Baadhi ya wanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Mengwa wakiwa nje ya darasa lao. Darasa hili kama lilivyoandikwa juu ya mlango wake pia hutumiwa kwa kupokezana na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.
Hili ni darasa moja ambalo hutumiwa na wanafunzi wa darasa la tano na la sita kwa pamoja wa Shule ya Msingi Mengwa. Kulia walionyoosha mikono ni darasa la sita baada ya mpiga picha kuomba darasa la sita kunyoosha mikono ili niweze watambua.
Hapa walionyoosha mikono juu upande wa kushoto ni wanafunzi wa darasa la tano wa shule ya Msingi Mengwa baada ya kuomba kufanya hivyo ili uweze kuwatenganisha na wale wa darasa la sita.
Na Joachim Mushi, Thehabari-Kisarawe
WAKATI Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini ikijipanga kuanza kufundisha kwa kutumia teknolojia ya kompyuta katika shule mbalimbali, wanafunzi wa darasa la tano na sita wa Shule ya Msingi Mengwa bado wanatumia darasa moja kwa wakati mmoja.
Hali hiyo imejulikana juzi baada ya mwandishi wa habari hizi kutembelea shule hiyo, iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mengwa, Peter Gadie alisema kitendo cha wanafunzi hao kutumia darasa moja kimefanya wapunguziwe muda wa vipindi wa kawaida ili kupishana kwa zamu kutumia darasa hilo.
Alisema badala ya kila kipindi kufundishwa kwa dakika harobaini walimu wameamua kufundisha kwa dakika ishirini kila kipindi ili kupeana zamu kuwafundisha wanafunzi hao.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia darasa hilo likiwa na wanafunzi wote yaani wa darasa la tano ambao wapo 24, na darasa la sita wakiwa 29 wakiendelea na masomo kwa pamoja huku wakitenganishwa kwa mistari ya madawati.
Akizungumzia staili ya ufundishaji wa walimu kwa kutumia darasa moja, Gadie alisema mwalimu wa darasa la tano anapoingia darasani huendelea na kipindi kwa dakika 20 huku akiwataka wanafunzi wa darasa la sita kujiinamia na kujisomea ama kuendelea na kazi walizoachiwa na mwalimu aliyetoka punde.
“Anapoingia mwalimu kufundisha darasa moja uwaamuru wanafunzi wa darasa lingine wajisomee ama kuendelea kufanya kazi ambazo wameachiwa na mwalimu aliyetoka…kweli wanapata usumbufu lakini haina namna maana tunaupungufu wa madarasa shuleni kwetu,” alisema Gadie akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Aidha alisema tatizo hilo halipo kwa wanafunzi wa darasa la sita na la tano pekee, kwani wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili nao usomea darasa moja kwa kupokezana saa; ambapo darasa la kwanza huingia saa mbili hadi saa sita na baadaye kuwapisha darasa la pili ambao huingia saa sita na kuendelea hadi mchana.
Alisema upungufu wa vyumba vya madarasa umeifanya shule hiyo kukodisha ukumbi wa kuoneshea video kijijini Mengwa na kulifanya darasa la awali kwa wanafunzi wa shule hiyo wanaosoma darasa la awali kabla ya kujiunga na darasa la kwanza.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
No comments:
Post a Comment