CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wazi masuala kitakayotetea kuwa
katika Katiba mpya huku kikiruhusu wananchi kuamua kuhusu masuala ya
madaraka ya Rais na uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi.
“Sisi CCM tumeona suala hili tuwaachie wananchi walijadili na kuamua
wenyewe wanaona Rais apewe madaraka ya aina gani. Ni fursa yao
kupendekeza apunguzwe, aongezwe madaraka au madaraka yake yaweje,”
alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye.
Katika eneo la Tume Huru ya Uchaguzi, Nape aliyezungumza na vyombo
vya habari jana, alisema eneo hilo limekuwa gumzo hasa nyakati za
uchaguzi huku malalamiko mengi yakiegemea katika utaratibu uliotumika
kuteua wajumbe wa Tume hiyo.
Alisema mapendekezo hayo yaliamuliwa katika semina ya wajumbe wa NEC
kuhusu mchakato wa Katiba mpya iliyomalizika hivi karibuni Dodoma.
“Chama kimeona suala hilo lijadiliwe na wananchi na wapendekeze
utaratibu mwafaka wa kuteua Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema Nape.
Alitaja masuala mengine ambayo chama hicho kimeona wapewe wananchi
fursa ya kuchangia maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi na
ikiwezekana yabadilishwe, kuwa ni masuala yanayosababisha kero za
Muungano na utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Uteuzi wa mawaziri Alitaja pia maeneo ya kujadiliwa kuwa ni eneo la
uteuzi wa mawaziri, waziri mkuu, muundo wa Bunge, Baraza la Wawakilishi
na aina ya wabunge na wawakilishi, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi
wa Rais ambapo kwa sasa, mfumo hauruhusu suala la mgombea binafsi.
“Kuna watu wanadhani kuwa CCM inaogopa mgombea binafsi, si kweli,
hatuna tatizo na hilo na ndiyo maana tumeliweka hili watu walijadili na
kuamua watakavyo, ingawa kwa mtazamo wangu, mgombea binafsi ni kitanzi
kwa upinzani,” alisema.
Aidha alitaja maeneo mengine kuwa ni uwepo wa Baraza la pili la
Kutunga Sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, nafasi ya Rais wa Zanzibar
katika uongozi wa Serikali ya Muungano na mfumo wa Mahakama.
Pia chama hicho kilitoa mapendekezo yake juu ya masuala ya msingi
yanayofaa kuingizwa kwenye Katiba, kuwa ni pamoja na maadili ya viongozi
kupewa nguvu kikatiba na Serikali kuendelea kuwa mmiliki mkuu wa
rasilimali zote za nchi.
Katika masuala ya msingi ya kuingizwa katika Katiba yaliyopendekezwa
na chama hicho, ilikuwa suala la maadili ya viongozi kuingizwa na
kutambuliwa kikatiba ili kudhibiti wabadhirifu na wasio na maadili, kwa
kuwa kwa sasa hata Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi haina meno ya
kutosha kama inavyotarajiwa.
“Kutokana na yaliyotokea juzi ya mawaziri kuhusishwa na ubadhirifu
wa fedha za umma, ni vema suala hili la maadili likajengewa nguvu ya
kikatiba, kuliko ilivyo sasa lakini pia sera ya sasa ya Serikali kuwa
mmiliki wa rasilimali kuu za nchi, iendelee hususan eneo la ardhi,”
alisisitiza.
Serikali mbili Aidha, alitaja maeneo mengine ambayo chama hicho
kimependekeza yaingizwe kwenye Katiba mpya kama msimamo wake, kuwa ni
kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kubaki na muundo
wa serikali mbili ya Muungano na ya Zanzibar.
“Serikali mbili ndiyo sera ya CCM, tumejadili na kuona haina
upungufu, ila ukumbi uko wazi kwa wanaoona tofauti kutoa maoni yao kwa
Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba Mpya,” alisema.
Alitaja maeneo mengine yaliyopendekezwa kuingizwa kwenye Katiba mpya
kuwa ni kuendelea na mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama),
kuendelea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na umoja wa kitaifa,
amani, utulivu, usawa na haki.
Maeneo mengine aliyotaja ni kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalumu na kuzingatia haki ya kupiga kura.
“Eneo hili limetujengea heshima kidemokrasia, kwani kuna nchi
ambazo marais wao wako madarakani muda mrefu na hawataki kuondoka.”
Katika kipengele cha uchaguzi mdogo alisema CCM ilishatoa msimamo
wake, ambapo ilipendekeza inapotokea mbunge amefariki dunia au
kung’olewa madarakani kisheria, chama kilichokuwapo madarakani kipewe
nafasi ya kuteua mrithi wake kama inavyofanyika sasa kwa wabunge wa viti
maalumu. “Tulishasema hili tukaambiwa CCM tunaogopa uchaguzi mdogo.”
Aidha, Nape alitaja maeneo mengine ya kuingizwa kwenye Katiba, kuwa
kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa haki za binadamu, kuheshimu usawa
mbele ya sheria, kuendeleza sera ya Dola kutokuwa na dini rasmi na
kuruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka.
Maeneo mengine ni kuimarisha madaraka ya umma, kuhamasisha sera ya
msingi wa kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake,
watoto na makundi mengine maalumu katika jamii, kusimamia hifadhi ya
mazingira na kuendelea kuwapo kwa Rais Mtendaji.
Nape alisema mapendekezo hayo yataandaliwa kimaandishi na
kukabidhiwa kwa Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba
Mpya na masuala ya kujadiliwa yatapelekwa kwa wanachama wa chama hicho
ili waweze kujiandaa kuchangia.
No comments:
Post a Comment