CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kilikuwa katika furaha
baada ya Mbunge wake wa Ubungo, John Mnyika kuthibitishwa na Mahakama
Kuu kuwa Mbunge halali wa Ubungo jijini Dar es Salaam.
Ubunge wa Mnyika ulikuwa unapingwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng’humbi.
Mahakama hiyo jana kupitia kwa Jaji Upendo Msuya, ilitamka kuwa
uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni
halali.
Aidha, Jaji Msuya alisema maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo
ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa kwa kuwa
hakuthibitisha madai yake na kutakiwa kulipa gharama za kesi hiyo
aliyoifungua mwaka 2010, siku chache baada ya kubwagwa na kijana huyo.
Awali kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mahakama hiyo jana ilijaa
wanachama na wapenzi wa Chadema na CCM na kusababisha askari Polisi
kufanya kazi ya ziada ya kutanda kila mahali katika mahakama hiyo na
katika Barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari
ili kuimarisha ulinzi.
Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Msuya mahakamani hapo kwa takribani saa
moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi ambapo pia amuru gharama za kesi
hiyo kubebwa na Ng’humbi ambaye kabla ya kuwania ubunge mwaka 2010,
alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Jaji Msuya alisema Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna
hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika
kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na
kutoa ushahidi kuonesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.
Alisema Ng’humbi na mashahidi wake aliowaita mahakamani,
hawakuonesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa hapo kwamba
yalitendeka na namna gani madai hayo yaliathiri matokeo ya uchaguzi
uliofanyika Oktoba 31, mwaka juzi.
“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na
vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii, lakini nimeshangaa
ni kwa nini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika
chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,”
alisema Jaji Msuya.
Alisema hakuelewa ni kwa nini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha
ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na kuhoji kama kweli madai hayo
yalitokea, ni kwa nini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba
cha majumuisho hawakulalamika?
Katika madai ya Ng’humbi ya dosari ya kura zaidi ya 14,000 alizodai
hazieleweki zimetoka wapi, Jaji alisema alipata nafasi ya kuhesabu kura
walizopata wagombea wote wa vyama vilivyogombea jimbo hilo ambavyo ni 16
na kubaini ilikuwa ni kosa tu la kibinadamu na halina uhusiano wowote
na mdaiwa wa pili, Mnyika.
Kwa mujibu wa Jaji Msuya, fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo
ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi kwa kuwa ilikosewa kuandika.
Alisema Mnyika alitangazwa kuwa ni mshindi baada ya kupata kura
66,742 wakati Ng’humbi alipata kura 50,544 na wagombea wote kuwa kura
132,496.
Jaji Msuya alisema katika ushahidi wa Ng’humbi, hakuonesha ni vipi
ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na vipi Mnyika
alihusika na ongezeko hilo.
Kabla ya kuanza kuchambua hoja za Ng’humbi, Jaji Msuya aliwapongeza
mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na
kuhoji maswali ya msingi.
Alisema mawakili hao hawakupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na
msingi wala kuwasilisha pingamizi zinazosababisha shauri kuwa na
mlolongo mrefu.
Mnyika aliwakilisha na wakili Edson Mbogoro wakati wakili wa
Ng’humbi alikuwa Issa Maige na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
aliwakilishwa na Justus Mlokozi.
Kuhusu madai ya Ng’humbi kuwa alidhalilishwa kwa kuitwa fisadi na
Mnyika katika mkutano alioufanya katika kampeni kwamba aliuza nyumba ya
Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu
wasichague CCM inakumbatia mafisadi, Jaji Msuya alisema hayakuwa na
ushahidi.
Alifafanua kwamba Ng’humbi alidai maneno hayo yalizungumzwa na
Mnyika katika mkutano uliokuwa na watu zaidi ya 500, lakini yeye
hakuwapo. Kutokana na kukosekana kwa uwepo wake, Jaji Msuya alisema
Mahakama haichukui maneno ya kuambiwa, bali mtu aliyesikia mwenyewe au
kushuhudia.
“Katika watu wote hao 500 waliokuwa katika mkutano huo, hakuja hata
mtu mmoja kutoa ushahidi na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri
uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.
Kuhusu madai kwamba Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa Chadema
katika kujumlisha matokeo, Jaji Msuya alisema ushahidi pekee ni wa
Ng’humbi na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika
kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi.
Alisema mbali na ulinzi, hata wagombea wengine wangelalamikia jambo
hilo, lakini Ng’humbi hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho
kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.
Kuhusu madai kuwa Msimamizi wa Uchaguzi alitumia kompyuta za mkononi
(laptop) za Mnyika badala ya kompyuta rasmi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) na pia hazikukaguliwa kiasi cha kutia shaka kuwa pengine
kulikuwa na taarifa zisizo rasmi katika kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na
ongezeko lile la kura 14,000, Jaji Msuya alisema ushahidi umeonesha
kuwa kompyuta hizo hazikutumika.
Alifafanua kwamba kompyuta zilizotumika zilikuwa za mawakala na
kwamba katika madai hayo, Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi
kuthibitisha akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu.
“Tofauti ya kura kama nilivyosema nimepiga hesabu na nimeona kuwa ni
matatizo ya kibinadam na hakuna athari yoyote katika matokeo ya
uchaguzi, ni shahidi wa tatu pekee aliyekuja kutolea ushahidi hili na
Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi,” alisema Jaji Msuya ambaye
alianza kuisikiliza kesi hiyo kuanzia Aprili 19, mwaka huu na majumuisho
ya pande zote yalifanywa Mei 4, mwaka huu.
Baada ya hukumu hiyo, Mnyika alikumbatiana na Mwenyekiti wa Taifa wa
Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuwapo mahakamani hapo. Pamoja
walitoka nje, Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema wakiimba na
kushangilia kwa ushindi huo.
Hata hivyo, hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.
Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi
ya Sh bilioni mmoja na kutaka kabla ya kusikiliza kesi kama hiyo,
uchunguzi ufanyike kwanza ili ikionekana haina hoja za msingi, itupwe
mapema.
“Mahakama imetenda haki na hii inaonesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani,” alisema Mbowe.
Naye Ng’humbi alisema amepokea uamuzi uliotolewa, lakini hawezi
kusema lolote kwa sasa na kuwataka wana CCM wawe na utulivu kwa sababu
anaamini ni watulivu na kama kuna jambo tofauti, atazungumza baadaye.
Hadi sasa, Mahakama imekwisha kutengua matokeo ya ubunge ya mwaka
2010 katika majimbo mawili pekee, Arusha Mjini kwa Godbless Lema wa
Chadema na Sumbawanga Mjini lililokuwa la Aeshi Hilary wa CCM.
Majimbo ambayo kesi zao zilitupwa na mahakama na wabunge wake
kuendelea na nafasi zao ni Segerea, Kasulu Mjini, Biharamulo, Singida
Mashariki, Ilemela, Nyamagana, Kilwa Kusini, Muhambwe na Meatu.
No comments:
Post a Comment