BAADA ya kulala usingizi wa “pono” kwa muda mrefu na kushindwa kudhibiti biashara sugu ya magendo katika mipaka yake ya Namanga, mkoani Arusha na Holili mkoani Kilimanjaro, Serikali sasa imebuni mkakati mpya wenye “sura ya kibinadamu” utakaofanya biashara hiyo ya magendo kuwa historia.
Biashara ya magendo inayohusu bidhaa za aina mbalimbali imekuwa sehemu ya mapambano ya usiku na mchana, baina ya vyombo vya dola vilivyoko katika mipaka hiyo na wafanyabiashara wasio waadilifu kwa muda mrefu, licha ya Tanzania na Kenya kutia saini mkataba wa itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Biashara hiyo pia inadaiwa kuwa chanzo cha kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika mipaka hiyo kutokana na tabia ya maofisa wa Serikali kuchukua fedha za rushwa kutoka kwa wafanyabiashara pindi wanapowakamata na bidhaa zinazovushwa kwa magendo.
Ingawa hakuna takwimu rasmi za makadirio ya biashara hiyo ya magendo, lakini inaaminika kuwa kuwa serikali za nchi zote mbili zinapoteza mabilioni ya fedha kila mwaka. Mabilioni hayo ya fedha yamekuwa yakipotea kutokana na serikali hizo kukosa fursa ya kutoza kodi mbalimbali, iwapo biashara hizo zingekuwa rasmi.
Kwa upande wa Tanzania, wafanyabiashara wake wamekuwa wakidaiwa kupeleka kwa magendo nchini Kenya, mazao ya chakula kama mahindi, mchele, viazi, matunda na mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Wakati upande wa Kenya, kwa kiwango kidogo wamekuwa wakiingiza nchini kwa magendo bidhaa za viwandani kama mafuta ya kupikia, sabuni, vifaa vya umeme na bidhaa nyingine za matumizi ya nyumbani.
Pamoja na kukosa mapato yatokanayo na kodi kwa serikali za pande zote mbili, biashara hiyo ya magendo inaelezwa kuwa imewatia hasara baadhi ya wafanyabiashara kutokana na kudhulumiwa fedha na bidhaa zao, na wenzao wasio waaminifu hivyo kukosa nafasi ya kulalamika katika vyombo vya dola.
Kwa upande wa Tanzania, mifano ya wafanyabiashara waliodhulumiwa kwa kupeleka bidhaa zao nchini Kenya kwa njia za magendo ni mingi, lakini waathirika wakubwa wanatajwa kuwa ni wafanyabiashara wa mifugo.
Moja ya mifano hiyo ni pale wanapofikisha mifugo yao upande wa Kenya ambapo madalali wanaotaka kununua mifugo hiyo hutoa taarifa kwa vyombo vya dola hasa polisi kuwa mifugo imeingizwa kutoka Tanzania na haina chanjo na polisi huwakamata wafanyabiashara hao na kwa kuwa mifugo hiyo haikuwa na vibali halali, basi wafanyabiashara hao hulazimika kuitelekeza kwa kuogopa kufunguliwa mashitaka na mamlaka za nchi hiyo.
Kutokana na mazingira ya aina hiyo, Watanzania wengi wanaelezwa kuwa wamepoteza mali zao kwa njia hiyo na wafanyabiashara wengi wameingia hasara kwa kupoteza mitaji yao.
Kutokana na matatizo hayo yanayojitokeza kila mara katika maeneo hayo, Serikali sasa imefanya mabadiliko makubwa kwa kutengeneza mazingira yatakayowezesha wananchi kufanya biashara halali bila bugudha.
Ziara ya Waziri Samuel Sitta
Wafanyabiashara wengi sasa wanamshukuru Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye wizara yake imebuni mkakati utakaowawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara zao kwa uhuru zaidi, baada ya Serikali kutangaza mkakati wa kufungua minada ya mifugo na masoko ya kuuza nafakakatika mipaka hiyo.
Waziri Sitta wiki iliyopita alitembelea mipaka hiyo hiyo inayovuma kibiashara ya Namanga na Holili. Pamoja na mambo mengine, akiwa akiwa katika ziara hiyo, alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa maeneo husika.
Katika mpaka wa Namanga, Waziri Sitta alifanya kikao cha pamoja na watendaji wa idara zote muhimu za serikali katika mpaka huo na pia alifanya kikao cha pamoja na Waziri wa Wizara ya Afrika Mashariki wa Kenya, Musa Sirma.
Baada ya vikao hivyo, Waziri Sitta aliwatangazia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Namanga kuwa, katika kipindi kifupi kijacho Serikali ya Tanzania itajenga mnada wa mifugo katika eneo hilo la mpakani ili kuwapa fursa wafanyabiashara wa Tanzania kuuza mifugo yao kwa uhuru zaidi.
Alisema mnada huo utawasadia wananchi wa upande wa Tanzania kuuza mifugo yao kama ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa wafanyabiashara kutoka Kenya ambao watafuata taratibu za kawaida, tofauti na ilivyo sasa, mifugo mingi huuzwa kwa magendo nchini Kenya na hivyo Serikali ya Tanzania kukosa mapato.
“Lengo la serikali ni kuona kuwa wananchi mnafanya biashara kwa urahisi zaidi na katika mazingira salama ya mali na bidhaa zenu, huku Serikali ikipata kodi kutokana na tozo zitakazowekwa kisheria,” alisema Sitta huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza.
Alisema pamoja na mnada wa mifugo serikali pia itafungua soko kubwa la mazao kama mahindi, mchele, maharage na aina nyingine za nafaka ili kutoa fursa kwa wakulima na wafanyabishara wa Tanzania kuuza mazao yao kwa uhuru badala ya kutumia njia za panya kuuza mazao hayo Kenya.
“Ni wazi kuwa kama mazingira ya kibiashara ni mazuri, si rahisi kwa wafanyabiashara kutumia njia za panya kutorosha mahindi au bidhaa nyingine nje ya nchi hivyo Serikali inaamini kuwa mipango hiyo itasadia sana kupunguza au kutokomeza biashara haramu ya magendo,” alisema Sitta.
Alisema kuwa wamekubaliana na wenzao wa upande wa Kenya kuwa kuanzia sasa, watafanya vikao vya pamoja vya ujirani mwema kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kwa lengo la kutatua matatizo madogo yanayowakabili wananchi wa mipakani.
“Tumekubaliana pia kuanzia sasa serikali itaandaa utaratibu utakaowezesha vibali na hati za dharura za kusafiria kupatikana katika eneo la mpakani badala ya wananchi kuzifuata Arusha mjini na wakati mwingine hadi jijini Dar es Salaam, hali ambayo imekuwa ikiwapa usumbufu kubwa,” alisema.
Waziri Sitaa pia aliwataka Watanzania kuanza kubadilika sasa kama walivyo wenzao katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kwenda na wakati kibiashara, kujituma katika kutafuta masoko ya bidhaa zao, badala ya kuwauzia wenzao wa nchi jirani.
“Wenzetu Wakenya wananunua mahindi Tanzania, wanayasaga na kuuza unga Sudan ya Kusini na wananunua ngo’mbe, mbuzi na kondoo upande huu na wanauza nyama nje ya Kenya na kutengeneza faida kubwa ya fedha lakini sisi tunabaki kulalamika tu, lazima tukubali kubadilika ili tuwe washindani katika soko hili la Afrika Mashariki,” alisema.
Ziara katika mpaka wa Holili
Katika mpaka huo uliopo mkoani Kilimanjaro, Waziri Sitta baada ya kuzungumza na watendaji wa idara mbalimbali za Serikali aliuagiza uongozi wa mkoa huo kusitisha mara moja utozaji kodi wa dola 200 za Marekani, kwa magari kutoka Kenya yanayoingia Tanzania kununua mahindi na nafaka nyingine.
Alisema kodi inatozwa kinyume cha makubaliano yaliyomo katika mkataba wa itifaki ya umoja wa forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na itifaki ya pamoja ya soko la Afrika Mashariki ambayo mkataba wake ulitiwa saini na viongozi wakuu wa nchi hizo.
“Kodi hiyo ni haramu na haikubaliki hivyo, naagiza uongozi wa mkoa kusitisha utozaji wake mara moja na wizara yangu itawaandikia barua rasmi kuhusu jambo hilo kuanzia wiki ijayo,” alisema.
Waziri huyo alitahadharisha watendaji hao kuwa makini na masuala ya aina hiyo ambayo alieleza kuwa yanaweza kuathiri hata uhusiano wa kidiplomasia, baina nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani yanakwenda kinyume cha malengo ya kuanzishwa kwake.
Hali ya kibiashara baina ya Tanzania na Kenya kwa sasa ni nzuri kuliko wakati mwingine wowote na takwimu zinaonyesha kuwa, Tanzania inaongoza kufanya biashara na Kenya, kiasi cha kuizidi Uingereza ambayo awali, ndiyo ilikuwa mshirika mubwa wa Kenya kibiashara.
No comments:
Post a Comment