WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amewataka Watanzania kujenga
ujasiri kukabiliana na rushwa, huku akiwataka viongozi kuwa mfano katika
hilo kwa lengo la kulikomboa Taifa kutokana na hali ya umasikini.
Sumaye aliyazungumza hayo jana wakati wa muda wa ‘Busara za kiongozi’ iliyofanyika katika
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe jijini Dar es Salaam, linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima.
Katika busara zake alizozitoa kwa zaidi ya nusu saa, Sumaye alisema
matatizo mengi yanayoikumba nchi, yanasababishwa na viongozi wengi wa
nchi kukumbatia vitendo vya rushwa huku wakiwaacha wananchi wao
wakihangaika.
“Japo kuna gharama zake katika kuzungumzia suala hili, ukweli upo wazi kuwa rushwa,
ufisadi utajiri kwa watu wachache ni matatizo yanayolifanya Taifa
hili liendelee kukandamizwa hivyo ni lazima tuwe wajasiri dhidi ya mambo
yote mabaya ili tuweze kulikomboa,” alisema Sumaye na kuongeza: Huku
akitumia vifungu mbalimbali vya Biblia, Sumaye alisema maendeleo ya nchi
yanayoliliwa yamesababishwa na baadhi kuwapa nafasi ya kuongoza
viongozi wanaoingia madarakani kwa kutoa rushwa.
Alisema japo wananchi wengi wamekuwa wakishawishika kupokea rushwa kutokana na hali
yao ya umasikini, wanapaswa kubadilika kwa kuepuka kuwachagua
viongozi hao ili wasije kujutia kwa kutopata maendeleo pindi kiongozi
huyo anapokuwa amechaguliwa.
“Nikisema msipokee bahasha ni sawa na kubeba maji katika gunia, kikubwa ukipokea fikiria
mambo mengi atakayokutendea kiongozi huyo ukijua wazi kuwa kwanza
lazima atafute fedha alizowapatia wakati wa kutafuta kura kabla ya
kuanza kuwaletea maendeleo,” alisema Sumaye.
No comments:
Post a Comment