Kwa muda mrefu mjadala unaohusu
mchakato wa kaundikwa upya kwa katiba mpya umekuwa ukisikika zaidi kupitia kwa
watu au makundi yenye majina makubwa kama wanasiasa na wasomi na wale wenye
nafasiki ya kuvifikia vyombo vya habari, lakini jamii ya
chini au makundi ya pembezoni yametawaliwa na ukimya wa ajabu kana
kwamba hawana la kusema.
Ukifuatilia vijijini na katika maneo
mengine ya kukusanyika wananchi utaona jinsi wanavyoshiriki kutoa sauti zao kwa
namna wanavyofuatilia mchakato unaoendelea. Vijiweni, masokoni, vilabuni nako
kuna mijadala ya katiba mpya nao wanapokusanyika wanajadili kuwa ni masuala
gani wanayataka au wangependa kuona yameingizwa kwenye katiba mpya. Lakini je
matokeo ya mjadala ngazi ya jamii ni nini? Je sauti zao zinasikika kwa mamlaka
za juu?
Suala la nani anafanya nini au
anasema nini na kwa manufaa ya nani kwenye Bunge la katiba au mijadala
mikubwa kwenye makongamano na matamasha ambayo wanajamii wa ngazi ya kijiji au
kitongoji hawaalikwi yanasikika huko ngazi ya chini kabisa. Wananchi hao hao
wanafuatilia kupitia redio na magazeti, na tujue kuwa siku hizi watu wengi
wanamiliki simu za tochi ambazo zina redio. Wanachokisikia wanajadiliana jinsi
wanavyoweza kuhakikisha sauti zao zinasikika au ziwafikie viongozi.
Kutokana na kukosekana kwa jukwaa la
kisheria au mijada inayotakiwa kuongozwa kisheria na serikali zetu hasa kwenye
ngazi za vijiji na kata, wanajamii sasa wameanzisha kitu kinachoitwa sauti ya
jamii (jamii Voice) hii ipo katika kata za Kisarawe (Pwani) Mkambarani
(Morogoro Vijijini), Songwa (Kishapu), Songea mjini, na kata ya Mwananyamala
(Kinondoni), wananchi wameanzisha mitandao ya vikundi vidogo vidogo, na kuunda
mtandao mkubwa unaokusanya sauti za wengi na kuzisambaza.
Mitandao hii kwa ngazi walio nayo ya
kata wanashirikiana na wanajamii kupaaza sauti zao kwa nguvu kuwasiliana
na Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba moja kwa moja bila kuandika barua au
kuwafuata huko Dodoma, wanawaeleza wanataka kitu gani kifanyike na waseme nini
kwenye mchakato wa Katiba mpya.
Wakati wa uendeshaji wa mabaraza ya
katiba uliofanyika katikati ya mwaka 2013 wanajamii hawa walitumia mfumo huu wa
kupeana taarifa kupashana habari juu ya ushiriki wao kwenye mabaraza ya katiba
na kinachoendelea, baadaye walijiunga na kuandaa mabaraza ya katiba ya asasi
ambayo nayo walitumia sms kupashana habari na kupata maoni ya wengi.
Nilibahatika kukutana na baadhi ya wananchi
wanaoshiriki kwenye mpango huu wa kupaaza sauti za jamii, mmoja wao ni Janeth
Mawinza kutoka Mwananyamala ambaye anasema kuwa wao wanamtambo mdogo wa kurusha
ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwenda kwa watu zaidi ya 1000 kwa mara moja.
Wanafuatilia mjadala wa Bunge la Katiba na kuandika ujumbe mfupi ambao
wanaurusha kwenda kwenye simu za wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kwa wakati
mmoja wakidai wanataka mjadala wa namna gani na wanataka nini kwenye mchakato.
“Mpango huu unasaidia sasa kuweka
msukumo na kuonesha kuwa sisi wananchi wa ngazi ya mtaa huku chini tunafuatilia
kile wawakilishi wetu wanachokijadili kwenye Bunge la katiba, tunasema na
tunawaeleza mmoja mmoja anasoma ile meseji kwenye simu yake kama anampango wa
kupoteza muda au kufifisha masuala ya wananchi masikini kwenye Katiba
anaacha..”anasema Janeth.
Mara nyingi wananchi wamekuwa
wakilalamika kuwa mchakato umewatenga haswa kutokana na wajumbe wa Bunge
kugawanyika kimakundi na kiitikadi ndani ya Bunge hilo na kuwaacha wananchi
bila kiongozi wao.
Janath anasema kuwa wametambua
kuwa wanawake wengi wanamiliki siku lakini hawana uwezo wa kutazama TV au
kusikiliza redio, wanatumia njia hiyo kuwafikia wanawake wakiwa jikoni wakipika
na badaye wanachukua hatua. “mfano ukituma ujumbe kuwa kesho tuna mkutano wa
kuhamasisha kuhusu jambo fulani, wataikia wengi kuliko tungetangaza kwenye
chombo cha habari..”anasema.
Huko Kisarawe wananchi wa
kituo cha taarifa na maarifa kutoka vijiji vya Kisarawe mjini na
Visegese, wanatumia njia hii ya ujumbe mfupi kuhamasishana juu ya kampeni
yao ya utunzaji misitu na mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia kwa jamii na
upatikanaji wa huduma za msingi kama maji, afya, elimu na miundombinu kwa jamii
hasa wanawake.
Wanatumia mfamo huu wa upashanaji
habari kusambaza meseji kwa wanavijiji zaidi ya 5000 kwa mara moja, pamoja na
viongozi wa kijamii na wanaona mwitikio wa jamii kutokana na ujumbe unaotumwa.
Wakiwa mjini wanafikia wananchi walio katika vijiji ambavyo magari hayafiki.
“hapa Kisarawe mfumo huu umetusaidia
kwa kiasi kikubwa kupashana habari, kwanza tunawatumia viongozi wetu ujumbe kwa
njia ya sms, tukiwakumbusha kutimiza ahadi zao huko vijijini, baadaye
tunafuatilia utekelezaji. Tumekuwa na kampeni yetu ya kupinga ukatili wa
kijinsia kwenye vijiji nyetu ambavyo vingine havififikiki kiurahisi, tunatuma
ujumbe” anasema Simon Mpunga mratibu wa IGN
Kisarawe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa na Maarifa.
Aidha wametumia njia hiyo
kuhamasisha viongozi wa vijiji kuwachukulia hatua watu wanaowazuia watoto wa
kike kupata elimu kwa kuwapa mimba. Katika mfumo huu ambao pia wameshiriki
kuwahamasisha wananchi kufuatilia mjadala wa Bunge la katiba wakati
linaanza mjini Dodoma, wakati rasimu ya Pili ya Katiba ilipotoka walihamasisha
wananchi wote wa Kisarawe kujitahidi kufuatilia na kupata rasimu ya pili ya
Katiba mpya ili wajue ni masuala gani ya wananchi yameingizwa humo na kuyatetea
ili yasiondolewe na wajumbe wa Bunge maalum la Katiba.
Tuna kila sababu ya kupongeza mpango
huu wa wananchi kusimama na kudai mabadiliko wao wenyewe. Kuchukua hatua ni
jambo la msingi kuliko kusubiri kusemewa na watu ambao wakati mwingine
wanaongozwa na itikadi za kisiasa au maslahi binafsi.
Tumeona matokeo ya kuwa na Bunge la
katiba lenye zaidi ya watu 600 tena wanaotokana na Bunge la kawaida ambalo
limezoea kujiendesha kisiasa. Lakini wananchi wanapoona wameachwa na sauti zao
hazisikiki wanaamua kuchukua hatua ya kupaaza sauti zao wenyewe.
Wajumbe hawa wa Bunge la katiba wanaamua
kutumia muda na rasilimali za wananchi kutetea vyeo na nafasi zao za uongozi
siziondolewe kupitia katiba mpya. Lakini hali ilivyo sasa wananchi wameamka na
wanajua haki zao wanadai mabadiliko yanayoonekana.
No comments:
Post a Comment