-Wa Sweden aenda hadi ofisi za CCM
-Msekwa aziandikia waraka kuzipoza
-Akiri NEC ilikosea taratibu
BAADHI ya balozi nchini zimefuatilia taarifa za kikao kilichopita cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotafsiriwa kuwa kililenga kuziba midomo ya wabunge, ili kujiridhisha na usalama wa fedha zao zinazokuja Tanzania kwa njia ya msaada wa kibajeti, Raia Mwema imeambiwa.
Hatua hiyo ya ufuatiliaji, taarifa zinasema, imechagizwa na hoja kwamba kama ni kweli kwamba chama tawala kiliwaonya wabunge wake wapunguze kelele dhidi ya Serikali na hivyo kuua uhuru wa Bunge na mbunge mmoja mmoja wa kuikosoa, basi kazi muhimu ya Bunge na wabunge ya kuisimamia Serikali, itakuwa hatarini.
Taarifa kutoka kwa maofisa wasaidizi wa baadhi ya balozi hizo, zinaeleza ya kuwa baadhi ya mabalozi wamepelekewa waraka maalumu ulioandikwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, kwa lengo la kueleza kwa ufasaha kile kilichojiri katika kikao cha NEC cha mwezi uliopita mjini Dodoma.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mmoja wa balozi zilizopelekewa waraka huo wa Msekwa ni wa Sweden, ambao Balozi wake alifika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo hayo na masuala mengine ya kisiasa, hatua ambayo imethibitishwa na ubalozi wa Sweden nchini, ingawa pia ubalozi huo umesisitiza kuwa hayo yalikuwa mazungumzo ya kawaida kuhusu masuala ya kisiasa nchini.
‘‘Ni kweli (Balozi Staffan HerrstrĖm) alikwenda CCM Lumumba. Na walifanya mazungumzo kuhusu masuala ya kisiasa. Huu ni utaratibu wa kawaida,’’ alisema katibu muhtasi Doris Lema, akikariri majibu ya Balozi kwa maswali ya Raia Mwema juu ya safari yake ya ofisi za CCM.
Katika hatua nyingine, Raia Mwema imefanikiwa kupata nakala ya waraka wa Msekwa kwa balozi kadhaa zinazoifadhili Tanzania ambao, pamoja na mambo mengine, unazungumzia yaliyojitokeza katika kikao hicho cha NEC, akionyesha upungufu katika taratibu za kumjadili Spika Samuel Sitta na kasoro miongoni mwa wabunge wa CCM wanaojitambulisha kuwa ni wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi.
Katika maelezo yake, Msekwa anatoa ufafanuzi katika maeneo makuu matatu aliyoyaweka kwenye mtindo wa maswali, jambo la kwanza likiwa ni “Mjadala kwenye NEC umehoji uendeshaji wa Bunge, hatua ambayo ni uvunjaji wa kifungu cha 100 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?”
Jambo la pili: “Ni sahihi kwa NEC-CCM kujadili mwenendo wa wabunge wake ndani ya Bunge, akiwamo Spika? Kwa maneno mengine, kitendo hicho kinavunja sheria ya mamlaka na haki za Bunge? Pili: “Spika amekabwa kwenye kikao hicho kwa sababu ya kuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya mafisadi? Kabla ya kutoa ufafanuzi wa kina katika maeneo hayo, Msekwa anaeleza; “ jibu kwa kila swali ni hapana.”
Anasema katika waraka huo ya kuwa NEC ina wajibu wa kujadili mwenendo wa viongozi wake ingawa katika kikao cha Dodoma utaratibu wa chama hicho kumlalamikia kiongozi au mwanachama mwingine yeyote haukuzingatiwa.
“Kifungu cha 108 cha Katiba ya CCM kinaeleza majukumu ya jumla ya mikutano ya NEC, na kifungu kidogo chake cha nane kinaeleza kudumisha uangalizi juu ya vitendo vya wanachama na viongozi wa CCM, hii maana yeke ni kudhibiti mwenendo na vitendo vya wanachama na viongozi wake.
“Kuingilia mambo ya Bunge ni makosa, lakini umma unajua kuwa kumekuwa na makundi hasimu miongoni mwa wabunge kuhusu vita dhidi ya ufisadi, wapo wanaopinga ufisadi na wengine wanaopuuza vita hiyo. Spika alikosolewa kwa kushindwa kuendesha mijadala bila kuzingatia maslahi ya chama, na wabunge wamekosolewa kwa kushindwa kutumia kamati ya wabunge wa CCM,” anasema Msekwa.
Hata hivyo, pamoja na kuonyesha kuamini kuwa kulikuwa na nafasi kwa Spika kuendesha mijadala kwa kutazama maslahi ya chama na pia NEC kuwa na wajibu kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho kufuatilia na kuhoji mienendo na vitendo vya wanachama na viongozi wake, Msekwa anasema makosa yalifanyika ndani ya NEC.
“Kitendo hicho cha NEC kinaweza kuwa ni makosa. Ingawa kujadili mwenendo wa Spika na baadhi ya wabunge wengine wa CCM kinaweza kutetewa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, lakini pia kuna makosa yamefanyika na hasa kwa upande wa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.
“CCM imekuwa na utaratibu na kanuni nzuri kwa viongozi wake wanaolalamikiwa mwenendo wao kwamba wamekiuka kanuni na maadili ya chama. Sheria na kanuni hizo zinaeleza kuwa kiongozi anayetuhumiwa anapaswa kupelekewa orodha ya tuhuma zake na kupewa fursa ya kuzijibu.
“Na baada ya hapo, Kamati ya Maadili ya CCM inakutana kwa ajili ya kuchambua suala hilo na kufanya uamuzi na pia kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu (NEC). Kwa hiyo inaridhiwa kuwa taratibu za kisheria hazikufuatwa katika suala hili,” anaeleza Msekwa katika waraka wake huo wenye kurasa 11.
Anaongeza:“Ni vizuri ikaeleweka kwamba katika utamaduni wa siasa za vyama vingi umuhimu ni lazima uwekwe na kudhibitiwa ndani ya chama cha siasa, hususan suala la nidhamu. Na uhai wa chama chochote cha siasa ni umoja na nidhamu.’’
Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Alain Noudehou, amewasifu Rais Jakaya Kikwete na Spika Sitta kwa kazi nzuri ya Rais Kikwete kuruhusu uhuru wa kuzungumza ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa Watanzania kumuuliza maswali ya papo kwa papo.
Akizungumza, jana, Jumanne, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Mwakilishi huyo wa UN alimsifia Sitta kwa mpango wake wa kuendesha Bunge vyema katika wajibu wake wa usimamizi wa Serikali.
Source:www.raiamwema.co.tz
1 comment:
CCM wamezoea kupeleka nchi kibabe, this time tutawapiga chini kwenye kur hatutawapa
Benard
Post a Comment