Serikali imeombwa kuendelea kuifanyia marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayosimamia mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya kwa lengo la kupata Katiba bora na inayoakisi maoni ya wananchi wote.
Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Mei 21, 2012) Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Jukwaa hilo Bw. Hebron Mwakagenda alisema ingawa kwa ujumla sheria hiyo ni nzuri, lakini ina mapungufu yanayohitaji kurekebishwa ili kuufanya mchakato huo kuwa huru zaidi.
“Kwanza tunadhani Tume imepata Wajumbe wenye sifa na weledi wa kufanya kazi na kupata Katiba nzuri wakiwemo wajumbe wa Jukwaa wawili walioteuliwa kupitia asasi nyingine,” alisema Bw. Mwakagenda alipomtembelea Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias Chikawe ofisini kwake.
Kwa mujibu wa Bw. Mwakagenda, pamoja na uzuri huo, baadhi ya vifungu katika sheria hiyo kikiwemo kifungu cha 21 kinachozuia wananchi kukusanya na kutoa maoni kinyume na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunadhani kifungu hiki inabidi kibadilishwe ili kuzungatia matakwa ya Katiba,” alisema Bw. Mwakagenda ambaye aliongozana na wajumbe wengine watano kutoka Jukwaa hilo.
Wengine ni Bi. Ussu Mallya, Bw. William Kahale, Bi. Sara Mkenda, Bi. Gloria Mafore na Bw. Almando Swenya.
Pamoja na mambo mengine, kifungu hicho kinatoa adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya shughuli ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kinyume na Sheria hiyo.
Bw. Mwakagenda pia alipendekeza kuwa kifungu cha 22 cha Sheria hiyo kifanyiwe marekebisho na kujumuisha makundi mbalimbali ya kijamii kutoka nchini kote yaingizwe.
Kwa upande wake Bi. Mallya alipendekeza Serikali kuendelea kuzingatia usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu yake hasa katika uteuzi wa nafasi muhimu.
“Ukiangalia wajumbe wa Tume, kuna wanawake 10 na wanaume 20, nadhani wakati mwingine Serikali izingatie usawa,” alisema Bi. Mallya.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Chikawe alisema ni nia ya Serikali kuona Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawezeshwa ili itekeleze majukumu yake kwa uhuru.
“Serikali kupitia Mheshimiwa Rais ndiyo iliyoanzisha mchakato huu.
Ni nia yake kuona jukumu hili linatekelezwa kwa uhuru na wazi ili tupate Katiba nzuri,” alisema Waziri Chikawe na kuongeza:
“Hili la usawa wa kijinsia tunakwenda vizuri na kama unavyofahamu tumeongeza usawa kwa kiasi kikubwa. Ni dhamira ya Serikali kuona tunasonga mbele zaidi…sasa tuna kiongozi wa mhimili mwanamke,” alikumbusha Chikawe.
Pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali, Waziri Chikawe aliwasihi wadau mbalimbali kupelekeza maoni yao kwa Tume hiyo yenye ofisi zake jijini Dar es Salaam.
“Kile ni chombo huru, wadau mbalimbali wasisite kwenda na kutoa maoni yao kwa uhuru,” alisema Chikawe aliyeteuliwa hivi karibuni kuongoza Wizara hiyo kutoka Ofisi ya Rais, Utawala Bora.
No comments:
Post a Comment