Monday, March 19, 2012

CHADEMA yatikisa vigogo wa CCM

HALI ya wasiwasi imezidi kuenea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na pingamizi jipya dhidi ya mgombea wao katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, Siyoi Sumari, na sasa chama hicho tawala kimekuwa kikiendelea na kampeni zake kwa kusubiri huruma ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa mujibu wa taarifa zilizobainiwa na Raia Mwema, endapo pingamizi hilo lililowekwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) litaridhiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), CCM itaweza kutupwa nje ya kinyang'anyiro hicho cha ubunge kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Awali, gazeti hili lilipata taarifa kuwa CCM kilikuwa na mpango wa kumteua mgombea wake namba mbili katika duru la pili la kura za maoni katika chama hicho, William Sarakikya, kuwa mgombe ili kujiepusha na uwezekano wa Sumari kuwekewa pingamizi ambalo linaweza kukigharimu chama hicho kikongwe katika historia ya chaguzi ndogo nchini.

Katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni jitihada za kushughulikia kadhia hiyo inayoitia hofu CCM, tayari Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva, ameanza vikao na timu yake kuchambua rufaa ya CHADEMA, ambayo msingi wake ni kulalamikia kutupiliwa mbali kwa pingamizi lao waliloweka dhidi ya Sumari kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Tracius Kagenzi.

“Viongozi wameanza kuzungumzia na hata kutafakari namna ya kumudu changamoto inayoweza kujitokeza endapo pingamizi la CHADEMA litakubaliwa na kwa hiyo, Siyoi Sumari akaenguliwa kwenye mbio za ubunge zilizokwisha kuanza. Hata hivyo, licha ya kuanza kutafakari suala hilo, bado wanaamini tume itamwacha Sumari aendelee ingawa kwa kweli hawana uhakika na hilo. Kuna wasiwasi kati yao,” anaeleza mtoa habari wetu ndani ya CCM.

Rufaa ya CHADEMA

Mgombea wa CHADEMA jimboni Arumeru, Joshua Nassari ndiye aliyekata rufaa NEC, akipinga hatua ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Tracius Kagenzi, kutupilia mbali pingamizi aliloweka kuhusu utata wa uraia wa mshindani wake kutoka CCM.

Nasari na chama chake wanataka ufafanuzi wa kisheria kutoka Tume hiyo ya Uchaguzi, wakidai kuwa msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo kashindwa kufafanua sheria za masuala ya uhamiaji.

Mgombea huyo anadai kuwa, Kagenzi ameshindwa kutafsiri ipasavyo Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 1995 na pia Siyoi ameshindwa kutoa vielelezo vinavyothibitisha kuwa yeye ni raia wa Tanzania.

Katika uamuzi wake kuhusu pingamizi hilo, Kagenzi alisema msingi wa uamuzi wake wa kutupilia mbali pingamizi la Chadema dhidi ya Siyoi ni kwamba; vifungu namba 6 na 7 (1) vya Sheria ya Uhamiaji ya 1995 havipaswi kusomwa pamoja kwani vinaelezea mambo mawili tofauti ambayo “hayana uhusiano hata kidogo”.

Ni kutokana na hali hiyo Chadema walidai kuwa ama Kagenzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, ameshindwa au hajui kutafsiri sheria kama inavyotakiwa, wakidai ameonekana kwenda kinyume cha vifungu husika kama Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha ilivyofafanua suala la uraia wa Siyoi, katika barua yao waliyoituma kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Chadema wanaamini kuwa Idara ya Uhamiaji ndiyo yenye mamlaka na inayohusika katika kutafsiri Sheria za Uhamiaji kuliko anavyoweza kufanya Mkurugenzi wa Halmashauri na wanasheria wake, na wamekuwa wakijikita katika barua hiyo toka Uhamiaji ambayo inaripotiwa kuleta mtafaruku mkubwa ndani ya CCM na serikalini.

Barua ya Idara ya Uhamiaji

Katika barua ya Idara ya Uhamiaji ambayo imeandikwa na Ofisa Mfawidhi wa Mkoa wa Arusha, Daniel Namwomba, yenye kumbukumbu namba AR/C/32/VOL1/85 kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, unatolewa ufafanuzi kuwa Siyoi Sumari hakufuata taratibu za kisheria alipofikisha umri wa miaka 18, kuukana uraia wa nchi ya Kenya alikozaliwa.

Mgombea huyo kwa mujibu wa maelezo yake alizaliwa katika mji mdogo wa Thika, nchini Kenya mwaka 1979, wakati Baba yake mzazi Jeremiah Sumari akifaya kazi nchini humo.

Sehemu ya barua hiyo ya Ofisa Uhamiaji Mfawidhi Mkoa wa Arusha inasomeka: “Kwa mtizamo huo kama Bw. Sumari (Siyoi) alizaliwa kweli Kenya, alipotimiza umri wa miaka 18 alihitajika kututhibitishia kuwa kweli yeye si raia wa Kenya na kutupatia ushahidi wa uraia wa wazazi wake au kuukana uraia wa Kenya na kutuletea cheti (renunciation certificate) toka Kenya”.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu kuhusu rufaa hiyo, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Malaba, alikiri ofisi yake kuipokea na akaongeza ya kuwa itafanyiwa kazi ndani ya muda mfupi ujao.

“Tutaifanyia maamuzi as soon as possible (haraka iwezekanavyo) ili kutoa fursa ya wagombea wote kuongeza umakini na kampeni zao za uchaguzi na ni matarajio yetu uchaguzi utakuwa wa amani,” alisema Malaba.

CCM ‘watafutana’ miongoni mwao

Habari zilizofikia Raia Mwema kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa pamoja na suala la uraia wa mgombea huyo kuleta mtafaruku, viongozi wa juu wa chama hicho wamekuwa katika harakati za kumtafuta “mchawi” aliyefikisha barua ya Uhamiaji kwa CHADEMA.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa makundi ndani ya chama hicho katika Mkoa wa Arusha yamekuwa yakishutumiana kuhusika katika ‘kuvujisha’ barua hiyo kwa CHADEMA.

Ingawa hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuwa suala hilo litafanyiwa uchunguzi, zipo taarifa kuwa suala hilo huenda likajadiliwa ili kufahamu kiini cha ‘kuvuja’ kwa barua hiyo ya siri.

“Hatulali usiku na mchana tunapambana kuhakikisha kuwa rufaa hiyo inatupwa na NEC ili mgombea wetu aendelee na kampeni zake bila hofu, lakini suala hilo limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya CCM,” alieleza kada mmoja wa chama hicho aliyeko ndani ya timu ya kampeni zinazoendelea Arumeru Mashariki, ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Kada huyo aliimbia Raia Mwema kuwa suala hilo la utata wa uraia wa mgombea pamoja na vita baina ya makundi CCM vinatishia mshikamano ndani timu ya kampeni na uongozi wa chama hicho kikongwe nchini kwa ujumla wake.

Kampeni za CHADEMA

Katika uzinduzi wao wa kampeni Chadema walionyesha hofu ambayo msingi wake ni kuwapo kwa idadi kubwa ya askari polisi jimboni humo katika kipindi hiki cha kuelekea Aprili Mosi, mwezi ujao, ambayo ni siku ya kupiga kura.

Hofu hiyo ya CHADEMA inazingatia uzoefu wao ambao unahusisha uhusiano usioridhisha kati ya chama hicho na Jeshi la Polisi nchini, na hususan, ndani ya Mkoa wa Arusha, ambako CHADEMAa kimewahi kuingia katika mvutano na Jeshi la Polisi kwa madai ya kufanya maandamano bila kuomba kibali.

Katika tukio hilo, CHADEMA walifanya maandamano wakipuuza agizo la Jeshi la Polisi kutofanya maandamano hayo na Polisi hatimaye walitumia nguvu kuzima maandamano hayo. Katika vuta nikuvute hiyo, watu kadhaa waliuawa, sambamba na uharibifu wa mali, mambo ambayo hayakupata kushuhudiwa mkoani Arusha.

Arusha ni kati ya miji iliyokuwa na historia nzuri ya utulivu ikitawaliwa na pilika pilika za kibiashara, zikiwamo shughuli za utalii. Hali ilianza kuchukua sura mpya mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambapo Godbless Lema, alishinda ubunge kwa tiketi ya CHADEMA.

“Wingi wa polisi hawa ni kilelezo cha kutosha kuwa CCM na serikali yake wameanza vitisho dhidi ya wananchi wa Arumeru ili wapate hofu na kushiriki harakati za kampeni kwa wasiwasi. Lakini sisi tutafanya kampeni za kistaarabu na tutashinda kwani mungu yuko upande wetu,” anasema Freeman Mbowe Mwenyekiti wa CHADEMA-Taifa.

Kauli hiyo ya Mbowe kuahidi kampeni za kistaarabu huku wakionyesha hofu kuhusu wingi wa askari polisi, iliungwa mkono na Meneja wa kampeni wa CHADEMA Arumeru Mashariki, Vicent Nyerere.

Kwa upande wake mgombea, Joshua Nassari, aliewaeleza wananchi kuwa iwapo watamchagua kero ya kwanza atakayoitatua ni migogoro ya ardhi ambayo kwa mujibu wa maelezo yake, inaelekea kutishia amani jimboni humo.

“Ndugu zangu karibu kila kijiji na mtaa katika jimbo letu wananchi wake wanakabiliwa na mgogoro wa ardhi hivyo kazi ya kwanza kama mbunge itakuwa ni kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inatafutiwa ufumbuzi,” alisema.

“Pia kuna tatizo la maji katika maeneo mengi ya jimbo letu licha kuwa na mito na chemichemi nyingi zinazotiririsha maji kutoka katika miinuko ya Mlima Meru na badala yake maji hayo yanatumiwa na wananchi wa Jimbo jirani la Monduli huku nyie wa Arumeru mkiishi bila ya maji. Hali hii lazima ikomeshwe kwa kuweka mradi wa maji ambao utaondoa kero hii sugu,” alisema Nassari.

Kampeni za CCM

Kampeni za chama hicho tawala zilizinduliwa Jumatatu wiki hii na rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alianza hotuba yake kwa kukanusha taarifa kuwa alikuwa amegoma kuzindua kampeni hizo kutokana na mgawanyiko wa makundi ndani ya chama hicho huku akiwashambulia kwa maneno wapinzani wa chama chake.

Mkapa alisema; “Maneno yanayoenezwa na wapinzani kuwa nimegoma kuja kuzindua kampeni ya CCM ni ya kijinga, uzushi na yanaenezwa na watu waliokosa adabu. Mimi ni zao la CCM, na hilo linafahamika kwa viongozi wote na wanachama wa chama changu,” alisema Mkapa.

Mkapa pia alikanusha kumiliki mashamba katika jimbo la Arumeru Mashariki kama ilivyodaiwa na wanasiasa wa upinzani ambao walidai alikuwa akimiliki mashamba hayo kwa ubia na baadhi ya wawekezaji wa kigeni, wakiendesha kilimo cha maua na mazao ya mboga mboga.

“Sijawahi kudhulumu ardhi katika sehemu yoyote ya nchi hii. Huu ni uzushi unaoenezwa na wanasiasa wachovu, wasio na uwezo wa kufikiri hata kidogo,” alisema Mkapa, bila kugusia tuhuma dhidi yake kwamba alijibinafsishia na kujimilikisha kwa “bei poa” mgodi wa serikali wa makaa ya mawe, Kiwira (pamoja na ardhi yake) wakati akiwa rais. Hadi leo Mkapa ameshindwa kuzikana tuhuma hizo nzito dhidi yake, ambazo zimekuwa ni mojawapo ya madoa mazito zaidi ya ufisadi na wizi katika utawala wa CCM.

Kwa upande wake, mgombea Siyoi Sumari alieleza kuwa amejipanga kurithi kiti cha ubunge kilichoachwa wazi na baba yake mzazi.

“Nitajikita sana katika mambo makubwa mawili ambayo ni tatizo la maji na ajira kwa vijana wetu kwa kupigania kuenezwa kwa elimu ya ujasiriamali ili vijana wengi waweze kujiari wenyewe,” alisema.

Hata hivyo Siyoi alitia doa hotuba yake mwanzoni pale aliposema kuwa anawashukuru watu wa Mkoa wa “Arumeru” ilihali Arumeru si mkoa bali ni wilaya ndani ya Mkoa wa Arusha. Kauli yake hiyo ilizua manung’uniko kutoka wanachama na wapenzi wake baada ya mkutano kwisha.

“Mgombea wetu ameshindwa kutofautisha mkoa na wilaya, hii ni hatari sana katika uchaguzi wenye ushindani kama huu. Sina hakika kama alisema kwa bahati mbaya au hajui, lakini hapa timu ya kampeni inabidi iwe inampangia maneno ya kuzungumza jukwaani, vinginevyo tutavuna aibu kila mara,” alisema mmoja wa makada aliyekuwa amekaa jukwaa kuu.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

No comments: