Thursday, March 15, 2012

Madaktari Waliogoma Kushitakiwa Mahakamani

KAMATI ya wanaharakati 36 nchini inatarajia kuwaburuta mahakamani madaktari walioshiriki mgomo kwa wanachodai ni kulisababishia Taifa hasara na vifo vya watu wasio na hatia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwa niaba ya wanaharakati hao, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Godfrey Mosha, alisema mgomo wa madaktari ni kitendo kisicho cha kiungwana na kisichovumilika.

“Kamati yetu ipo katika hatua ya kuandaa vielelezo vya kwenda kushitaki katika Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ili kuwawajibisha walioshiriki na liwe fundisho kwa makundi mengine ambayo hayana nia njema na Taifa letu, lenye amani na utulivu kwa kipindi kirefu,” alisema Mosha.

Alifafanua, kwamba wanataka kudai haki iliyokiukwa na watu waliolewa nafasi walizopewa na Taifa, hivyo ni lazima haki hiyo ipiganiwe na wanaharakati wote na makundi yote ya Watanzania wenye nia njema na nchi yao.

Alidai Kamati hiyo inayoundwa na wanamazingira, wanasheria na madaktari wastaafu, imegundua kuwa mgomo huo ulisababisha vifo vya watu takribani 300; huku madaktari hao wakiendelea kusaini vitabu vya mahudhurio na kupokea mishahara bila kazi.

Akifafanua, Mosha alisema mbali na kuwa ni kinyume na utaratibu na sheria za nchi, madaktari hao pia walipoteza maadili ya kazi yao. “Kwa nini wao wajione ni kundi muhimu sana kuliko mengine nchini yakiwamo ya Jeshi, Polisi na ualimu?” Alihoji.

Alisema Kamati hiyo na Watanzania wengi walishitushwa na kitendo cha madaktari kupinga mazungumzo waliyofanya na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwa ni cha dharau kwa kiongozi wa nchi huku wao wakiwa watumishi wa umma na wasomi.

Alisema madaktari kudai nyongeza kubwa ya mishahara, hadi Sh milioni 17 kwa daktari bingwa na milioni 3.5 kwa daktari anayeanza kazi kwa mwezi, ilitakiwa kuzingatia uwezo wa Serikali ya nchi yao.

Mosha alisema Kamati pia inampongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa kufikia mwafaka na madaktari hata kurudi kazini na kuendelea na kazi ya kuhudumia Watanzania. Alisema watumishi wa Serikali katika taasisi mbalimbali wanatakiwa kuwa wazalendo kwa Taifa lao, ili nchi iendelee na amani na maendeleo.

Aliwaomba Watanzania wa makundi yote ya kijamii, wakiwamo maaskofu na mashehe, kutoa maoni yao kupitia barua pepe ya madaktarimashtaka@gmail.com au ewaldsuvey@yahoo.com au simu namba 0773-772213 ili kukamilisha azma yao ya kwenda mahakamani.

Chimbuko la mgomo Mwishoni mwa mwaka jana, wataalamu mbalimbali wa afya madaktari walio mafunzoni - ‘interns’, wakijumuisha madaktari, madaktari wa meno, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara na kadhalika, wanaofanya kazi chini ya uangalizi wa madaktari bingwa na wataalamu wengine wa afya, waligoma.

Mgomo huo ulitokana na ‘interns’ hao kucheleweshewa posho zao kwa kipindi cha kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana. Mbali na kucheleweshewa malipo hayo, wataalamu hao walijumuisha madai mengine kama vile, nyongeza ya posho za kuitwa kazini kwa asilimia 10.

Walidai pia nyongeza kwa asilimia 30 ya posho ya mazingira hatarishi na kupewa chanjo ya kuzuia magonjwa yanayozuilika; walitaka nyumba au posho za nyumba kwa asilimia 30 na pia posho ya mazingira magumu wakitaka ilipwe kwa asilimia 40 ya mishahara yao.

Madaktari hao pia walitaka walipwe posho ya asilimia 10 ya mshahara kwa ajili ya usafiri au wakopeshwe magari na kupewa kadi za kijani za Bima ya Afya.

Lakini kingine walitaka watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wachukuliwe hatua huku wakimpa Rais saa 72 kufanya hivyo. Serikali iliyapokea madai hayo na mengine kuyafanyia kazi papo hapo, ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.

Lakini madaktari waliishiwa na subira na kutoa madai mengine ya kutaka kufukuzwa kazi kwa Waziri, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya. Hata hivyo mwafaka ulipatikana walipokutana Ikulu, Dar es Salaam na Rais Kikwete, ambaye aliwaambia suala la kufukuzwa mawaziri si suluhisho la matatizo yao.

Hatimaye baada ya mazungumzo na Rais, ambaye aliwataka wamwamini na kumpa muda wa kushughulikia madai yao, walimwamini wakakubali kurejea kazini.

No comments: