dharura ya chakula, mahema na maji pamoja na kupewa maeneo ya kulisha mifugo yao kutokana na opoeresheni kuwahamisha.
Kiongozi wa wanawake hao aliyesoma Tamko hilo Pirias Maingo aliwaambia wanaoshiriki tamasha la 9 la Jinsia Dar es Salaam, lililoandaliwa na Mtandao wa mashirika wateteza wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia (FemAct) Pirias Maingo alisema jana kuwa wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu tangu waanze kuhamishwa kwa nguvu katika eneo hilo.
Pirias alisema wanasikitishwa kwa serikali kutowaonyesha maeneo ya kuishi baada yakuchomewa nyumba zao kupisha shughuli za uwindaji. Alifafanua kuwa wamelazimika kuhamia maeneo ambayo yana ukame , hayana maji hata malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Tamko hilo lilitolewa baada ya Mwanamke wa Kimasai Kooya Oletiman, kuzungumza kimasai na kutafsiriwa na Paulina oletipap kuwa wanawake na watoto ndiyo wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na majukumu waliyonayo ya kutunza familia ambapo tangu oparesheni ya kuwahamisha ilipoanza wamekuwa wakihama hama na kukosa mahali pa kujisitiri.
Wanawake hao wapatao 978 kutoka katika vijiji vya Arash,Maaloni, Ololosokwan, Olipiri, Soitsambu, Olorien Piyaya na Malambo wamesema kuwa wametaka pia kampuni ya uwindaji ya OBC iondolewa ktika eneo hili badala yake ardhi ya vijiji ihakikishiwe usalama wake kwa mujibu wa sheria.
Tamasha la Jinsia 2009 linaendelea leo kwa mada mbalimbali ambazo msisitizo wake mkubwa ni rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni
No comments:
Post a Comment