Na Privatus Karugendo
“UKISEMA, ‘ndiyo’, basi, iwe ‘ndiyo’, ukisema ‘siyo’, basi iwe kweli ‘siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu” (Mathayo 5:37).
Haya ni maneno ya Yesu Kristu wa Nazareti wakati akiwafundisha wafuasi wake. Somo lenyewe lilikuwa juu ya mtu kuwa na msimamo, uadilifu na uaminifu. Kwamba mtu ukiamua kuisimamia “ndiyo”, basi aisimamie bila kutetereka, na akiamua kuisimamia “siyo” vile vile aisimamie bila kuyumba. Na kwamba mtu akiisimamia “ndiyo” ukijua kwamba ni “siyo” ni unafiki na uovu. Vilevile akiisimamia “siyo” ukijua kwamba ni “ndiyo” ni unafiki na uovu!
Kwa maneno mengine, mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu hawezi kujiwekea kikao cha kujadili “ndiyo” anayoijua ni “ndiyo” na “siyo” anayoijua ni “siyo”. Mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu.
Hii ni falsafa ya Yesu wa Nazareti aliyowafundisha wafuasi wake. Bila kuingilia masuala ya imani, mtu yeyote anaweza kuitumia falsafa hii katika maisha yake; maana ina msingi chanya wa kuendesha maisha katika jamii yoyote ile.
Wakati Yesu wa Nazareti akifundisha falsafa hii ya msimamo, uadilifu na uaminifu katika jamii ya Wayahudi; jamii yenyewe ya Wayahudi ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha mabadiliko. Watawala waliabudu madaraka na mali; walipinduana katika utawala, walisalitiana na wakati mwingine waliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Unafiki na uovu viliongoza maisha yao ya siku kwa siku. Kuna wanaojenga hoja kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa mwanasiasa aliyeguswa na hali ya maisha ya watu katika jamii yake ya Wayahudi. Kwa wale wanaoipokea imani ya Kikristu bila kuchimba kwa kina historia, theolojia na elimu ya Biblia, watasema mimi ni mzushi; lakini ukweli utabaki pale pale kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa katika jamii fulani na kuishi akizungukwa na historia, utamaduni na desturi za watu wake.
Ingawa sisi hapa Tanzania hatujafikia hatua ya kupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, hatujabaguana na kushindana kama walivyokuwa wana wa Israeli, unaweza ukafananisha hali ya Uyahudi ya wakati ule na hali ambayo taifa letu la Tanzania linapitia hivi leo.
Unafiki na uovu vinawaongoza watawala wetu; hivyo tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Tunahitaji viongozi watakaosema “ndiyo” wakimaanisha “ndiyo” na watakaosema “siyo” wakimaanisha “siyo”. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba viongozi wetu wanasema “ndiyo” wakimaanisha “siyo” na wanasema “siyo” wakimaanisha “ndiyo”.
Tuna viongozi ambao wanacheka kumbe wanalia, na ambao wanalia kumbe wanacheka! Tuna wabunge wanaosinzia Bungeni wakisingizia kutafakari. Wakibanwa zaidi wanasema huo ni uchochezi wa waandishi wa habari! Wabunge wetu walipambana kufa na kupona waitwe “Waheshimiwa” na kusahau kabisa kwamba waheshimiwa ni wananchi waliowatuma Bungeni.
Katika familia zetu, katika jamii zetu na katika taifa letu, tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Hatuwezi kujenga familia, jamii na taifa imara bila kuwa mbali na unafiki na uovu. Bila kujenga utamaduni wa “ndiyo” kuwa ni “ndiyo na “siyo” kuwa ni “siyo”, hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo bila kuizingatia falsafa hii.
Jambo hili ni muhimu; maana jinsi mambo yanavyokwenda ni kama vile sisi (kama taifa) hatujakubaliana “ndiyo” ni nini na “siyo” ni nini. Na kama makubaliano haya yapo, kitu ambacho sina imani kubwa nacho, basi ni lazima tukubaliane kwamba msimamo, uadilifu na uaminifu vimezikwa kaburi moja na Azimio la Arusha!
Huu ni mjadala mrefu ambao ninafikiri unahitaji makala inayojitegemea. Ni mjadala ambao ni lazima kuendeshwa kwa uangalifu mkubwa ili kukwepa ushawishi wa kuichukulia falsafa yenyewe kama kichocheo cha udini.
Watanzania wakitaka kupindisha ukweli wanauweka udini mbele. Wakati mwingine udini ni silaha ya kuifumba midomo ya watu na kulenga kuwatenga Watanzania kwenye makundi ili wasishirikiane kudai haki zao kutoka kwa watawala. Hivyo falsafa hii ya “ndiyo” na “siyo” nitaijadili wakati muafaka ukifika.
Hata hivyo, hoja ninayoijenga leo kwenye makala hii ni kule kupoteza muda mwingi na fedha nyingi kuijadili “ndiyo” ambayo hata kama watu wengi wanajua na kuamini kwamba ni “siyo” lakini watawala na mfumo uliopo unaamua kwamba ni “ndiyo”.
Tunahitaji muda kuyashughulikia mambo mengine mengi; maana taifa letu bado ni masikini. Tunahitaji fedha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo. Kwa nini basi muda huu unaohitajika hivyo na fedha hizi za maendeleo vitumike kujadili “ndiyo”?
Tunalalamikia ufinyo wa bajeti. Kila wizara inalalamika kupata mgawo kidogo kutoka kwenye mfuko wa taifa letu. Watanzania walio wengi wanashauri wizara zote bajeti zao zipanuliwe na kuongezewa fedha nyingi, na hasa fedha inayowalenga Watanzania wanaoishi pembezoni.; badala yake tunawaweka wabunge pale Dodoma kwa kipindi cha miezi miwili, wakitumia fedha za Watanzania.
Siku za kuishi Dodoma zikipunguzwa, ni wazi fedha nyingi zitapatikana ili ziongezewe kwenye bajeti za wizara mbalimbali. Ingawa sina takwimu za fedha wanazolipwa wabunge wetu, ni wazi siku zaidi ya 30 zikipunguzwa kwenye siku ambazo wabunge wanalazimika kuishi Dodoma, tutapata fedha ya kutosha kufanya miradi mingine ya maendeleo.
Bajeti yetu ya taifa inayojadiliwa kila baada ya mwaka mmoja kwa utawala na mfumo uliopo sasa ni “ndiyo”. Ijadiliwe isijadiliwe ni lazima ipitishwe. Hata pale inapoonekana wazi wazi kwamba kuna ulazima wa kubadilisha kama inavyojionyesha kwenye bajeti ya mwaka huu ya Nishati na Madini, bado bajeti inapitishwa hivyo hivyo; maana wabunge wa chama tawala ni wengi kuliko wa upinzani.
Wakati mwingine inasikitisha zaidi bajeti inapopitishwa hata bila kujadili vifungu vyote kwa kisingizio cha kukimbizana na muda. Hoja ni kwamba kwa nini wabunge wakae Dodoma miezi miwili wakijadili “ndiyo”. Ni busara gani inayotumika? Kama lengo ni wabunge kuibariki bajeti, kwa nini bajeti isisomwe kwa siku mbili au tatu na kupitishwa ili kuokoa muda na fedha?
Bunge letu lina utamaduni wa kupitisha mambo kwa swali: Wanaokubali waseme “ndiyo” na wasiokubali waseme “siyo”. Kufuatana na utawala na mfumo tulio nao kwa sasa hivi, jibu ni “ndiyo” hata pale ambapo na watoto wadogo wanaweza kutambua kwamba “ndiyo” ni “siyo”, na wakati mwingine sauti za wabunge wanaosema “siyo” ni nyingi zaidi ya wale wanaosema “ndiyo”, Spika na wasaidizi wake watasema wa “ndiyo” wameshinda; maana vichwani mwao hakuna kitu kingine zaidi ya “ndiyo”.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment