Leo
vikao vya Bunge la bajeti ya mwaka 2014/2015 vimeanza rasmi mjini Dodoma ambapo
tayari serikali kwa kupitia Waziri wa Fedha na Uchumi Mhe. Saada Nkuya, imeshatoa mwelekeo wa bajeti unaofikia zaidi ya trilioni 19 ikilinganishwa
na trilioni 18.2 za mwaka wa fedha unaoishia Juni 2014. Kwa mujibu wa serikali
vipaumbele vya mwaka huu ni mwendelezo wa kutekeleza mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza 2011 na Mpango wa
Matokeo makubwa sasa (BRN) kwenye sekta za nishati, kilimo, maji, elimu,
uchukuzi na kuboresha mazingira ya biashara. Aidha sehemu kubwa ya bajeti
imeelekezwa kugharamikia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu wa
mwakani pamoja na kukamilisha mchakato wa kuandaa katiba mpya ya Tanzania.
TGNP
Mtandao tunafuatilia kwa ukaribu mijadala ya Bunge inayoendelea, tunasisitiza
matumizi bora ya muda na kuheshimu fedha za walipa kodi ambazo zitatumika
kuwalipa wabunge na watendaji wa serikali posho wanapokuwa Dodoma, muda wa siku
52 uliotengwa utumike kutengeneza mijadala yenye tija itakayozaa bajeti ya
wananchi inayozingatia usawa wa kijinsia na kuwanufaisha wananchi wote hasa
wanawake na wanaume walioko pembezoni.
Tunalitaka
Bunge kutumia kipindi cha mijadala kuibana serikali na kutokupitisha bajeti
isiyo halisia. Serikali inatakiwa kueleza kwa ufasaha ni wapi itapata fedha
Shilingi trilioni 19.6, pia wanatakiwa kukataa kupitisha bajeti yenye fedha
nyingi za matumizi ya kawaida au posho na chai badala ya kuelekezwa kwenye
miradi ya wananchi.
Hata
hivyo hofu yetu ni uwezekano wa kujitokeza matukio ya aibu ya vurugu, kejeli,
matusi, majigambo na zomea zomea kama
ilivyotokea kwenye Bunge maalum la katiba na kupoteza muda kujadili masuala ambayo
hayana tija na ni nje ya vipaumbele vya serikali kwa ajili ya wananchi. Tunatoa
raia kwa wabunge kutokutumia nafasi hii adimu vibaya kulumbana kisiasa. Tutambue
kuwa Bungeni ni mahali pa kujadili na kujenga hoja za wananchi na kuzitafutia
ufumbuzi hasa changamoto zinazowakabili vijijini na mijini. Kwa mantiki hiyo,
tunawataka wabunge wote watakaokuwa Dodoma kutenda haki kwa wananchi kwa:
- Kutumia muda wanaopewa kujadili masuala ya wananchi, kutetea utekelezaji wa miradi muhimu ya wananchi iliyoanishwa kwenye bajeti hasa afya ya uzazi salama kwa wanawake, mazingira bora ya elimu, upatikanaji wa maji ya kutosha safi na salama na mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogowadogo wanawake na Vijana mijini na vijijini.
- Kuacha mijadala inayotoka nje ya mada husika na kuingiza masuala binafsi au siasa.
- Kuacha lugha chafu za kuudhi, matusi, kejeli, udhalilishaji wa kijinsia, majigambo, vurugu na kuheshimu hoja na mchango wa kila mmoja.
- Wabunge kuhakikisha siku 52 watakazokuwa Dodoma zinatumika kikamilifu kubeba masuala ya wananchi hasa changamoto kubwa zinazowasumbua na kutafuta ufumbuzi.
Mwisho
tunaomba uongozi wa Bunge (Spika, naibu Spika) na sekretarieti kusimamia
kikamilifu mijadala hii na kutenda haki kwa wabunge wote bila upendeleo na
kuhakikisha kuwa kiti cha spika hakigeuzwi kuwa chanzo cha vurugu Bungeni.
Imetolewa
na
Signed
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji -
TGNP Mtandao
No comments:
Post a Comment