WANAFUNZI 200 wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya
Ulyankulu wilayani hapa mkoani Tabora, hawajaripoti shuleni kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo hofu ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni
hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa, Mkuu wa Shule
Msaidizi, Alphonce Makaza alisema kuwa mwaka huu walitegemea kuwa na
wanafunzi 602 wa kidato cha kwanza na kwamba walioripoti hadi sasa ni
wanafunzi 400.
Alisema umbali uliopo kati ya shule na makazi ya watu, unawakatisha
tamaa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike ambao wanapolazimika
kutembelea umbali mrefu wanaweza kukutana na watu wenye tabia ya
unyanyasaji wa kijinsia.
Mwalimu Makaza alitaja sababu nyingine za wanafunzi kutoripoti
shuleni kuwa ni mtazamo wa jamii kuhusu watoto wa kike kuwa hawana
umuhimu wa kusoma kama ilivyo kwa watoto wa kiume.
Aidha alibainisha kuwa mfumo wa maisha katika ngazi ya familia
unawanyima watoto hao fursa ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya
elimu na kwamba wanatumika zaidi katika shughuli za kilimo na uzalishaji
mali.
Mkuu huyo wa shule msaidizi alisema pamoja na kwamba shule hiyo ina
bweni la wanafunzi wa kike lenye uwezo wa wanafunzi 80, lakini waliopo
kwa sasa ni 46.
Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Bahati Msengi alisema kuwa
wanafunzi wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga jambo ambalo
linahatarisha usalama wa wanafunzi wa kike.
No comments:
Post a Comment