Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya madaktari kutishia kuanza mgomo mwingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema amesikitishwa na tishio hilo akisema kwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa utekelezaji wa makubaliano mbalimbali na wanataaluma hao.
Pinda alitoa kauli hiyo jana aliokuwa akizungumzana katika mahojiano maalumu na Gazeti dada la Mwananchi, The Citizen na kusema hatua hiyo mpya ya madaktari inamsikitisha kwa kuwa Serikali ndiyo kwanza inaendelea na vikao kwa ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza madai yao hayo.
“Siwezi kuzungumza chochote sasa wakati Serikali inaendelea kushughulikia mgogoro huo. Niseme tu kwa kweli wananisikitisha (madaktari). Ninasikitika kuona kwamba wakati bado tuko kwenye mazungumzo, wenzetu wanafanya vikao vingine,” alisema Pinda.
Akilihutubia taifa Februari 29 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alieleza kufurahishwa na hatua ambayo suala hilo limefikia akisema:“Nashukuru mgomo huo umekwisha lakini makovu yake yatabaki maisha katika kumbukumbu za historia ya taaluma ya tiba hapa nchini.”
“Leo (Februari 29), Mheshimiwa Waziri Mkuu amenipa taarifa kuwa kamati aliyounda kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa yake kwake. Kuanzia kesho (Machi, Mosi), Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo. Ninawaomba ndugu zetu madaktari kuwa na moyo wa subira.”
Rais Kikwete alisema Serikali inatambua, inajali na kuthamini kazi za madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya katika kulinda na kudumisha afya za Watanzania hivyo itajitahidi kuona kuwa inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa mgomo haujirudii tena.
Hata hivyo, wakati Pinda akieleza kusikitishwa na hatua hiyo mpya ya madaktari, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya alisema hawezi kujiuzulu kama madaktari hao wanavyotaka kwa kuwa suala hilo liko nje ya uwezo wake.“Hivi sasa siwezi kuzungumza chochote kwa kuwa suala hilo liko juu yangu na siwezi kujiuzulu,” alisema Dk Nkya.
Tishio la madaktari
Juzi, madaktari hao waliipa Serikali siku tatu kuanzia jana hadi Jumatano wiki hii kuhakikisha inawatimua kazi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu wake, Dk Nkya vinginevyo watatangaza mgomo mwingine waliouita wa kihistoria.
Pia, madaktari hao kupitia kwa wawakilishi wao waliopo katika kamati iliyoundwa na Pinda kujadili madai yao, wamekubaliana kutoendelea na majadiliano hadi hapo mawaziri hao watakapoondolewa kwenye nyadhifa zao.
Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kikao kilichoitishwa na Serikali kujadili suala hilo kuvunjika huku kila upande ukituhumu mwingine kuhusika.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari hao ulifanyika Dar es Salaam juzi, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisema kama mawaziri hao wataendelea na nyadhifa zao hadi Jumatano, madaktari hawatakuwa tayari kuendelea na kazi.
“Madaktari wameona isingekuwa jambo jema kuendelea kujadiliana na kufikia uamuzi na Serikali huku Waziri na Naibu wake wakiendelea kushikilia nyadhifa zao, watu hao wanawajibika kwa kila kilichotokea? Nani asiyejua kuwa vifo vilitokea wakati wa mgomo?” alisema Dk Mkopi na kuongeza:
..Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment