KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zinachangia kuchelewa kwa kesi dhidi ya watumishi wa halmashauri, majiji na manispaa wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu.
Kamati hiyo imedai kuwa taasisi hizo nyeti za Serikali zimekuwa zikikalia majalada ya kesi dhidi ya watuhumiwa wa nafasi mbalimbali za uongozi ambao wamesimamishwa na wengine kufukuzwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustino Mrema aliyasema hayo jana katika kikao cha pamoja na viongozi wa halmashauri za Monduli, Arusha na Jiji la Arusha ikiwa ni baada ya kukaguliwa kwa hesabu zao kwa mwaka 2008/2009.
“Wapo wakurugenzi, waweka hazina na wakuu wa idara mbalimbali wamesimamishwa kwa tuhuma tofauti kwa zaidi ya miaka miwili sasa lakini DPP haelezi kama wanatakiwa kufikishwa mahakamani…Takukuru nao wanachunguza muda mrefu sana,” alisema.
Mrema alisema ili kuisaidia Serikali kusimamia halmashauri kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, wahisani na wananchi kwa ujumla ipo haja kwa taasisi hizo kutekeleza wajibu wake kwa wakati ili kuwatendea haki wanaotuhumiwa.
Mwenyekiti huyo alitolea mfano halmashauri za Wilaya ya Monduli ambayo kuna nafasi 12 za wakuu wa idara muhimu ambazo zinaendeshwa na makamu huku pia Halmashauri ya Jiji nayo ikiwa na nafasi sita zinazokaimiwa.
Kamati hiyo iliiomba Serikali kuhakikisha taasisi zake hizo zinakuwa mstari wa mbele katika kusukuma halmashauri kutekeleza wajibu wake jambo ambalo litachochea maendeleo ya haraka katika sekta mbalimbali.
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo, akiwemo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, walisema upo uzembe wa wakuu wa idara katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Walisema baadhi ya miradi katika wilaya za Monduli, Arusha na Jiji la Arusha umetekelezwa kwa ubabaishaji huku wakuu wa idara wakionesha uzembe katika ufuatiliaji wake licha ya kutumia mamilioni ya fedha za serikali.
No comments:
Post a Comment