Friday, August 12, 2011

Wabunge kataeni ufadhili huu

TUNAANDIKA kumpongeza mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine kwa kitendo chake cha juzi cha kukataa kujumuika na wabunge wengine kwenye ‘lifti’ ya ndege zilizokodishwa na kampuni ya Barrick kwenda kwenye mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

Lengo la safari hiyo ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni kwenda kuona iwapo mgodi huo umetekeleza ahadi yake ya kuboresha mazingira kufuatia tukio la mwaka juzi ambapo wanavijiji wengi walidhurika kwa sababu ya sumu kutoka mgodi huo kuingia katika mto Tingite ambao maji yake hutumiwa na vijiji kadhaa.

Kama lengo la safari hiyo ni hilo, haingii akilini kwamba mgodi huo huo ambao wabunge wanakwenda kuuchunguza kama umechukua hatua za kuwalinda wanavijiji wanaouzunguka dhidi ya sumu unaozalisha, ndio huo huo unaowakodishia ndege na kugharimia safari hiyo nzima.

Tuonavyo sisi, jambo hilo halina tafsiri nyingine yoyote mbali ya kwamba ni rushwa itolewayo na mgodi huo kwa wabunge ili warejee Bungeni Dodoma wakiwa na ripoti nzuri kuhusu Barrick; hata kama walichokiona huko hakiridhishi.

Ndiyo maana tumeshawishika kumpongeza Mbunge Nyangwine kwa kukataa ‘lifti’ ya Barrick kwenda Nyamongo; maana hakika angeonekana msaliti kwa wananchi wa jimbo lake hilo; kama ambavyo baadhi yetu tunavyowaona hivi sasa wabunge hao waliokubali kugharimiwa safari hiyo na mgodi wanaokwenda kuuchunguza.

Kwa hakika, tunashangaa na hatuelewi ni vipi Spika Anne Makinda aliruhusu safari hiyo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ifadhiliwe na mgodi huo inaokwenda kuuchunguza. Na hapa, tunaingiwa pia na shaka juu ya ufadhili huo unaanzia wapi na unaishia wapi.

Labda tukumbashane kwamba Bunge lipo kwa ajili ya maslahi ya wananchi, na hivyo safari hiyo ilipaswa igharimiwe yote na Bunge lenyewe; yaani fedha za walipa kodi nchini; badala ya kufadhiliwa na kampuni hiyo ya Barrick ambayo tayari ina migogoro kibao na wanavijiji wanaoishi katika vijiji vinavyoizunguka migodi yao. Kwa walichokifanya wabunge hao, ni kukaribisha migongano ya kimaslahi inayoweza kutia dosari utendaji wao ndani na nje ya Bunge.

Ni matumaini yetu kwamba ufadhili wa aina hiyo hautakubaliwa tena na Bunge letu - uwe unatoka kwa Barrick au kampuni nyingine yoyote.

Chanzo: Raiamwema

No comments: