MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Haruna Masebu,amehenyeshwa kwa kuhojiwa kwa undani na Baraza la Mawaziri kuhusu kuyumbisha bei ya mafuta.
Baraza hilo lilitaka kujua kwa nini mamlaka hiyo imekuwa ikiyumbisha nchi na wananchi kuhusu bei za mafuta.
Kwa zaidi ya saa moja, Masebu na wasaidizi wake waliwekwa kiti moto kuhusu bei zilizotangazwa na Ewura mwishoni mwa wiki, ambazo zimepanda kwa asilimia sita kutoka zile zilizotangazwa awali.
Habari za kuaminika kutoka kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, mjini Dodoma zinasema kuwa waziri mmoja baada ya mwingine walimhoji Masebu na wasaidizi wake kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za mafuta nchini.
Habari zinasema kuwa Masebu ambaye aliingia kwenye ukumbi huo akionesha kujiamini, alianza kupoteza mwelekeo kwa kadri maswali yalivyokuwa yakimiminika kutoka kwa mawaziri.
Hatimaye siyo yeye mwenyewe ama yoyote kati ya wasaidizi wake ambaye alikuwa na majibu ya kutosheleza ama hata ya kuwashawishi mawaziri kuhusu hatua hizo za Ewura na kwa kadri kikao hicho kilivyoendelea, Masebu na wenzake walionekana kukosa hoja.
Habari zinasema kuwa Masebu na wasaidizi wake walitakiwa kujielezea mbele ya Baraza la Mawaziri ili kuliwezesha Baraza hilo, chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, kujiridhisha na mwenendo mzima wa bei mafuta.
Baraza hilo lilitaka ufafanuzi kuhusu bei za petroli, mafuta ya taa na dizeli; nishati ambazo ukosefu wake nusura uiingize nchi katika zahama kubwa wiki iliyopita.
Moja ya maswali ya awali kutoka kwa Baraza la Mawaziri ilikuwa ni kwa nini Masebu na Ewura walitangaza kupanda tena kwa bei za mafuta siku chache baada ya kuzishusha kwa asilimia 9.17 kwa petroli, asilimia 8.31 kwa dizeli na asilimia 8.70 kwa bei ya mafuta ya taa.
Hatua hiyo ya Ewura kupunguza bei ya mafuta ilikuwa inatekeleza uamuzi na maagizo ya Serikali yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo Juni 22, mwaka huu, bungeni wakati alipowasilisha Bajeti ya Serikali.
Katika bajeti hiyo, Mkullo alisema kuwa Serikali iliamua kuondoa kodi na tozo kadhaa kwenye bei ya mafuta yanayoingizwa nchini kwa nia ya kupunguza bei ya bidhaa hizo ili kumpungumzia makali ya maisha mwananchi.
Hatua hiyo ya Mkullo, pamoja na ile ya Ewura kupunguza bei za mafuta ziliungwa mkono na Bunge na wananchi kwa kiwango kikubwa ambao walikiri kuwa hatua hiyo ilithibitisha jinsi gani Serikali yao inavyowajali.
Hatua ya Ewura kupunguza bei ya mafuta ilipingwa na kampuni karibu zote kubwa za kuingiza mafuta nchini ambazo zilianzisha mgomo kupinga hatua hiyo hasa BP, Engen, Oilcom na Camel Oil.
Baada ya siku moja ya mgomo huo, kampuni zingine nchini zilianza tena kuuza mafuta, lakini kampuni hizo nne zilikataa kufungua vituo vyao kuuza mafuta.
Agosti 9, mwaka huu, Ewura ilitoa amri ya Kimahakama (Compliance Order), kwa kampuni hizo nne kuanza mara moja kutoa huduma katika maghala yao na katika vituo vya rejareja vikiwemo vile vilivyoko chini ya miliki zao.
Katika amri hiyo, kampuni hizo zilitakiwa kuacha mara moja kusababisha upungufu wa makusudi wa mafuta ya petroli katika soko la Tanzania na kujieleza katika saa 24 kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka matakwa ya Sheria ya Mafuta na Utaratibu wa Ewura.
Siku iliyofuata, kampuni tatu zilianza kutoa huduma lakini BP (T) Ltd iliendelea kukaidi amri ya Ewura.
Bodi ya Ewura katika kikao chake cha Agosti 12, ilichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kali kwa kampuni za Oilcom, Camel Oil na Engen, na kuisitishia BP leseni ya biashara ya jumla ya mafuta kwa miezi mitatu na kuamuru Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo na mwenyekiti wake wa bodi wafikishwe kortini.
Lakini katika muda wa saa 48 tu, baada ya hatua hiyo ambayo iliungwa mkono na nchi nzima, Ewura ilibadilisha msimamo na mwelekeo wake na kutangaza kupandisha tena bei ya mafuta hayo ya petroli, dizeli na taa kwa asilimia tano.
Hatua hiyo ya Ewura, ilisababisha hasira ya Serikali yenyewe, Bunge, wabunge na wananchi kwa jumla.
“Ulichofanikiwa kufanya Masebu ni kuharibu kabisa mamlaka na madaraka ya Ewura. Hii ni taasisi ambayo ilikuwa imeanza kujijengea heshima kubwa kwa wananchi kwa kuchukua hatua mwafaka, na sasa mmevuruga kabisa heshima hiyo ya Ewura.
“Kwa kuvuruga heshima ya taasisi hiyo mmezitia doa siasa za nchi yetu,” waziri mmoja alimwambia ana kwa ana Masebu katika mkutano huo.
Masebu alijaribu kujitetea kwa kusema kuwa upandishaji huo wa bei ya mafuta uliofanywa na Ewura kwa mujibu wa Sheria na kwa mujibu wa makubaliano ya kuangalia upya bei kila baada ya wiki mbili kwa sababu mafuta huingizwa nchini kutoka Uarabuni kila baada ya wiki mbili.
Lakini Masebu aliambiwa kuwa hakuna mafuta yoyote yaliyoingizwa nchini tangu mvutano ulipoanza kati ya Ewura na kampuni za mafuta baada ya tangazo la kupunguza bei ya mafuta la Agosti Mosi, mwaka huu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ni mafuta yapi yameingia nchini kutoka Uarabuni katika wiki mbili zilizopita kwa sababu katika muda wote kwanza ulikuwepo mgomo wa kampuni za mafuta uliokolezwa zaidi na kampuni zile kubwa nne.
“Katika kipindi hiki, hakuna mafuta yaliyoingia nchini kwa sababu mafuta yalikuwepo kwenye matangi ya maghala na hayakuuzwa. Sasa Mkurugenzi anatuambia mafuta haya mapya yametoka wapi?” Alihoji waziri mmoja na kuongeza;
“Walichofanya Ewura ni kupandisha bei ya mafuta ambayo yalikuwa yamekwishafika nchini kabla ya mzozo kuanza mwanzoni mwa Agosti mwaka huu,” alisema waziri huyo.
Masebu alipojaribu kujitetea kuwa kwa taratibu za Ewura ni lazima bei za mafuta zipitiwe upya kila baada ya wiki mbili, waziri mwingine aliingia kati na kumwuliza:
“Mnapitia tu hata kama hakuna mafuta mapya yaliyoingizwa nchini kama ilivyotokea katika wiki mbili zilizopita? Mnafanya kazi kama mashine bila kutilia maanani hali halisi?” Alihoji.
Waziri mwingine alionya kuwa vitendo vya Ewura katika wiki mbili zilizopita vililenga kuyumbisha nchi na kuipeleka pabaya bila sababu za msingi.
“Inaelekea nyie Ewura mnahangaika zaidi kutetea maslahi ya wafanyabishara kuliko maslahi ya wananchi wetu,” alisema Waziri huyo.
No comments:
Post a Comment