RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (73) amepanda kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kumtetea
aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu
anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Katika kesi hiyo, Profesa Mahalu anadaiwa kuiibia Serikali Sh.
bilioni 2 katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Huku Mahakama hiyo ikiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, Mkapa
aliwasili saa 4.45 na kutoa ushahidi kuanzia saa 5.32 asubuhi na
kumaliza saa 7.08 mchana.
Katika ushahidi wake, Mkapa alimmwagia sifa Profesa Mahalu kuwa ni mchapa kazi, mwenye heshima na mwaminifu mkubwa.
Alidai kuwa hajui aliyemshitaki mahakamani ni nani kwa sababu mpaka
anaondoka madarakani, mchakato wa ununuzi wa jengo hilo anajua ulikwenda
sawa.
“Namfahamu Balozi Mahalu kama msomi mzuri, mtumishi mwadilifu …na
balozi wetu Bon, Ujerumani,” alidai mahakamani Mkapa alipoulizwa
anamfahamu vipi Profesa Mahalu.
Huku akiongozwa na Wakili wa Upande wa Utetezi, Alex Mgongolwa mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta; mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Mwaka 1995 hadi 2005 ulikuwa wapi?
Mkapa: Nilikuwa Dar es Salaam nikishika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania.
Alipoulizwa uzoefu wake katika mambo ya kimataifa, alifafanua kuwa
alipata kuwa Ofisa wa Mambo ya Nje na Balozi wa Tanzania katika nchi za
Nigeria, Canada na Marekani.
Wakili: Ukiwa Rais unafahamu nini kuhusu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia?
Mkapa: Nilifahamu Balozi wetu alifanya ununuzi wa jengo kwa euro
3,098,741.40 kwa maagizo ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa wakati huo
alikuwa Profesa Mahalu.
Wakili: Katika ununuzi mlipewa masharti yoyote?
Mkapa: Ndio, mimi nilielezwa kuwa mmiliki wa jengo alitaka alipwe
mara mbili, kiasi kimoja akaunti moja na kiasi kingine akaunti nyingine
na akaunti zote ni za mtu mmoja ambaye ndiye mmiliki wa jengo.
Maelezo mengine ya Mkapa
Mkapa aliendelea kudai kuwa Serikali ilitoa baraka na yeye
alitaarifiwa na hakuzuia, kwa sababu nia yake ilikuwa ni kupata jengo
kwa ajili ya ofisi za ubalozi, hivyo masharti hayo hayakuwa kizuizi
kwake.
Kuhusu mikataba miwili iliyosainiwa katika ununuzi wa jengo hilo,
Mkapa alidai kuwa yeye hakumbuki kama alijulishwa, anachojua ni kwamba
fedha zingelipwa katika akaunti mbili.
Amshangaa Lumbanga
Rais huyo mstaafu alidai kumshangaa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi
ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo,
Matern Lumbanga, kwa madai yake mahakamani hapo kuwa Serikali haitambui
ununuzi wa jengo hilo.
“Namshangaa sana, kwa nini alisema hivyo wakati mimi Rais nilikuwa na taarifa!” Alisema huku akionesha mshangao.
Mkapa katika ushahidi wake alidai kuwa angeweza kuzuia ununuzi wa
jengo hilo, lakini aliona umuhimu wa kulinunua akatoa amri linunuliwe,
ingawa nchi ilikuwa kwenye matatizo ya fedha na fedha za ununuzi huo
zingeweza kwenda katika mambo mengine.
JK atajwa
Mkapa alipewa taarifa ya kumbukumbu za Bunge ambamo Waziri wa Mambo
ya Nje wa wakati huo (Rais Jakaya Kikwete), akitoa taarifa bungeni kuwa
mwaka 2001/02 wizara hiyo ilinunua jengo hilo la ofisi ya ubalozi Italia
kwa Sh bilioni 2.9.
Kikwete katika taarifa hiyo ya Bunge, alieleza kuwa lengo ni
kuondokana na adha ya kupanga kwenye majengo ya watu na kwamba ununuzi
wake ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na ushauri wa watathimini wa
Wizara ya Ardhi na Wizara ya Ujenzi.
Baada ya kusomewa taarifa hiyo, Mkapa aliulizwa na Wakili Mgongolwa
kama kuna usahihi katika taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati
huo, akajibu kuwa taarifa hiyo ilikuwa sahihi na ndicho anachotambua
yeye akiwa Rais wakati huo.
Mkapa alipoulizwa kama kuna malalamiko yoyote kuhusu mchakato wa
ununuzi wa jengo hilo yaliyotolewa na Serikali ya Italia au mmiliki wa
jengo kuwahi kuyapata baada ya ununuzi, alijibu kwa kifupi. “Hapana.”
Kuhusu mawasiliano kati ya Serikali na Balozi Mahalu, Mkapa alidai
kuwa balozi anaweza kuandika barua kwa waziri wake ambaye ni wa Mambo ya
Nje, au Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Rais moja kwa moja na kuongeza kuwa
mawasiliano mengine yanaweza kufanyika kwa mdomo tu.
Aliongeza:“Inategemeana na unyeti wa jambo mnalowasiliana.”
Mawakili wa Serikali
Katika maswali na majibu na mawakili wa Serikali, Wakili Vincent
Haule alitaka kujua tofauti kati ya kiwango alichodai kufahamu cha
ununuzi wa jengo hilo cha euro milioni 3.09 na kiwango kilichotajwa
bungeni kuwa ni gharama ya jengo hilo Sh bilioni 2.9.
Mkapa alijibu kuwa yeye mambo ya viwango vya kubadilisha fedha
hakuyajua kwa wakati huo, ndiyo maana akataja bei aliyokuwa akiijua na
kwamba hiyo haikuwa kazi yake kujua.
Ashtuka Mahalu kushitakiwa
Mkapa alidai kuwa hajui aliyeagiza upelelezi dhidi ya ununuzi wa
jengo hilo na pia hajui kama upelelezi ulifanywa akiwa madarakani au la,
ila alipata taarifa za kushitakiwa Mahalu siku aliyoletwa mahakamani
kusomewa mashitaka na pia aliona kwenye magazeti kesho yake.
Alipohojiwa na Wakili Haule kuhusu ruhusa aliyoitoa kwa mdomo kwa
Mahalu kama ilikuwa ya kuridhia mikataba miwili au kuingiza malipo ya
jengo katika akaunti mbili alijibu: “Mimi niliagiza ununuzi huo mambo
mengine sijui, si kazi yangu mambo ya makaratasi.
“Nilitoa maelekezo … utekelezaji ni kazi ya wizara, lakini mwisho tulipata ubalozi nilioutaka,” alisisitiza Mkapa.
Alipohojiwa na Wakili Ponziano Lukosi kuhusu uhusiano wake na
Lumbanga, Mkapa alidai alimwamini Katibu Mkuu Kiongozi huyo wa zamani na
kumshirikisha katika mambo yote na pia alijua ununuzi wa ubalozi si
Italia tu, ila ni pamoja na Marekani, Uingereza na India na akashangaa
kudai kwake mahakamani hapo kuwa hajui.
Alipoulizwa kama anakumbuka jengo lingine walilowahi kununua kwa
mfumo huo wa kuingiza fedha katika akaunti mbili, alijibu kwa ukali
kidogo; “nakumbuka lakini siwezi kusema…kwa sababu mambo mengine
yanaweza kuharibu uhusiano wa nchi na nchi.”
Baada ya kuonesha ukali kidogo, Hakimu Mgeta aliuliza kama mazingira hayo yapo na Mkapa akajibu kwa kifupi: “Yapo”.
Akijibu swali la Lukosi, aliyetaka kujua kama kulipwa katika akaunti
mbili muuzaji wa jengo hilo, haoni kuwa alikuwa akikwepa kodi katika
nchi yake, alijibu: “Nitasema kuwa hilo ni tatizo la nchi yake, mimi
nimepata jengo nililolitaka nasema alhamdulilah!”
Kuna wizi?
Akijibu swali la mwisho la Lukosi kuwa kwa ulipaji huo wa akaunti
mbili haoni kuwa ulikuwa ni wizi wa mshitakiwa Mahalu, alijibu;
“nitashangaa sana na nitakushangaa wewe, Mahalu ni mwaminifu sana.”
Baada ya jibu hilo, Mkapa alitaka kuongeza neno, lakini akasita
akidai: “Unanichokoza utanifanya niongee mengine mengi (anacheka).”
Kesi hiyo inaendelea leo mahakamani hapo ambapo mshitakiwa wa pili,
Grace Martin ambaye alikuwa ofisa wa ubalozi Italia atatoa ushahidi
wake.
No comments:
Post a Comment