Tuesday, May 13, 2014

TGNP wahimiza wahariri kufanya uchambuzi wa bajeti kabla ya kuripoti




WANAHARAKATI wa masuala ya Kijinsia, haki za binadamu, demokrasia na utawala bora nchini (TNGP) wameshauri wahariri wa vyombo vya habari nchini kusaidia umma kwa kuchambua bajeti na kuonesha maeneo ambayo yana mushkeri kwa lengo la kuboresha maisha binafsi na jamii.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana ambao uliambatana na utoaji wa taarifa nini kinatokea katika tafiti mbili za vipaumbele vya taifa kwa sampuli za mkoa wa morogoro, Mbeya, Shinyanga  na Dar es salaam,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa TGNP, Lilian Liundi alisema kuwa   mpaka sasa vyombo vya habari havina uchambuzi wa kutosha kueleza wananchi kuhusu mustakabali wao katika muktadha wa bajeti kwa mwaka jana na hii ijayo ya mwaka wa fedha 2014/2015.
Katika mkutano huo ambapo wahariri walipata nafasi ya kuzungumza walikiri kuwapo kwa tatizo la kutozungumzia masuala ya uhusika na kufanya mambo kishabiki zaidi.
“Ni kweli kuna tatizo kubwa kwenye uchambuzi wa bajeti, mara kadhaa tunaripoti kile ambacho wanahabari wameandika au wamesikia mbunge akisema lakini hatuendi zaidi kufanya uchambuzi wa kina” alisema Theodatus Muchunguzi, Mhariri Mtendaji wa habari wa Nipashe.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Usu Mallya, ambaye sasa ni mwanachama wa TGNP akizungmza na wahariri juu ya kufanya uchambuzi wa bajeti kila mara na kutokuripoti tu bila kufanya uchambuzi

Katika mkutano huo aliyekuwa  Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Usu Malya,  alizungumzia haja ya wahariri kutambua  misingi ya bajeti na umuhimu wake katika masuala ya kijinsia kwa maana utekelezaji wake ni ama unawanasua watu katika umaskini na ubaya wa maisha au unawasukumia huko.
Alisema kwamba tafiti zilizofanywa katika mkoa wa Morogoro na Dar es salaam unaonesha ni namna gani bado taifa hili linahitaji bajeti yenye uhalisia ambayo itazingatia mahitaji ya kimakundi na hatimaye kitaifa.
Katika mkutano huo tatizo la hospitali ya Palestina ya jijini Dar es salaam la kukosa mtambo wa kuchomea taka, kumefanya wanawake wanaokwenda kujifungua kutakiwa kwenda na ndoo za kuwekea mabaki yanayotokana na shughuli yao ya uzazi ikiwemo kondo.
"Huwezi kuamini lakini ndio hali hiyo.." alisema Mtendaji huo wakati wa kuelezea mahitaji ya kimakundi yana maana gani katika kutekeleza bajeti inayozingatia jinsia.
Aidha tatizo la bajeti kukumbatia wawekezaji wakubwa badala ya mtu mmoja mmoja wanaotengeneza asilimia 80 ya uchumi unaotegemea kilimo kunawaweka wananchi katika uchumi mdogo japokuwa alama za upandaji wa uchumi zimefikia asilimia 7.
Na mfano ulikuwa namna wakulima wadogo Morogoro wasivyofikiriwa katika mpango wa ghala la chakula na mahitaji mengi katika bajeti ya mwaka huu kuzingatia wawekezaji toka nje wanacokuwa maeneo makubwa.
Aidha mfano mwingine ulikuwa juhudi za marafiki wa UDA kusaidia kampuni hiyo kupata msamaha wa magari yake wanayoingiza wakati wenye daladala wengine ambao wanakusudia kuhudumia Dar es salaam hiyo hiyo wakitoswa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TGNP Mtandao Lilian Liundi akizungumza na wahariri kuhusu namna ya kushiriki katika kuhabarisha jamii juu ya mchakato wa bajeti na kushiriki kuichambua kwa mrengo wa kijinsia
"huyu mwekezaji mkubwa kwanini apewe msamaha wakati huyu mdogo ndiye hasa alitakiwa kupewa nafasi ya kunyanyuka?" liliulizwa swali hilo  na wahariri pamoja  na mamengine kadhaa yakiwemo UDA kubadili njia wanavyotaka na kutoza nauli kubwa kuliko iliyopangwa na Sumatra.
"Ukiwa Mwenge jioni utaona UDA nayo inaingia katika mkumbo wa magari ya kitalii ya kutoza nauli ya sh 1000 kuelekea Mbezi" alisema mmoja wa wahariri.
Walisema UDA na kampuni ya biashara  haistahili msamaha na pia lazima wafanye kazi kwa kutumia masharti ya Sumatra. Katika uchambuzi wa bajeti tatizo la uchukuzi linaonekana kuwa dogo lakini linavuruga bajeti za watu wa hali ya chini na kujikuta wakikosa fedha za maendeleo wakibaki na fedha za matumizi pekee.
Katika mkutano huo wahariri walichambua mwenendo mdogo wa makundi ye pembezoni na kuzungumzia haja ya kujikita katika uchambuzi wa mambo badala ya kutumikia wanasiasa ambao wanaonekana kutosimamia vyema utendaji wa serikali katika kutekeleza vipaumbele vyake.
Uchambuzi wa bajeti unaweza kusaidia sana katika ushawishi wa mabadiliko hasa katika maeneo ambayo yanatengeneza fursa za mtu mmoja mmoja hasa za wale ambao hawana uwezo wa kujikwamua katika uchumi ila kwa kutengenezewa fursa na kusaidiwa.
Uchambuzi wa bajeti katika masuala ya makusanyo na matumizi wka mantiki ya kodi na vyanzo vingine vya mapato kwa serikali kunaweza kusaidia kuona kama kuna makusanyo yaliyo sahihi na matumizi sahihi ya raslimali zilizopo. Hali inawezekana kwa kuangalia sera  zinazoambatana na utayarishaji wa bajeti. "Uchambuzi wa bajeti unaweza kabisa kusaidia kuona mianya yenye udhaifu kwa kuangalia sera zilizopo na hivyo kusaidia kupata kile kilichokusudiwa katika sera, ustawi wa jamii" alisema Usu.
Katika uchambuzi Malya aliwataka wahariri kuzingatia mzunguko mzima wa bajeti na si tu inapokuwa imesomewa.
Alisema uchambuzi wa bajeti ni moja ya moja ya silaha ya kutambua mipango ya serikali itawezesha nini katika matumizi ya raslimali za taifa kwa manufaa ya watu.
Pia uchambuzi utaonesha namna bajeti ilivyoangalia mahitaji halisi kwa makundi mbalimbali kama wanawake, watoto, wale wenye mahitaji maalumu na maskini na namna kero zao zinavyoathiri mwenendo wa kiuchumi.
Wahariri walikubaliana kwamba uchambuzi wa bajeti unatakiw akufanyika kwa lengoi la kuibua hoja muhimu za kuweza kuwabana watengeneza sera kuhusu matatizo ya makusanyo na matumizi ya bajeti kw amanufaa ya watu na hasa makundi ambayo yapo pembezoni.
Aidha kwa kufanya uchambuzi wenye uhakika mashirika au taasisi za kiraia zinaweza kuwa na nafasi ya kutumia chambuzi hizo kusaidia  kuwakumbusha watengeneza bajerti na sera nini wanatakiwa kufanya ili kuwa na mnyororo unaotakiwa katika kuwezesha maisha bora wkla kila mwananchi.
Aidha katika michango yao wahariri walizungumzia ukusanyaji hafifu wa mapato na matumizi yake na kutoshirikishwa kwa wananchi katika bajeti ndogo za kata,tarafa, wilaya hadi mkoa na taifa hali inayowafanya watanzania wengi kubaki na dhana dhaifu kuhusu bajeti maana na sababu zake.
TGNP iliyoanzishwa 1993 imejikita zaidi katika kushawishi na kuwezesha makundi mbalimbali kutambua umuhimu wa usawa katika jinsia na kuboresha maisha kwa akuangalia muundo wa kisera na utekelezaji wake ikiwa na mikataba ya kimataifa ya usawa wa jinsia  katika mamlaka ya uamuzi na utekelezaji.
Aidha inashughulikia pia kuangalia mfumo wa sera za kiuchumi na mchakato wake kwa lengo la kuona kama sera hizo zinalipeleka taifa katika kuzingatria mahitaji ya makundi katika kuboresha maisha ya taifa. Mwaka 1997, TGNP wakishirikiana na FemAct walianzisha ushawishi wa bajeti inayozingatia jinsia ( Gender Budget Initiative-GBI-)  lengo likiwa kuwa na nafasi pana ya ushiriki uliosawa katika fursa za kiuchumi na mamlaka kwa makundi yote.
mwisho

No comments: