POLISI imevionya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki, viepuke vurugu, huku CCM nayo ikitishia kuwaagiza vijana wake kuingia msituni kama vitendo vya vurugu dhidi ya chama hicho vitaendelea.
Tamko la Polisi na la CCM yalitolewa siku moja baada ya msafara wa mgombea ubunge wa CCM, Sioi Sumari, kushambuliwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Chadema katika kitongoji cha Maji ya Chai juzi usiku, wakati ukirejea kutoka kwenye mkutano wa kampeni.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martin Shigela, akizungumzia tukio hilo mjini hapa jana, alisema CCM imechoka kuvumilia vitendo vya vurugu na fujo vinavyofanywa na wanachama wa Chadema.
“Tukio la jana (juzi) ni la pili. Awali wafuasi wa Chadema walitufanyia fujo kwenye mkutano wa uzinduzi (Machi 12) walipofika kwenye mkutano wetu wa kampeni na kuweka bendera na picha za mgombea wao, lakini pia walileta magari yao pale.
“Jana (juzi) pia walishambulia msafara wetu wakati mgombea wetu anarejea kutoka katika mkutano wa kampeni. Tunaliomba Jeshi la Polisi kukomesha matukio haya mara moja.
“Bado tuna imani na Polisi, tunaomba tukio hilo liwe la mwisho, vinginevyo nasi tutashindwa kuvumilia na tutawaambia vijana wetu waingie msituni,” alisema Shigela.
Alisema CCM imeisamehe Chadema kutokana na tukio hilo la juzi na inawaomba wananchi wa Arumeru Mashariki kuwasamehe wafuasi wa chama hicho, kutokana na tukio hilo, lakini akasema viongozi wa chama hicho wanapaswa kuonya wafuasi wao.
“Sisi tangu tumeanza kampeni tumejitahidi kufanya kampeni za amani, staha na kuheshimiana. Hatujawahi kuingilia mikutano ya Chadema, hatujarusha mawe kwenye msafara wao wala hatujatoa lugha ya matusi. Tunawaomba na wao waheshimu suala hili,” alisema.
Gari la waandishi wa habari, lilishambuliwa juzi katika kitongoji cha Maji ya Chai wakati msafara wa mgombea wa CCM, Sioi, ulipokuwa unarejea kutoka kwenye mkutano wa kampeni katika kata ya Ngarenanyuki saa 1.30 usiku.
Wakati CCM wakionya, Polisi jana ilitoa onyo kwa vyama vya siasa kuepuka fujo na vurugu zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu na kutia kasoro mwenendo wa uchaguzi huo.
Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu, ambaye ndiye Mkuu wa Operesheni za Uchaguzi kwa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Arumeru Mashariki, alisema tayari Jeshi hilo limepokea mashitaka matano ya vurugu na fujo katika mikutano ya kampeni.
Matukio hayo kwa mujibu wa Mngulu, yanahusu uchanaji wa bendera za vyama vya siasa, picha za wagombea, wizi wa bendera na picha za wagombea, na lugha za matusi zinazodhalilisha wagombea na viongozi wa vyama hivyo.
“Wanaacha kunadi sera wanaingilia mambo ya ajabu, mara huyu ukoo wao hivi mara huyu si raia. Haya mambo hayana manufaa kwa wananchi ambao lengo lao ni kutaka kusikia sera zitakazowaletea maendeleo,” alisema Mngulu.
Alisema tayari mashitaka hayo yamewasilishwa kwa Kamati ya Maadili iliyo chini ya Msimamizi wa Uchaguzi, ili kuyafanyia kazi na jana wajumbe wa Kamati hiyo inayojumuisha wawakilishi wa vyama vya siasa, ilitarajiwa kukutana ili kukumbushana kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema Polisi itaendelea kushirikiana na vyama vya siasa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika hali ya amani na utulivu.
Tamko la wanahabari Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), kimetoa tamko la kuvitaka vyama vya siasa kujiepusha na vurugu zinazoweza kuleta athari kwa wadau kama ilivyotokea kwa tukio la gari lao kurushiwa mawe juzi usiku.
Katibu Mkuu wa APC, Eliya Mboneya, ambaye aliathirika katika tukio la juzi kwa kuangukiwa na kioo cha gari kilichovunjwa na watu hao wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Chadema, alisema vitendo hivyo vikiachwa vikaendelea, vitaleta athari na kutia doa kampeni.
“Gari tulilopanda waandishi wa habari halikuwa na alama yoyote ya chama hivyo hawakupaswa kutushambulia kwa mawe kwa vile hawakujua ni akina nani wamebebwa ndani ya gari hilo,” alisema Mboneya.
Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, umelaani vikali tabia iliyojitokeza ya vijana kukashifu viongozi wastaafu. Taarifa ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya, kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kusikitishwa na kilichoitwa matusi yaliyotolewa na kiongozi wa upinzani dhidi ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Sisi kama wazazi, jukumu letu ni kulea vijana ili wawe na adabu na tabia njema kwa lengo la kujenga Taifa lenye maadili na kuheshimiana. Hivyo vijana wanapovunja maadili ni wajibu wetu kuwakemea, bila maadili mema Taifa litaangamia,” alisema Ngawaiya katika taarifa hiyo. Hivi karibuni kulizuka malumbano baina ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na Mbunge wa Musoma Mjini ambaye pia ni Meneja wa Kampeni za Chadema, jimboni Arumeru Mashariki, Vincent Nyerere.
Wakati Mkapa akikana kumtambua Vincent kama mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mbunge huyo kwa upande wake, alimshambulia Mkapa akimtaka asiingilie ukoo wa Nyerere huku akidai kuwa ndiye aliyechangia kifo cha Mwalimu. Hali hiyo ilisababisha mjane wa Mwalimu, Mama Maria, kukemea kitendo cha Vincent kumshambulia Mkapa na kusema sababu za kifo cha mumewe anazijua yeye na kukanusha Mkapa kuhusika, huku akitaka aheshimiwe kama kiongozi mstaafu.
No comments:
Post a Comment