WANANCHI katika Kijiji cha Singa wilayani Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, wamevunja Bodi ya Watumiaji Maji wa mradi wa kijiji hicho kwa madai kuwa haikuwepo kwa mujibu wa sheria na sera ya maji.
Wanakijiji hao walichukua uamuzi huo wa kuvunja Bodi hiyo kwa madai haikuwa na wajumbe halali kutoka katika kila kitongoji waliochaguliwa na wananchi wenyewe kwa mujibu wa sheria na Sera ya Taifa ya Maji.
Diwani wa Kata ya Kibosho, Thobias Ndakidemi alitoa ufafanuzi huo baada ya kutolewa kwa madai kuwa Bodi hiyo ilichaguliwa kisheria, na kuvunjwa kwake kumesababisha kusitishwa misaada ya mradi wa maji wa kijiji hicho na shirika lisilo la kiserikali la Ako la Ujerumani.
Ndakidemi alisema baada ya kugundua dosari hiyo, wananchi waliamua kuanza upya mchakato wa kufanya mikutano kwenye vitongoji vinne vya kata hiyo na kuwachagua wajumbe halali chini ya usimamizi wa Mhandisi wa Maji wa Wilaya, John Lyimo.
Alisema vitongoji hivyo vya Singa Juu, Kifueni, Tobo na Singa kati vilifanya uchaguzi wa wajumbe wawili wa kuunda bodi mpya kwenye mkutano wa wananchi wa Februari 13 mwaka huu.
Diwani huyo alisema wajumbe wa Bodi ya kwanza hawakuchaguliwa na mikutano ya wananchi ya vitongoji hivyo akiwemo Mwenyekiti wake, Gerald Ngotolainyo wa kitongoji cha Kifueni ambaye alichaguliwa kwenye mkutano wa kijiji.
Meneja wa mradi huo, Sindbadi Mlaki alisema Ako imesitisha misaada yake kutokana na uharibifu wa miundombinu ya mradi huo wa maji na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 1.6.
No comments:
Post a Comment