Friday, March 23, 2012

DC awaonya wanaharakati wanaopinga michango

MKUU wa Wilaya Tarime mkoani Mara, John Henjewele ameonya kikundi cha watu wanaojiita Wanaharakati katika mji mdogo wa Sirari Tarafa ya Inchugu, kinachoendesha siasa kupinga michango ya wananchi katika shughuli za maendeleo.

Kikundi hicho kinadaiwa kukwamisha juhudi za wananchi wanaotaka kuchangia maendeleo katika ujenzi wa shule za msingi za Keryoba, Sirari, Nyairoma na Shule ya Sekondari Sirari.

Pia ameonya kuwa atawachukulia hatua kali watendaji na wenyeviti watakaobainika kujihusisha na uvujaji wa fedha za michango ya wananchi.

Alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara ulifanyika katika Tarafa ya Inchugu na kuhudhuriwa na wenyeviti wa vitongoji na madiwani.

Awali Henjewele alikutana na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kupinga mchango wa Sh 10,000 kwa kila chumba badala ya kaya, ambapo mengine yalidai wananchi wanapendekeza mchango wa hiari kwa maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Sirari uwe Sh 5,000.

Mabango mengine yalidai kuna uongozi wa kimila na vitisho kutoka uongozi wa vitongoji na kata wakati kuna hujuma ya fedha zao za michango ya mara kwa mara na isiyo na kiwango malumu.
Pia walidai kuwa licha ya wengine kuchanga Sh 30,000 na wengine Sh 10,000 walidai kuwepo stakabadhi bandia katika michango hiyo hali ambayo inatia shaka kama michango hiyo inakwenda katika ujenzi wa shule hiyo.

Henjewele baada ya kusoma na kuwasikiliza alisema amepokea malalamiko hayo na atayafanyia kazi lakini akawaomba waache siasa katika maendeleo ya jamii.

No comments: