Wednesday, May 14, 2014

TAMKO LA WANAHARAKATI WA NGAZI YA JAMII NA WASHIRIKI WA GDSS DHIDI YA MWENENDO WA BUNGE LA KATIBA LILILOPITA



.
Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao tunatoa tamko hili baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa bunge la Katiba lililomaliza hivi karibuni. Tumeshtushwa sana na namna bunge hili lilivyoendeshwa na kugubikwa na kasoro mbali mbali ambazo zisipochukuliwa hatua madhubuti kuna uwezekano wa kutopata Katiba au kupata  Katiba ambayo haitokani na  mapendekezo au maoni ya wananchi walio wengi.
Bunge hili liligubikwa   na Kauli za kuudhi, matusi, kauli za kibaguzi, dharau za Kijinsia, vitisho na siasa chafu na ushabiki wa kisiasa unatokana na utashi wa vyama. Hali hii ilipelekea masuala ya msingi yanayogusa ustawi wa taifa kutojadiliwa na kupelekea baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba kususia bunge hilo.
Wakati Bunge hili limetumia billion 27 kwa siku 67 walizokaa kujadili kanuni za bunge maalum la katiba na  sura mbili za rasimu ya katiba, ni dhahiri limewanyima watanzania fursa ya masuala ya msingi yanayowahusu kutojadiliwa.  Hali hii imewaweka watanzania  wengi njia panda kwani hadi sasa hawajafanya  kazi waliotumwa. Wakati huo huo kazi waliofanya iko  chini ya matarajio  ya wananchilakini wametumia pesa ambazo zingeweza kuelekezwa katika huduma za msingi za wananchi kama vile maji, afya, elimu na miundombinu mibovu.
katibu wa kamati ya wanaharakati ngazi ya jamii wanaoshiriki GDSS Badi Darus akisoma tamko la wanaharakati mbele ya wanahabari leo

Pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya  Mrisho  Kikwete kuonesha nia  njema  ya  kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya hapa Tanzania, nia hiyo haionekani kuwa  ndani ya wanasiasa  kwa  ujumla  wake. Kwa vitendo  na  maneno  ya watendaji waandamizi  wa  serikali  ya  Tanzania, Wanaharakati wa ngazi ya jamii na wana GDSS tunachelea  kuamini  kuwa  ipo nia  ya dhati  na ya kweli  ya kuhakikisha  kuwa  nchi  yetu  inapata Katiba  Mpya  inayotokana  na  maoni  ya  Watanzania wenyewe.  Kwa  mwelekeo  wa  mijadala  ya  hivi  karibuni ndani  na  nje  ya  Bunge  Maalum  la  Katiba pamoja  na serikalini,  nia  ya  watawala  inaonekana  kuwa  ni kutaka kufanya  mabadiliko  madogo madogo  katika  Katiba  ya  sasa na kuacha  kila  kitu  kama  kilivyo. Kwa  mtazamo  wetu,hiyo inapingana  na  nia  na  kiu  ya  watanzania  walio wengi kuona  kuwa Mchakato  wa  Kuandika  Katiba  Mpya  unaleta  mapinduzi  ya Kikatiba yatakayokuwa chachu ya nchi yetu kuongozwa kwa misingi  ya  uwazi,  uhuru,  demokrasia  na  kuheshimu  utu  wa mtu na haki za binadamu.
wanahabari waliofurika katika ukumbi wa TGNP Mtandao wakiwasikiliza wanaharakati

wanaharakati wakifuatilia tamko likitolewa


wanaharakati wakiendelea kujibu maswali ya wanahabari
Mapungufu  katika  sheria  inayoongoza  Mchakato  huu  ni makubwa  kiasi  kwamba  utata  wa  mchakato  mzima  ni  wa Kisheria. Kwa mfano, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilivyo sasa inashindwa kutoa mwelekeo thabiti wa nini kifanyike inapofikia  hali  ya  sintofahamu  na  mkanganyiko  wa mchakato  kama  ilivyo  sasa.  Mianya  hiyo  ya  Kisheria imepelekea  utata  katika  utungaji  Kanuni  za  Bunge  Maalum la  Katiba  hadi  kuleta  mkanganyiko  na  kufanya  Bunge kutofikia  muafaka  katika  maeneo  kadhaa  ikiwemo  aina  ya Kamati ya Utendaji, kura katika kupitisha vifungu vya rasimu, idadi inayohitajika katika  kupitisha  jambo  ndani ya  Bunge  Maalum  pamoja  na mambo  mengine  kadhaa. Hata  malalamiko  yaliyopo  hivi sasa  juu  ya  baadhi  ya  makundi  kutokuwa  na  uwakilishi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni suala lenye mizizi yake kaika  Sheria  ya  Mabadiliko  ya  Katiba.  Suala  hii  limeleta hisia kuwa liliwekwa hivyo  makusudi kisheria ili CCM iwe na wajumbe wengi kuliko makundi mengine ndani ya Bunge Maalum  la  Katiba  na  hivyo kupitisha  vifungu  vya  Katiba kwa urahisi bila kuhitaji maridhiano na pande zenye mawazo tofauti.
Sheria ya  Mabadiliko  ya  Katiba  sura  ya  83  ya  imempa  Rais  madaraka  makubwa  sana  katika  hatua zote  sita  za  mchakato wa  Katiba  Mpya,Rais  ana  sauti  na mamlaka  makubwa  sana  ya  kufanya  maamuzi  kuanzia kutangaza  kuanza/kusitishwa kwa  mchakato,  kutungwa  na kurekebishwa  kwa  sheria,  uteuzi,  uendeshaji    na  uvunjaji  wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum  laKatiba,  uzinduzi,  uendeshaji  na  uvunjaji  wa  Bunge la  Katiba na  usimamizi  wa  mchakato  mzima  wa Katiba. Hali hii imepelekea Rais ambae pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi  kuingilia mchakato huu kwa kofia ya chama.  Kwa mfano maamuzi yaliofikiwa na Kamati kuu ya chama cha mapinduzi hivi karibuni hayaonyeshi kama CCM ina nia njema na mchakato huu wa katiba .
Ushiriki wa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano katika bunge maalum la katiba kumewanyima nafasi wananchi kukutana na wawakilishi wao ili kuwasilisha masuala yao katika bunge la bajeti linaloendelea, hali hii imepelekea watanzania kutowakilishwa vyema kwenye bunge hili la bajeti na kukosa sauti za wananchi.
Kutokana na tuliyoyaeleza hapo juu tunadai yafuatayo:
i.                    Mchakato wa maridhiano kati ya pande mbili zinazosigana (UKAWA na Tanzania Kwanza) ufanyike haraka ili kuweza kunusuru mchakato na bunge la katiba.
ii.                  Kutokana na bunge maalum kutumia fedha nyingi kinyume na ilivyotarajiwa na kazi walioifanya ipo chini ya matarajio ya watanzania, tunadai awamu ya pili ya bunge hili matumizi yapungue ili fedha zielekezwe katika kugharamia masuala ya maendeleo.
iii.                Kwakua wananchi walitoa maoni yao na ndio msingi wa chimbuko la madaraka na mamlaka yote ya nchi tunadai maoni ya wananchi yaliopo katika rasimu ya katiba, yaheshimiwe.
iv.                Dharau, ubabe, vijembe, vitisho, matusi, kashfa na ubaguzi wa kijinsia unaokuzwa na kulelewa na kanuni za bunge maalum la katiba,  tunadai ziundiwe kanuni mpya kwa ajili ya kuondoa na kukemea vitendo hivyo.
v.                  Tunalaani malumbano yasio na tija yenye lengo la kupoteza muda ili wajumbe wa bunge maalum la Katiba waongezewe siku na posho.
vi.                Bunge la katiba limejipa madaraka makubwa yakubadili rasimu ambayo imebeba maoni ya wananchi. Tunadai maoni yaliopo katika rasimu ya katiba ilioandaliwa na tume ya Warioba yaheshimiwe.
vii.              Kama hayo yote hayakuheshimiwa na kuzingatiwa, tunadai bunge hili la Katiba livunjwe na kuundwa kwa bunge jipya la Katiba litakalobeba uwakilishi wa wananchi wenyewe hasa makundi ya walio pembezoni.


Imetolewa na kusainiwa kwa niaba ya washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) na wanaharakati wa ngazi ya jamii

Amina Mcheka                                  Badi  Darusi
...........................                                 .........................
Mwenyekiti                                       Katibu
Tarehe 14, Mei 2014 inatatikana pia  
www.gdss.blogspot.com

No comments: