Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Kisarawe
WANAFUNZI 159 wa Shule ya Sekondari Maneromango wametoroka kufanya mitihani ya majaribio ya robo muhula iliyoanza juzi katika shule hiyo.
Wanafunzi hao ambao ni vidato mbalimbali kuanzia cha kwanza hadi cha nne, ni kati ya wanafunzi 383 wa Shule ya Sekondari Maneromango waliotakiwa kuanzia kufanya mitihani yao Machi 27, 2012 shuleni hapo.
Akizungumza katika mahojiano na mtandao wa Thehabari.com katika shule hiyo iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Jonas Buheruko alisema ofisi yake imebaini utoro huo baada ya kukusanya taarifa kutoka vidato vyote.
Akifafanua alisema hali hiyo ya utoro na hasa wanafunzi kukimbia mitihani hujitokeza mara kwa mara jambo ambalo limekuwa miongoni mwa vikwazo vya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma.
Alisema taarifa zilizokusanywa siku ya kwanza kuanza kwa mitihani hiyo, Machi 27 mwaka huu, zimebaini kidato cha nne ndiyo wanaoongoza kwa utoro wa mitihani kwani kati ya wanafunzi 106 waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo ya majaribio ni 45 pekee walifanya huku 65 wakiingia mitini.
“Taarifa zangu nilizokusanya baada ya kuanza tu kwa mitihani zinaonesha kidato cha kwanza wametoroka wanafunzi 10 kati ya 81, kidato cha pili wametoroka 31 kati ya 103, kidato cha tatu wametoroka 53 kati ya 93 waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo,” alisema Mwalimu Buheruko.
Hata hivyo alisema kitendo cha utoro wa mithani shuleni hapo sasa kinaendelea kuwa sugu licha ya walimu kufanya jitihada za kuwafuatilia wanafunzi na kutoa adhabu mbalimbali kulingana na taratibu za shule.
Aidha aliongeza mwaka 2011 wanafunzi 34 wa kidato cha nne kati ya 85 walikimbia kufanya mtihani wa majaribio wa Wilaya shule hapo jambo ambalo linawakatisha tamaa walimu katika utoaji wa elimu shuleni hapo.
“Wamekuwa wakikimbia mitihani mara nyingi…tunawapa adhabu lakini wapo radhi kufuraia adhabu unayowapa kuliko kuja kufanya mitihani…wakati mwingine tunapozidiwa tumekuwa tukipeleka majina ya watoro kwa Mwenyekiti wa Kijiji na Ofisa Mtendaji wa Kata lakini bado hatujaweza kudhibiti utoro huu,” aliongeza mwalimu Buheruko.
Akizungumzia hali hiyo, Mratibu wa Elimu Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma amesema wamekuwa wakiwaita mara kadhaa wazazi wa wanafunzi na kuwashtaki pale inapobainika wanachangia utoro wa watoto wao, ila tatizo hilo si kwa sekondari pekee bali hata shule za msingi eneo hilo.
Habari hii imeandaliwa na Thehabari.com kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
No comments:
Post a Comment