Thursday, May 17, 2012

Chadema ‘wamvaa’ Shibuda

BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha) limeeleza kushitushwa na kauli ya Mbunge wake wa Maswa Mashariki, John Shibuda kwamba atagombea urais mwaka 2015 kwa tiketi ya Chadema.

Akiwa kwenye semina ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyoandaliwa na Taasisi ya Kutathmini Utawala Bora Afrika (APRM) juzi Dodoma, Shibuda alisema atafanya hivyo na kumwomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake. Kikwete atakuwa amemaliza muda wake wa uongozi.

Taarifa iliyotolewa jana na Bavicha ikiwa imesainiwa na John Heche ambaye ni Mwenyekiti wake, ilieleza kushangazwa na kutoa kauli hiyo katika kikao cha NEC ya CCM; kumtangaza Kikwete kuwa meneja wake wa kampeni na kusema hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi zaidi ya CCM, na kutoa kauli kwa niaba ya APRM.

“Mambo hayo manne ndiyo yametushtua na kutufedhehesha sana sisi vijana wa Chadema na ndiyo maana tumelazimika kutoa kauli kuhusu suala hili,” ilisema taarifa.

Ikifafanua kuhusu kauli yake, Bavicha ilisisitiza kwamba kamwe haitaruhusu mgombea urais wa Chadema awe na Meneja wa Kampeni ambaye ni Mwenyekiti wa CCM hata siku moja, “ kwani tunao watu wa kutosha na wenye uwezo wa kutosha kufanya kazi hiyo na hatuhitaji msaada huo.”

Taarifa pia ilisema haitaruhusu mgombea urais wa Chadema awe anatangaza nia kwenye vikao vya CCM, kwa kuwa chama hicho tawala hakina mamlaka ya kuteua mgombea wa Chadema. “Kama Shibuda alikuwa hajui hilo, anapaswa kulifahamu kuanzia sasa, kuwa vijana wa Chadema hatuchaguliwi mgombea na NEC ya CCM, kwani Chadema kuna vikao na taratibu zetu za kuteua wagombea,” ilisema taarifa.

Kuhusu kauli ya kutokuwapo chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi, taarifa ilisema ni kudhalilisha vijana wa Chadema na Watanzania ambao wanaiona Chadema kama tumaini pekee la kuwakomboa.

“Kauli hii tunaamini vijana wa Chadema, kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuiachia bila kutakiwa maelezo ya kina, tutaitisha kikao cha Baraza na tutaijadili na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama,” ilisema taarifa ya Bavicha.

Walimwambia Shibuda, kuwa kama anaona haendani na utamaduni wa chama hicho na kuwa hakina uwezo wa kuongoza Dola aondoke.

“Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza Dola, kwani lengo la chama chochote ni kuchukua Dola na si vinginevyo”.

Taarifa hiyo iliwahakikishia vijana nchini, kwamba wawe tayari kwani Chadema imejiandaa kikamilifu kuongoza Dola na kwamba wasiwe na hofu na maneno yaliyotamkwa na Mbunge huyo.

Heche katika taarifa hiyo, aliwataka vijana wote Chadema wajiandae kukabiliana na mtu yeyote atakayeonekana kuwa kikwazo kwa chama chao kuelekea kuchukua Dola mwaka 2015.

No comments: