BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hazina ya Taifa inazo fedha za kigeni za kutosha za kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.
Aidha, imehadharisha kwamba taarifa zozote zisizo na ukweli
zinazotolewa kuhusu hali ya fedha za kigeni ya nchi, zinaweza kuleta
matatizo makubwa ya kiuchumi.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema jana kwamba hazina ya
taifa ina akiba ya Dola za Marekani bilioni 3.6 inayotosheleza mahitaji
ya kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.
“Akiba ya fedha za kigeni hivi sasa ni Dola za Marekani bilioni 3.6, hizi zinatosheleza kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.
Tumewahi kulisema hili, tumezungumzia haya katika Kamati ya Bunge na
hata taarifa hizi zipo IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa),” alisema
Profesa Ndulu alipozungumza na gazeti hili kwa simu.
Profesa Ndulu alisema kiasi hicho cha hazina ya taifa kinakidhi
vigezo vya IMF ambavyo vinataka akiba hiyo itosheleze mahitaji ya nchi
husika siyo chini ya miezi mitatu. Aliongeza kuwa hata pamoja na ukweli
kwamba thamani ya Euro imeshuka duniani, lakini hali hiyo haijaathiri
hazina hiyo ya Taifa, na kwamba uingizaji wa bidhaa ndani ya nchi
umeongezeka.
Gavana huyo alitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti hili kutaka kujua
ukweli wa hazina ya taifa na hasa kutokana na taarifa ya Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), akihoji ukimya wa BoT katika
masuala mbalimbali ikiwamo hazina hiyo na taarifa zinazohusu uchumi hasa
suala la mfumuko wa bei.
“Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni –
foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa
mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika
tovuti ya Benki Kuu ili kupata habari rasmi (authoritative) nimekuta
takwimu za Novemba 2011,” alieleza Zitto katika taarifa hiyo aliyoituma
kwa vyombo vya habari. Hata hivyo jana jioni BoT iliongeza taarifa za
Januari mwaka huu.
“Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya
Tanzania ni ya Novemba mwaka 2011! Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya
Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Novemba
mwaka 2011.
“Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya
mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri
urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki
Kuu.Taarifa zinafichwa,” alidai Zitto na kumshauri Profesa Ndulu.
“Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi
imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki
inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi
yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni
muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge,
Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.”
Hata hivyo, katika ufafanuzi wake Profesa Ndulu alisema
wamebadilisha mfumo wa utoaji wa taarifa kila mwezi na sasa wanatoa kila
baada ya miezi miwili na kwamba Kamati maalumu ilikutana Februari mwaka
huu na taarifa zake zilitarajiwa kuwekwa katika tovuti ya benki hiyo
jana.
“Tumebadilisha mfumo wa Kamati ya Sera ya Fedha ambayo sasa
inakutana kila baada ya miezi miwili…mara ya mwisho ilikutana Februari
na leo (jana) taarifa zao zitakuwa katika website (tovuti). Kulikuwa na
matatizo ya kiufundi, lakini taarifa hizo zitakuwapo pamoja na taarifa
rasmi kuhusu hazina ya taifa,” alisema Gavana.
Lakini Profesa Ndulu alionya kuwa si vyema kutoa taarifa zisizo
sahihi zinazoweza kusababisha matatizo ya kiuchumi, ikiwamo soko la
kubadilisha fedha kwenda ovyo na hivyo thamani ya Shilingi kuporomoka
ghafla.
No comments:
Post a Comment