Thursday, August 30, 2012

Mwanamke Apigwa Na Mumewe Hadi Kuzirai Kwa Kushiriki Sensa 2012

Mkazi wa Ndembezi mjini Shinyanga amepigwa na mumewe hadi kuzirai na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutoa ushirikiano kwa karani wa Sensa ya Watu na Makazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Evarist Mangala, alisema jana kuwa mwanamke huyo, Esther Zablon (40) alipigwa juzi saa mbili asubuhi baada ya mumewe, Ismail Yahya kupata taarifa kuwa karani wa sensa alifika nyumbani kwao na mkewe kukubali kuhesabiwa na kutoa takwimu za familia yao.

Akisimulia, Kamanda Mangala alisema karani huyo alipokwenda nyumbani hapo, mume hakuwapo na kama mkuu wa kaya, Esther akazungumza na kutoa taarifa.

Alisema baada ya mume kurudi nyumbani na kugundua kuwa mkewe alikubali kuhesabiwa, alimshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha mke huyo kupoteza fahamu.

Kutokana na kipigo hicho, kwa mujibu wa Kamanda Mangala, Esther alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi na matibabu.

"Wakati mwanamke huyo akichukua fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kituoni kabla ya kufikishwa hospitalini, huku akilia kuwa sababu ya kipigo ni yeye kukubali kuhesabiwa, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa dini ya mumewe (Uislamu)," alisema Kamanda Mangala.

Hata hivyo, Kamanda alisema Esther alitoroka wodini kwa kuhofia mumewe kukamatwa na hatimaye kufungwa.
Kamanda Mangala alisema Polisi wanaendelea kumtafuta Yahya na akipatikana atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Taarifa Kwa Umma Mauaji Ya Morogoro

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauaji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).

Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.

Hivyokutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi wa kina.

Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao eneo la Msamvu, hivyo kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.

CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.

CHADEMA hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.

CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.

Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na kudondoka.

Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.

Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.

Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.

CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.

Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio cha Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.

Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la Polisi liliikubali.

Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia limekataza maandamano.

CHADEMA kikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.

Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu za misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.

Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.

Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.

Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.

Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi yafanyike kwa msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na vyombo vingine vya usafiri.

Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo yasingetokea madhara yoyote.

Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.

CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.

CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.

Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.

Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano yanayoendelea na familia.

CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.

CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio hicho.

Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe hiyo.

Tume hiyo inaendelea na mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.

CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.

CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.

Imetolewa tarehe 29 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Tuesday, August 28, 2012

Watu 73 kizimbani vita ya ardhi Dar

Watu 73 wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuwashambulia, kuwazuia polisi kufanya kazi yao, kuvamia maeneo ya watu na makosa mengine kufuatia operesheni ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo yanayomilikiwa na wengine iliyoendeshwa na manispaa ya Kinondoni, huko Nakasangwe, Kata ya Wazo wilayani Kinondoni.

Aidha watu wengine 50 wanashikiliwa na polisi kufuatia operesheni hiyo, kwa ajili ya mahojiano zaidi wakituhumiwa kutokuwa na uraia wa Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliiambia NIPASHE jana iliyotaka kufahamu maendeleo ya operesheni hiyo, ambayo mwishoni mwa wiki ililikumba pia eneo la Benaco lililoko katika kata ya Wazo jijini Dar es Salaam.

“Kwa hawa 50, kuna timu maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano zaidi kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa huenda si Watanzania, bali raia kutoka nchi jirani, na kwa hali hiyo, timu inayofanya kazi hii ya kuwahoji, inawajumuisha pia maofisa uhamiaji ambao ndiyo haswa wenye eneo lao,” alisema.

Kamanda Kenyela alisema kimsingi watu hao walikamatwa katika eneo walilolibatiza kwa jina la ‘Mungiki no go area’ lililoko kitongoji cha Kaza Raha huko Nakasangwe ambacho kilikuwa hakifikiwi na mtumishi yeyote wa serikali, mfanya biashara au mwananchi asiyefahamika nao kwa kuwa walikuwa wakiwakamata, kuwapiga na wengine kuwabaka.

Alisema kuwa kitendo cha watu hao kuwarushia mishale, mashoka na mapanga polisi kama ilivyotokea siku ya kwanza ya operesheni si tabia ya Watanzania na kwamba, miogoni mwa watu waliofanya kitendo hicho ni hao 53 wanaoshikiliwa.

Aliwaasa wananchi wote waliovamia maeneo katika Manispaa ya Kinondoni kuondoka kwa amani kwa kuwa, polisi wapo kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa sheria.

Monday, August 27, 2012

Mwanamke auawa kwa Imani za Kishirikina

Na Shomari Binda,Musoma

Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Bibi Majira mkazi wa Kata ya Nyakato katika Manispaa ya Musoma ameuwawa na Wananchi wenye hasira kali kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika Vitendo vya kishirikina.

Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii jioni ya leo mara baada ya Tukio hilo lililotokea Mchana katika Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya hiyo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi Mwandamizi Absalom Mwakyoma amesema Mwanamke huyo alifariki Dunia mara baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kupata Jeraha kubwa la panga katika upande wa kushuto wa Kichwa chake.

Kamanda Mwakyoma amesema Mwanamke huyo alivuja Damu nyingi baada ya kushambuliwa na Wananchi hao na hali yake ilikuwa mbaya zaidi mara baada ya kufikishwa katika Hospitali hiyo na alifariki baada ya muda mfupi.

Amesema si vyema kujichukulia sheria mikononi na kupoteza Uhai wa Binadamu kwa Imani za kishirikina na kusema Kitendo hicho ni kinyume cha Haki za Binadamu ambacho kinaweza kuleta Matatizo katika Jamii.
Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Mara amesema ajakipenda kitendo hicho na kukilani na kuitaka Jamii kubadilika na kujiepusha navyo kwani kunaweza kumuingiza Mhusika wa Matukio hayo katika Matatizo asiyoyategemea.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kufatilia na litamfikisha katika Vyombo vya Sheria Mwananchi yeyote atakayebainika kuhusika katika tukio hilo ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Awali wakizungumza na Mwandishi wa Habari hii katika eneo la tukio hilo,Wananchi hao wa Kata ya Nyakato walisema wameamua kuchukua Sheria mkononi kutokana na kudai kuwepo kwa Matukio ya kishirikina katika Kata hiyo huku Serikali ikisema haitambui Imani za kichawi.

Friday, August 24, 2012

Mitaala shule za msingi inawachanganya wanafunzi – Walimu

Joachim Mushi, Thehabari.com

BAADHI ya walimu wa shule za msingi wilaya za Korogwe na Moshi wamelalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala kwa shule za msingi pamoja na idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa madarasa ya chini, kuwa yamekuwa yakiwachanganya wanafunzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni walisema mabadiliko ya mara kwa mara kwa mitaala yanayofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bila maandalizi yamekuwa chanzo cha vikwazo cha kufanya vizuri kwa sekta hiyo.

Akizungumza hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Gerezani, mjini Moshi, Khadija Mtui alisema mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara yanawachanganya wanafunzi pamoja na walimu hivyo kuwa kikwazo.

Alishauri kuwepo na maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha walimu ambao ni wadau wakubwa wa sekta ya elimu kabla ya mabadiliko ya mitaala hiyo. Alisema pamoja na hali hiyo mabadiliko ya vitabu vya masomo bila utaratibu mahususi ni tatizo pia katika mafanikio ya sekta hiyo kitaaluma.

 “Mabadiliko ya mitaala na mchanganyiko wa vitabu bila utaratibu mahususi ni tatizo, kwa sasa hivi kila shule ina kitabu chake katika somo fulani…hata hivyo licha ya mabadiliko ya mara kwa mara hakuna maandalizi, mimi tangu nimalize chuo 1979 sijaenda semina yoyote wala mafunzo kujiandaa na mabadiliko ya mitaala hii. Hili linachangia pia,” alisema mwalimu Mtui.

Akifafanua zaidi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Muungano, ya wilayani Moshi, Ashati Elihaki alisema mbali na mchanganyiko juu ya suala la vitabu vya masomo mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya masomo kubaki kama ‘kiini macho’ jambo ambalo ni tatizo kwa walimu.

“…angalia kwa mfano somo kama la Tehama linaloanza kufundishwa darasa la tatu hadi la saba somo hili lipo kinadharia zaidi, hakuna walimu ambao wameandaliwa kufundisha somo hili lakini linatakiwa kufundishwa eti kwa kutumia mwongozo wa mwalimu kimsingi hii si sawa,” alisema Elihaki.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, Theodolph Karigita alisema tofauti na ilivyokuwa hapo awali mitaala ya sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo ambalo linawachanganya walimu na hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya vizuri.

“…Mitaala imevurugwa sana, kunamchanganyiko wa masomo nadhani unakumbuka kuna kipindi baadhi ya masomo yaliunganishwa kama Jiografia, Historia na Uraia wakaita maarifa ya jamii…kipindi hiki wanafunzi walifanya vibaya sana hivyo ikabadilishwa sasa watoto wanafanya vizuri tofauti na awali,” alisema Karigita.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo alisema idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu ni chanzo kingine cha wanafunzi hao kufanya vibaya kwani wamekuwa wakibebeshwa mzigo pasipo sababu za msingi.

Akizungumzia hoja hizo zilizotolewa na baadhi ya walimu, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema mabadiliko yanayofanywa na wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na changamoto kadhaa maeneo tofauti.

Wednesday, August 22, 2012

Wanaharakati waipa Serikali siku 7 kulifungulia Mwana Halisi

WATETEZI wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, leo wameipa serikali siku saba kufungulia gazeti la MwanaHALISI, vinginevyo wataitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na utesaji wa wanaharakati.

Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI ni MISA, Legal and Human Rights Centre, Tanzania Human Rights Defenders Coalition, Human Rights National Association of Educators For World Peace and Citizen Rights Watch.

Tamko la asasi hizo ni kama ifuatavyo hapa chini:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 22 Agosti 2012

YAH: KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI

KWA mara nyingine tena, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu kwa watawala. Ujumbe wenyewe unahusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyoitoa bungeni, Alhamisi tarehe 16 Agosti 2012. Kama mnakumbuka vema, wakati akijibu swali bungeni siku hiyo, Waziri Mkuu Pinda alisema, “Serikali imechukua wajibu wake kulifungia gazeti hilo, na kwamba kama wahusika hawakuridhika na hatua iliyochukuliwa na serikali wana haki ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu.”

Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatukuridhika na majibu ya Waziri Mkuu kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI. Majibu ya Waziri mkuu Pinda yamelenga kuahirisha tatizo, siyo kutatua. Kwanza, Waziri Mkuu anatetea uamuzi huo uliofanywa na sheria katili na kandamizi ya magazeti. Sheria inayonyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana. Pili, Mheshimiwa Pinda anatumia sheria hiyo kutaka kuliangamiza gazeti hili ambalo limesifiwa kwenye ripoti mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwamo ile iliyotolewa majuzi na Baraza la Habari Tanzania (MCT) inayochambua Mwenendo wa vyombo vya Habari nchini kwa mwaka 2011 inayosema katika ukurasa wa tisa:

“Pamoja na kusakamwa na serikali, MwanaHALISI limesimamia uandishi wake wa kuikosoa serikali.”
Serikali imelituhumu gazeti hili kwa kuchapisha habari ambazo inasema “zinakiuka” vifungu 32(1) (a), (c) – (d); 32(1)(c) na 36(1) vya Sheria ya Magazeti Na. 3 ya 1976. Habari hiyo inahusu kutekwa, kuteswa kinyama na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande kwa kiongozi wa madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka. Hii ndiyo habari ambayo serikali inaita ya “uchochezi.” Yaani badala ya serikali inayojigamba ina mkono mrefu wa kumfikia yeyote kuutumia mkono huo kutafuta watuhumiwa waliotajwa na gazeti kuwa walifanikisha kutekwa kwa Dk. Ulimboka, imeamua kutumia mabavu kulifungia MwanaHALISI huku wakiacha maisha ya Dk. Ulimboka na wanaharakati wengine njia panda.

Serikali imechukua hatua hiyo, huku wakijua kuwa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005), ilipanua haki ya kutoa, kutafuta, kupokea, na kusambaza habari. Mabadiliko hayo yaliondoa kivizo cha “kwa mujibu wa sheria” Kila mtu- anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

Aidha, mabadiliko hayo yanatoa haki kwa kila raia ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio muhimu mbalimbali kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii. Hivyo basi haki na uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari haina vipingamizi ambavyo serikali inadai kuwamo katika Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.

Vilevile, kuwekwa kwa Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya nchi yetu kulibadilisha sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu. Vifungu vyote tulivyovitaja hapo juu viliguswa moja kwa moja na Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu. Ibara ya 14 ya Katiba inalinda haki ya kuishi na inaitaka jamii kutoa hifadhi ya maisha kwa kila mtu. Kana kwamba hiyo haitoshi, Ibara ya 26(1) na (2) zinataka kila mtu na serikali kutii Katiba ya nchi na vilevile kuchukua hatua za kuheshimiwa haki na sheria za nchi.

Waziri mkuu anayajua haya vizuri. Anafahamu kuwa sheria iliyotumiwa kufungia gazeti, ni sheria katili na imepitwa na wakati. Kuitumia sheria hii kunaendeleza dhana ya kuwa serikali hii inatumia udhaifu wa Katiba na baadhi ya sheria kukandamiza Haki za Binadamu na Uhuru wa Habari! Mambo haya hayakubaliki.
Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:

1. Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja na bila masharti, gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi. Tunaitaka serikali ndani ya siku saba (7) kutekeleza hilo kwa kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya viongozi wenye maslahi fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.

Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo, na kwamba asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu zifuatazo:

Kwanza, sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa wahusika kusikilizwa. Pili, Waziri Mkuu Pinda pamoja na sheria hiyo kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya MwanaHALISI. Hivyo kutoelekeza kwake tunakuchukulia kama njia ya kukwepa wajibu wake.

Tatu, hatukubaliani na kauli ya Waziri Mkuu na wengine wanaoitaka MwanaHALISI waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali yenyewe haikutumia njia ya mahakama kufungia gazeti. Serikali inataka kuitumia mahakama ili kuchelewesha MwanaHALISI kupata haki yake. Nyote mnajua jinsi mahakama zetu zinavyokabiliwa na gonjwa kubwa la ucheleweshaji wa kesi.

2. Serikali, baadala ya kushughulika na watetezi wa haki na wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka. Ushahidi uliobainishwa na gazeti hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama serikali au watendaji wake waliotajwa (na waliohusishwa) wana mashaka wangetumia ushahidi na taarifa zile kutafuta haki zao: kwanini wasiende mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?

3. Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru wa habari. Matendo aliyofanyiwa Ulimboka, habari zilizobainishwa na MwanaHALISI juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru na haki.

Ikumbukwe pia kuwa, Kesi Na. 34/2009 iliyofunguliwa tangu 2009 kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuwafungia MwanaHALISI haijasikilizwa mpaka sasa. Hii inaenda sambamba na serikali kufumbia macho mahitaji ya sheria ya uhuru wa habari na kudharau mapendekezo ya muswada wa habari tangu 2007 bila kupeleka Bungeni.

Kwa hoja hizo, sisi watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, tunaendelea kusisitiza kuwa serikali itimize wajibu wake kwa kulifungulia mara moja gazeti hili na kufanyia kazi yaliyobainishwa. Kama ikishindwa kufanya hivyo, tutaitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hili, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na uteswaji wa wanaharakati na watetezi wa haki na kwamba tukifika hapo tunawaomba waandishi wa habari mtuunge mkono kwa yafuatayo.

i. Msichapishe habari yoyote inayomhusu Waziri wa Habari, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, na pia Mkurugenzi wa Maelezo. Tunawasihi wahariri wasiwatume waandishi katika Ukumbi wa Habari Maelezo kwa ajili ya kuchukua habari kama ilivyo kawaida na badala yake Watanzania wote wahakikishiwe kupata habari kwa njia nyingine mbadala.

ii. Tunawasihi wadau wote wanaoweza kutuunga mkono mara tutakapohitaji msaada wao ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maandamano na kupata mawakili ambao watasaidia katika uendeshaji wa shauri letu mahakamani.

iii. Tunawasihi wanaharakati wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.

Marcossy Albanie
Mwenyekiti wa Kamati


Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI ni MISA, Legal and Human Centre, Tanzania Human Rights Defenders Coalition, Human Rights National Association of Educators For World Peace and Citizen Rights Watch.

Tuesday, August 21, 2012

SEMINA: Jinsia na Kilimo Katika Muktadha wa Kibepari: Bajeti ya Kilimo na Chakula


SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

 UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII  Prof. Marjorie Mbilinyi na Geofrey Chambua  WATAWASILISHA


MADA:Jinsia na Kilimo Katika Muktadha wa Kibepari: Bajeti ya Kilimo na Chakula
Lini: Jumatano Tarehe 22/8//2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Sitta:Msiisubiri Serikali Kutaja Walioficha Mabilioni

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka wanaotangaza kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi kuwataja mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala ya kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini Awamu hii ya Nne imetia fora.

Utafiti huo uliofanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Akizungumza katika mahojiano maalumu, kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania isiendelee kufilisiwa na watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na watu hao kuogopa na kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale inapokuwa wahusika ni vigogo wa Serikali.

Alisema vigogo hao ni sababu ya watu kupata kigugumizi katika hili akihoji : “Kwa nini linapokuwa ni suala linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo hawatajwi?”

Sitta ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti, alisema haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje ya nchi huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha magumu.

“Watajwe! Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja na vyombo husika kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni msumeno, haipaswi kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa katika nchi.Sitta ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali la kwa nini hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”

Alisema amesikia na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja wahusika iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu yoyote ya mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.

“Haiwezekani kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”

Alisema hata kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango hicho hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”

Tuhuma hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitafanya hivyo.

Friday, August 17, 2012

Waziri Mkuu Asema Sheria Iliyotumika Kufunga Mwanahalisi Ni Halali

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kwamba mtu yoyote ambaye anona hakutendewa haki kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi anaweza kufafuta utaratibu mwingine wa kwenda mahakamani.

Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni na Waziri Mkuu Pinda wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzania Bungeni , Freeman Mbowe lililouliza kuwa Julai 30, mwaka huu, Serikali ililifungua gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana kwa kutumia sheria ya magazeti ya mwaka 1976.

Maadam katika siku za hivi karibuni serikali imetambua umuhimu wa mahakama ni

Kwanini wamelifungua gazeti hili badala ya kulipeleka mahakamani na wahusika wapate nafasi ya kujitetea kabla ya kuhukumiwa?

Akijibu swali hilo , Waziri Mkuu Pinda alisema "ni kweli serikali imechukua hatua hiyo, lakini imechukua hatua hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na mtu yoyote kwa msingi wa sheria hiyo kama anaona hajatendewa haki ni juu yake kutafuta utaratibu mwingine wa kwenda mahakamani,” alisema Waziri Mkuu Pinda.

Katika swali lake la nyongeza la kiongozi huyo lililouliza kuwa Sheria iliyotumika imekuwa ikilalamikiwa na wadau wengi na vyombo vya habari kwa muda mrefu . Je wewe huamini kwa kutumia sheria hiyo ni kunyima haki na ni msisitizo wa utawala usio bora?

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu Pinda alisema “ Mimi siamini hivyo kwa sababu sheria hiyo imetungwa na Bunge tukufu na kuwa bado inatumia ni sheria halali, sisi tutaendelea kuitumia mpaka hapo itakapobadilishwa.

Thursday, August 16, 2012

Msingi dhaifu madarasa ya awali chanzo cha wasiojua kusoma, kuandika

Na Joachim Mushi, Thehabari.com
MSINGI mbovu na dhaifu wa elimu kwa madarasa ya awali umebainika kuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi mkoani Kilimanjaro na Tanga kumaliza elimu hiyo huku hawajui kusoma na kuandika.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni katika Wilaya ya Moshi (Manispaa) umebaini idadi kubwa ya shule za msingi awali hazikuwa na madarasa ya awali kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi kujiunga na darasa la kwanza, jambo ambalo liliilazimu shule kupokea wanafunzi wa darasa la kwanza toka nje ya shule wengine wakiwa hawajaandaliwa kikamilifu.

Taarifa zimebaini vituo vingi vya shule za awali ambavyo baadhi ya shule za msingi zilikuwa zikitegemea kupokea watoto wa darasa la kwanza vilikuwa havina walimu wenye taaluma ya kuwaandaa watoto katika vituo hivyo kwa ajili ya kujiunga na darasa la kwanza.

Uchunguzi uliofanyika katika baadhi ya shule za katikati ya Mji wa Moshi (Manispaa) na pembezoni umebaini shule nyingi hivi sasa zimeanzisha madarasa ya awali ikiwa ni shinikizo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi la miaka ya hivi karibuni.

Shule ya Msingi Magereza ni miongoni mwa shule zinazofanya vibaya katika Manispaa ya Moshi, shule hii inashika nafasi ya 45 kiwilaya kati ya shule 46 za manispaa nzima. Kimkoa inashika nafasi ya 595 kati ya shule 638 japo ipo mjini ukilinganisha na zile za vijijini.

Akizungumza mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Magereza alisema awali haikuwa na darasa la awali bali ilikuwa ikipokea wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka nje ya shule. Alisema ilianzisha darasa la awali rasmi linaloendeshwa na shule hiyo Machi 1, 2012.

Taarifa zaidi zimebaini licha ya madarasa mengi ya shule za awali kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao huwa mzigo kwa mwalimu mmoja anayefundisha, mengi ya madarasa hayo yana umri kati ya miaka mitatu kushuka chini jambo ambalo linaonesha mafanikio yake hayajaanza kujitokeza.

Hata hivyo hali hiyo imejitokeza katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, kwani kati ya shule nne za msingi Silabu, Lwengera, Kitopeni na Boma ambazo mwandishi amezitembelea ni moja tu (Boma) ndio yenye darasa maalumu la wanafunzi wa awali. Uchunguzi umebaini kuwepo na shule zenye wanafunzi wa awali lakini hakuna vyumba vya kufundishia wala waalimu wenye sifa ya kufundisha kitengo hicho muhimu.

Akizungumza Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema kwa eneo lao bado suala la vyumba vya madarasa ni tatizo hivyo idara hiyo inajitahidi kulishughulikia suala hilo kwa kushirikiana na wazazi wa maeneo husika.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Manispaa, Leocadia Akaro alisema idara yao inajitahidi kuhimiza ujenzi wa madarasa ya awali na mafanikio ni makubwa kwani idadi kubwa ya shule za msingi zinamadarasa ya awali tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa ushirikiano na taasisi ya HakiElimu

Wednesday, August 15, 2012

CWT ‘yaponda’ bajeti ya Wizara ya Elimu

Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyosomwa bungeni na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, haina jipya kwa sababu imeshindwa kuzungumzia madai ya walimu yaliyowafanya wagome.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekia Oluoch, alisema bajeti hiyo imewashangaza sana walimu kwa kushindwa kuzungumzia madai yao ambayo waliahidiwa na serikali kuwa yangetekelezwa tangu Juni, mwaka huu.

“Tunamshangaa sana Dk. Kawambwa, kwa bajeti yake ambayo haina jipya. Imeshindwa kuzungumzia madai ya walimu ambayo yaliwafanya wagome na yeye mwenyewe ndiye aliyesababisha na kushindwa kulieleza Bunge,” alisema.

Alisema bajeti yake pia haijazungumzia juu ya walimu 900 kutoka vyuo vya ukufunzi ambao walitakiwa kupanda daraja.

Bajeti hiyo pia juzi ilipingwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Suzan Lyimo, kwa takwimu za serikali kuonyesha kiwango cha elimu kimepanda wakati wanafunzi 5,200 hawajui kusoma na kuandika walichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.

Lyimo alisema serikali ilitumia nguvu na vitisho kushughulikia madai ya walimu kama njia ya kuwanyamazisha badala ya kuwasikiliza na kufikia mwafaka.



Tuesday, August 14, 2012

Wasomi UDSM waikosoa bajeti ya elimu ‘live’

Na Joachim Mushi, Thehabari.com

TAASISI ya HakiElimu leo jijini Dar es Salaam imewakutanisha baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu ambapo waliishuhudia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu ikiwasilishwa ‘live’ mjini bungeni mjini Dodoma kabla ya kutoa maoni yao.

Wadau hao wa elimu kwa pamoja waliishuhudia kupitia king’amuzi bajeti ya Wizara ta Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwasilishwa ‘live’ wakiwa kwenye mkutano kisha baadaye kutoa maoni yao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa kuwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2012/13, Mhadhiri wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo alisema ameshangaa bajeti hiyo kutouona mgomo wa walimu wa juzi pamoja na migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kama ni tatizo kwa elimu na kuiingiza kama changamoto.

“Binafsi kati ya vitu ambavyo vimenishangaza ni bajeti hiyo kutotaja mgomo wa walimu katika bajeti iliyopita kuwa ni miongoni mwa changamoto za wizara hiyo…na hata migomo ya vyuo vikuu,” alisema Dk. Mkumbo alipokuwa akijadili katika mkutano huo.

Alisema wizara imetaja kufanya vizuri katika elimu upande wa msingi na sekondari kwa kidato, lakini imekwepa kutoa mafanikio kwa kidato cha tano na sita eneo ambalo limefanya vibaya kwa matokeo ya hivi karibuni. Alikosoa kiwango cha uwiano kati ya wanafunzi na walimu kilichotatolewa kwa sasa (1:46) kwani idadi kubwa ya walimu wapo shule za mjini huku hali mbaya ikiwa vijijini.

Aidha aliongeza kuwa wizara pia imeshindwa kuona migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya mara kwa mara ni changamoto hivyo kushindwa kueleza katika bajeti yake. “…karibu asilimia 80 ya migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu imesababishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, lakini hili halikutajwa katika bajeti ya waziri,” alisema msomi huyo.

Kwa upande wake Mhadhiri Adolf Mkenda kutoka Idara ya Uchumi ya UDSM akizungumza katika mkutano huo alisema bajeti iliyowasilishwa ni ya kawaida hivyo ni vigumu kumaliza changamoto lukuki za elimu zinazoikabili wizara hiyo.

Alisema bajeti imejivunia ongezeko la idadi ya vyuo vikuu lakini imeshindwa kuonesha ubora wa vyuo hivyo jambo ambalo ni hatari endapo litaachwa, bila udhibiti. “…Twaweza kuwa na vyuo vingi lakini suala la ubora ni tatizo lingine. Pia uandikishaji wa idadi kubwa ya wanafunzi unatakiwa kulinganishwa na waliokusudiwa kuandikishwa…maana twaweza jivunia kiwango kinapanda kumbe tunadanganywa na ongezeko la idadi ya watu,” alisema msomi huyo.

Akizungumza kwenye mjadala Meneja wa Kitengo cha Habari wa HakiElimu, Nyanda Shuli alisema Serikali haiwezi kufanikisha elimu bora bila kuaandaa walimu bora katika utoaji wa elimu husika. “Huwezi kutegemea elimu bora pasipo na walimu bora, binafsi sijaona mkakati wowote mahususi wa kuboresha elimu,” alisema Shuli.

Ameishauri wizara ya elimu kujiandaa vizuri kimipango kabla ya kutekeleza mpango wa kuwa na shule ya kidato cha tano na sita kwa kila tarafa ili kuepuka madudu yaliojitokeza katika mpango wa uanzishwaji shule za kata.

Hata hivyo kabla ya kuishuhudia bajeti hiyo ikiwasilishwa Dk. Mkumbo na Mkenda wakiongozwa na mhadhiri mwenzao kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano, Ayoub Rioba waliwasilisha mada zilizokuwa zikiiangalia elimu ya Tanzania na majaliwa yake.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu tayari imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/13 ambapo jumla ya sh. 724,471,937,000 ili zitumike kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake. Huku sh. 18,561,689,000 zikiwa ni fedha za ndani na sh. 74,019,627,000 kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Friday, August 10, 2012

Semina: Women Empowerment / Uwezeshaji Wanawake


SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

 UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII  Dr. DeWeever / U.S Speaker Program  ATAWASILISHA

MADA:  Women Empowerment: Uwezeshaji Wanawake

Lini: Jumatano Tarehe 15/8//2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Kukosekana viongozi wanawake Zanzibar kwachangia ukatili

WANANCHI wa mkoa wa kaskazini Unguja wamesema ni muhimu uongozi wa wilaya ya Kaskazini B, Unguja kuteua Masheha wanawake ili kudhibiti vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto (GBV) ambavyo vimeshamiri katika wilaya hiyo.

Utafiti wa kihabari uliofanywa na wanahabari huko Zanzibar unaoyesha kuwa Wilaya ya Kaskazini B, Unguja Shehia zote 29 za wilaya hiyo zinaongozwa na wanaume huku vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vikiwa ni vingi zaidi.

Mwanaharakati wa mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto katika wilaya ya Kaskazini B, Rukia Khaidar Gulam wa Bubwini, amesema matukio 108 ya ukatili wa kijinsia ukiwepo ubakaji yaliyoripotiwa katika wilaya hiyo mwaka 2011.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa ripoti utafiti huo hivi karibuni Rukia alisema baadhi ya matukio hayo yangeweza kuzuilika endapo Shehia zingekuwa zinaongozwa na wanawake wenye uelewa kuhusu athari za ukatili na jinsi ya kuepusha vitendo hivyo.

Alisema zaidi ya kesi 61 zinazohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto zimeripotiwa mwaka huu 2012 katika wilaya ya Kaskazini B na kwamba hakuna jitihada madhubuti zinazofanywa na Masheha kudhibiti uovu huo.

Mama huyo amesema kuwa viongozi Wanawake wenye mwamko na upeo kuhusu masuala ya jinsia wangeweza kutoa kipaumbele kushughulikia kesi za udhalilishaji ambazo zimekuwa zikiathiri wakaazi wa wilaya hiyo hasa wanawake na watoto.

Bwana Shaabani Juma wa Kaskazini A alisema kwa kauli kuwa wanawake hawawezi kufanya vizuri wanapopewa nafasi za uongozi zinatolewa na watu wasiothamini nafasi ya wanawake na ambao wana lengo la kuzorotesha maendeleo ya kundi hilo muhimu katika nchi.

Alitoa mfano wa Sheha wa Shehia ya Pitanazako, Acheni Machano Juma katika wilaya ya kaskazini A ambaye amesema anafanyakazi nzuri hasa ya kufuatilia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake.

Utafiti huo umebainisha kuwa wakati wilaya hiyo ya Kaskazini B, katika mkoa wa kaskazini Unguja ikiwa haina kabisa Sheha mwanamke, wilaya tisa za wilaya hiyo zilizobakia Masheha wanawake ni asilimia kati ya 3 hadi 19.

Mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake na watoto ambayo Tanzania imeridhia inaelekeza nchi kuhakikisha kuwa idadi sawa ya viongozi kati ya wanawake na wanaume.

Thursday, August 9, 2012

Wanaharakati Zimbabwe wataka kuungwa mkono

Ujumbe wa Mtandao wa Mashirika ya wanaharakati unaojulikana kama Crisis in Zimbabwe Coalition umewasili nchini kuomba ushawishi wa Tanzania katika mchakato unaoendelea nchini humo wa kabadiliko ya katiba na maandalizi ya uchaguzi wa kidemokrasia unaotarajiwa kufanyika Juni mwakani.

Zaa Twalangeti, Meneja wa Utetezi na Ushawishi wa  Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Tanzania (Tango), alisema  kuwa ujumbe huo ukiwa nchini katika ziara yake ya siku tano utakutana na mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali, vyama vua siasa na vyama vya waandishi wa habari.

Msemaji wa Crisis in Zimbabwe Coalition, Thabani Nyomi, wakati ujumbe huo ulipokutana na watendaji wa Baraza la Habari Tanzazia (MCT) alisema kuwa ujenzi wa demokrasia nchini Zimbabwe unasuasua licha ya mwafaka uliofikiwa wa kuundwa kwa serikali ya umoja.

Alisema bado uhuru wa kujieleza unabanwa kutokana na sheria mbaya zinazovibana vyombo vya habari na kuongeza kuwa wanaamini kuwa Tanzania itasaidia kutokana na msaada wake ilioutoa kwa Zimbabwe wakati wa harakati za kudai uhuru na  ushawishi wake kama mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano Kusini mwa Afrika (Sadc).

Aliongeza kuwa wana matumaini kuwa Tanzania itasaidia kwa kuwa hivi karibuni itakuwa mwenyekiti wa kmati ya ulinzi na Usalama ya Sadc, ambayo pamoja na mambo mengine, jukumu lake ni kuhakikisha nchi wanachama zinafanya chaguzi za kidemokrasia.