Friday, May 4, 2012

Rais Kikwete ateua wabunge wapya

WAKATI kukiwa na shauku ya kutaka kujua Rais Jakaya Kikwete atakuja na Baraza gani la mawaziri, amefanya uteuzi wa wabunge watatu wapya.

Amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka ya uteuzi aliyonayo chini ya Ibara ya 66(i) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, iliwataja wateule hao kuwa ni Profesa Sospeter Muhongo, Janet Mbene na James Mbatia. Uteuzi huo unaanza mara moja.

Kuteuliwa kwa wabunge hao watatu kunaleta hisia kuwa huenda miongoni mwao wakapata nafasi ya kuwa mawaziri kama Rais atafanya mabadiliko katika Baraza lake kutokana na tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa baadhi ya mawaziri wake.

Kwa mujibu wa Ibara iliyotajwa hapo juu, Rais ana mamlaka ya kuteua wabunge 10 kujiunga na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wabunge hao walioteuliwa wanafanya idadi ya waliokwishateuliwa kufikia sita.

Wengine wa awali ni Zakia Hamdan Meghji, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa ambaye hivi sasa ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanadai kuwa uteuzi huo unaonesha dalili zote za Rais kuwa tayari kutangaza mabadiliko katika Baraza lake, katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pia ripoti tatu za Kamati za Bunge za mwaka 2009/10, ambazo zimependekeza kuwajibishwa kwa baadhi ya watendaji serikalini, wakiwamo mawaziri wanane.

Taarifa iliyowasilishwa katika mkutano uliopita wa Bunge, ilizua mjadala mkali miongoni mwa wabunge hata kufikia kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hata hivyo, lengo lao lilikuwa ni kushinikiza mawaziri waliotajwa kwa ubadhirifu na CAG wajiuzulu kama si kuondolewa.

Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi anakuwa mpinzani wa pili kuteuliwa na Rais Kikwete tangu aingie madarakani mwaka 2005.

Mpinzani wa kwanza kuteuliwa na Kikwete ni Ismail Jussa Ladhu wa CUF, ambaye ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Zanzibar ambaye aliteuliwa katika muhula wa kwanza wa Rais Kikwete.

Hii ni mara ya pili kwa Mbene kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge na hivi karibuni aligombea ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM lakini hakufanikiwa.

Profesa Muhongo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye anateuliwa kwa mara ya kawanza, ni Profesa wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini; mjumbe wa Taasisi ya Kitaaluma ya Jiolojia ya London, Uingereza; Mjumbe wa Heshima wa Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya China, Mjumbe wa Heshima wa Taasisi ya Kitaaluma ya Sayansi ya Nchi Zinazoendelea (FTWAS).

Pia ni mjumbe wa Taasisi ya Kitaaluma ya Jiolojia ya Afrika (FGSAf) na Mjumbe wa taasisi zingine nane za kitaaluma za Sayansi duniani.

Alikuwa mtu wa kwanza kushinda tuzo ya Robert Shackleton mwaka 2004 baada ya kufanya utafiti kuhusu Jiolojia Afrika. Ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ramani ya Jiolojia ya Dunia (CGMW). Hakupata kuingia katika masuala ya siasa huko nyuma.

Mawaziri ambao walitawala mjadala wa Bunge huku wabunge wakiwatolea macho ili wang’oke ni Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, William Ngeleja (Nishati na Madini), Omari Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Waziri wa Viwanda na Biashara).

Hata hivyo taarifa ya Ikulu haikusema wabunge hao wateule wataapishwa lini na wapi, lakini Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alipoulizwa jana alisema alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, mtu yeyote anayeteuliwa kuwa mbunge, ataapishwa katika mkutano wa Bunge unaofuata baada ya uteuzi wake, bila kujali ni mbunge wa kuteuliwa au wa jimbo.

Ndugai alisema kwa msingi huo, wabunge hao wateule wataapishwa wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge la Bajeti unaotarajiwa kuanza mjini Dodoma, Juni 12.

Alipoulizwa itakuwaje ikitokea wateule hao wa Rais wakateuliwa pia kuwa mawaziri na kuendelea na kazi kabla ya kuapishwa kuwa wabunge, Naibu Spika alisema kwa hali ya kawaida, hilo haliwezekani.

“Kwa mujibu wa Katiba, mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na anakuwa mbunge mteule hadi pale anapoapishwa, na ndiyo maana baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, kazi ya kwanza ya Bunge ni kuchagua Spika na Naibu Spika, ambao baadaye watafanya kazi ya kuwaapisha wabunge, na ndipo atateuliwa Waziri Mkuu na kisha mawaziri,” alifafanua Naibu Spika.

No comments: