WABUNGE wanawake wamelitaka shirika la UN-Women kutekeleza nia yake ya kuwasaidia wanawake kwa wakati.
Walitoa mwito huo hivi karibuni mjini Dodoma wakati wa semina iliyoandaliwa kwa ajili ya kuelezea masuala mbalimbali yanayotekelezwa na shirika hilo.
Walisema imebainika kuwa shirika hilo limekuwa likijitokeza kuwasaidia wanawake wanaohitaji msaada dakika za mwisho wakati wakiwa wametatua matatizo yao au kuchukua hatua nyingine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia alisema licha ya kuomba msaada wa mafunzo kutoka katika shirika hilo mapema kwa ajili ya masuala ya kampeni, halikuwasaidia chochote kutokana na ukweli kuwa lilijitokeza dakika za mwisho wakati wanawake wagombea wakiwa wamemaliza sehemu kubwa ya maandalizi yao.
“Kwa kweli mimi sioni kama UN-women linatusaidia kwa sababu mwaka jana kwa mfano lilikuja kutoa mafunzo mwishoni wakati uchaguzi wa madiwani ulioshirikisha wanawake ukiwa umemalizika. Mafunzo yao kwa kweli hayakuwa na msaada kwa sababu yalitolewa yakiwa yamechelewa,” alisema Ghasia.
Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, alisema, “Hata msaada wa kifedha nao pia kuupata kutoka kwao ni tatizo sasa sijui labda watueleze wapo kwa ajili ya nani na ni kwa nini wanakuja kutuletea misaada hiyo ikiwa imepitwa na wakati?”
Mbugne wa Viti Maalumu, Regia Mtema (Chadema) alihoji sababu ya shirika kuishia kutoa mafunzo yake kwa wanawake waliokwishapata ufahamu hususan wabunge wakati waliopo vijijini ambao ndio wenye kuhitaji zaidi misaada ya UN Women hawawaoni.
Alisema asilimia kubwa ya wanawake wanaoandamwa na athari za mila mbaya , mfumo dume na unyanyasaji wa aina mbalimbali wa kijinsia wapo vijijini lakini shirika hilo haliwafuati na kudhani linamsaidia mwanamke wa Tanzania kwa kuonana na wachache wa mijini ambao hata hivyo wanauelewa mpana wa namna ya kuepuka au kupambana na unyanyasaji huo.
Akitoa maelezo kwa niaba ya shirika hilo, mwezeshaji wa semina hiyo ambaye pia ni Meneja wa Programu, Anna Falk alisema lengo lao la dhati ni kuwasaidia wanawake.
Alisema huchelewa kujibu maombi yao kwa vitendo kutokana na kucheleweshewa fungu au mahitaji ambayo yanakuwa yanaombwa na wanawake hao kutoka kwa mfadhili wao.
Alisema wao ni shirika dogo na hawana uwezo wa kifedha kiasi cha kutoa misaada inapotakiwa. “Lakini hilo tumeliona sasa tutajaribu kuwahimiza wanaotupatia fungu kufanya hivyo mapema ili nasi tuwe na faida kwenu wanawake wa Tanzania,” alisema.
Alisema UN-Women ina watendaji wachache hivyo ni vigumu kufika hadi vijijini kwenye wanawake wanaoathiriwa na vitendo vya unyanyasaji.
“Tunajua tukiwapa mafunzo wanawake viongozi tunakuwa tumewafundisha wanawake wa vijijini pia, lakini hata hivyo tutaangalia namna ya kulitafutia jibu pendekezo hilo,” alisema wakati akijibu hoja Waziri Ghasia.
No comments:
Post a Comment