BEI ya bidhaa za petroli imeshuka kuanzia leo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza jana, huku ikifunga biashara ya ghala la kuhifadhi mafuta la Kobil na vituo viwili vya mafuta.
Kushuka kwa bei hiyo kumefanywa na mamlaka hiyo baada ya kupandisha bidhaa hizo wiki mbili zilizopita hali iliyozua manung’uniko makubwa kutoka kwa walaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema Dar es Salaam jana kuwa kuanzia leo, petroli bei ya kikomo kwa Dar es Salaam itauzwa Sh 2,070 kutoka Sh 2,114 iliyokuwa inauzwa hadi jana.
Dizeli itauzwa kwa Sh 1,999 badala ya Sh 2,031 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,980 kutoka Sh 2,005.
Mikoani, bei ya kikomo pia itateremka kuanzia leo kulingana na umbali wa mkoa na bei ya juu ya kikomo itakuwa mkoani Kagera katika Wilaya ya Karagwe na Kigoma katika Wilaya ya Kigoma ambapo petroli lita moja itakuwa Sh 2,301, dizeli Sh 2,230 na mafuta ya taa Sh 2,211.
Bei iliyokuwepo mpaka jana ambayo ilitangazwa na Ewura wiki mbili zilizopita na kulalamikiwa na wananchi ni ya petroli kuuzwa kwa Sh 2,114 kutoka Sh 2,004, dizeli ikauzwa Sh 2,031 kutoka Sh 1,911 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh 2,005 kutoka Sh 1,860.
Masebu alifafanua kuwa bei hizo zimeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Kwa bei mpya, inaonesha kuwa petroli imeshuka kwa Sh 44. 55, dizeli Sh 31.99 na mafuta ya taa yameshuka kwa Sh 25.62.
Katika soko la dunia, petroli imeshuka kwa dola 43.33 kwa pipa, dizeli imeshuka kwa dola 30.04 na mafuta ya taa yameshuka kwa dola 27.69.
Masebu alisema bei ya mafuta katika soko la ndani zingeshuka zaidi kama thamani ya Shilingi ya Tanzania isingeendelea kuporomoka dhidi ya Dola ya Marekani.
Dola ya Marekani ndio inatumika katika ununuzi ya bidha za mafuta kwenye soko la dunia.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Dola moja ya Marekani katika soko la rejareja ilikuwa inauzwa kati ya Sh 1,616 na 1,630 hali inayoonesha kuwa sarafu hiyo inazidi kushuka thamani dhidi ya Dola.
Ewura imeendelea kutetea fomula mpya kuwa bado inaleta unafuu mkubwa kwa mlaji.
“Bei za rejareja na jumla zingepanda zaidi endapo fomula ya zamani ingeendelea kutumika,” alisema bosi huyo wa Ewura.
Alisema iwapo fomula za zamani ingeendelea kutumika, petroli kwa bei ya rejareja ingeuzwa Sh 2,249, dizeli Sh 2,179 na mafuta ya taa yangeuzwa kwa Sh 2,161.
Kwa upande wa bei ya jumla kwa kutumia fomula ya zamani, petroli ingeuzwa Sh 2,181, dizeli Sh 1,106 na mafuta ya taa yangeuzwa Sh 2,089.
Katika mazungumzo yake ya jana, Masebu aliishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kwa kutambua mchango wa Ewura wa kupanga bei kwa kuzingatia fomula mpya na mabadiliko inayoyafanya kila baada ya wiki mbili.
Katika maoni ya kamati hiyo yaliyotolewa na Mwenyekiti wake, Dk. Abdalah Kigoda wakati wa kuchangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha, alisema Serikali ilitakiwa ifanye mkakati wa makusudi wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya utaratibu wa bei za mafuta katika soko la dunia ambazo Tanzania haizipangi.
“Kwa kweli tunaishukuru kamati hii kwa kutambua juhudi zinazofanywa na mamlaka yetu, hii inaonyesha kuwa tunafanya mambo haya kama timu,” alisema Masebu.
Wakati huo huo, Ewura jana imetangaza kuvifungia vituo viwili kwa sababu mbalimbali pamoja na ghala moja. Ghala la Kampuni ya Kobil lililoko Kigamboni limefungiwa baada ya kubainika kuwa petroli iliyohifadhiwa humo haikidhi ubora uliowekwa na mamlaka hiyo.
Vituo vilivyofungiwa ni pamoja na cha Hass wilayani Magu Mkoa wa Mwanza, ambacho kimefungiwa baada ya kukaidi amri ya Ewura ya kukifungia na kuweka uzio; lakini wamiliki wake wakaondoa uzio huo na kuendelea kufanya biashara.
Pia kituo cha Petro kilichoko Mafinga wilayani Mufindi katika Mkoa wa Iringa kimefungiwa baada ya kuwazuia maofisa wa Ewura kuchukua sampuli za mafuta za kituo hicho.
No comments:
Post a Comment